Habari za Punde

BALOZI SEIF - ZANZIBAR KUNUFAIKA KWA MENGI NA USHELISHELI

· Ni katika utalii, ajira, soko la bidhaa

Na Juma Khamis

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema wasomi wa Zanzibar wanaweza kufaidika na nafasi za ajira za ualimu na udaktari nchini Seychelles.

Alisema Seychelles inahitaji idadi kubwa ya walimu kujaza nafasi katika chuo kikuu chao pamoja na madaktari wa kutoa huduma katika hospitali zake, hivyo Zanzibar imeombwa kutafuta wataalamu wa kujaza nafasi hizo.

Balozi Seif aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari uwanja wa ndege wa Zanzibar wakati akirejea kutoka ziara yake ya siku sita nchini Seychelles.

Akizungumzia suala la biashara, Balozi Seif alisema wafanyabiashara wa Zanzibar wana nafasi kubwa ya kufanyabiashara na Seychelles kwa kuwa visiwa hivyo vimekuwa vikiagiza kwa wingi vyakula kutoka nje.

“Sisi tumekuwa tukiangalia kufanya biashara mbali zaidi wakati Seychelles ina fursa nyingi za biashara ambazo wafanyabiashara wetu wanaweza kuzitumia,” alisema.

Akigusia sekta ya uvuvi, alisema Seychelles inategemea kwa kiasi kikubwa sekta hiyo ambapo imeanzisha viwanda vya kusindika minofu ya samaki na kusisitiza kwamba amewaalika wataalamu wa sekta ya viwanda hivyo, kuja Zanzibar kuangalia uwezekano wa kuanzisha viwanda vya aina hiyo.

Kwa upande wa sekta ya nyumba, alisema Zanzibar inaweza kuiga mfano wa Seychelles wa kujenga nyumba za bei nafuu kwa makazi ya wananchi ambazo zitasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa ardhi.

“Seychelles imefukia sehemu ya bahari kujenga nyumba ambazo baadae huuzwa kwa wageni na sisi tunaweza kutumia maeneo yetu yalio wazi au hata kufukia sehemu ya bahari kule Nungwi kuanzisha nyumba kwa ajili ya makazi ya wananchi wetu,” alisema.

Kwa upande wa sekta ya utalii, Makamu wa Pili wa Rais alisema Zanzibar ina matamasha mengi ambayo yanaweza kuimarishwa zaidi kwa kuwaalika wageni kutoka mataifa mengine duniani kuja kujionea vivutio vya utalii viliopo hali ambayo itasaidia kuutangaza utalii wa Zanzibar kama ilivyofanikiwa Seychelles.

Aidha alisisitiza haja ya kuimarishwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.

Katika ziara hiyo Balozi Seif na ujumbe wake walipata fursa ya kufanya mazungumzo na Rais wa Seychelles, James Michael ambapo mazungumzo yao yalijikita zaidi katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara hasa katika mazao ya baharini, viungo, mbogamboga na malighafi nyengine kutoka Zanzibar.

Pia walizungumzia uwezekano kushirikiana katika kupambana na maharamia wa Kisomali katika pwani ya Bahari ya Hindi.

Balozi Seif pia alikutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais wa visiwa hivyo, Dany Faure pamoja na kupata fursa ya kutembelea mradi wa kiwanda cha usindikaji minofu ya samaki mjini Victoria na mradi nyumba za makazi.

Balozi Seif alikuwa Seychelles kwa mwaliko wa nchi hiyo, kuhudhuria tamasha kubwa la utalii "Carnival International de Victoria, 2011

1 comment:

  1. Mcheza kwao hutunzwa, kwanza hiyo huduma iwapo nyumbani ndio ziada mpeleke kwengine; si hivyo itakua kivuli cha mvumo anaefaidika alie mbali.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.