Habari za Punde

KAMATI YAWAHURUMIA WAFANYAKAZI ZANZIBAR LEO

Na Mwantanga Ame

KAMATI ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari ya Baraza la Wawakilishi, imeombwa kulitilia mkazo suala la kupatikana mtambo wa kuchapishia gazeti ikiwa ni hatua itayoweza kusaidia kupunguza gharama za uchapishaji gazeti la Zanzibar Leo.

Ushauri huo umetolewa na Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, Abdulla Mohammed Juma, wakati kamati hiyo ilipofanya ziara katika ofisi zake Rahaleo mjini Zanzibar.

Mhariri huyo alisema kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakibeba mzigo mkubwa wa uendeshaji wa gazeti hilo kunakosababishwa na gharama za uchapishaji kuongezeka kila siku kutokana na ukosefu wa mtambo wa kuchapishia magazeti Zanzibar.

Alisema gazeti hilo hivi sasa limekuwa likichapishwa Tanzania bara kwa ajili ya kufuata mitambo jambo ambalo limekuwa likichangia kuwepo kwa gharama kubwa katika shughuli za uendeshaji wa Shirika hilo na kulikwamisha kufikia lengo la kujitegemea.

Alifahamisha hali hiyo imekuwa ikilifanya Shirika hilo kutotimiza mahitaji ya watendaji wake kwa kulazimika kulipia madeni ya uchapishaji huku ikikabiliwa na madeni makubwa ya watumishi kushindwa kulipwa posho zao kwa wakati.

Alisema hivi sasa, Shirika hilo linadaiwa posho za wafanyakazi, jambo ambalo linaweza kuleta tatizo kutokana na wafanyakazi hao kutumia muda mwingi wakiwa kazini kunakosababishwa na mazingira ya kazi ya utengenezaji wa gazeti.

Mhariri huyo alisema tayari Shirika hilo limeshawasilisha Fomu ya Mradi Wizara ya Fedha kwa ajili ya kuomba fedha za kununulia mtambo huo, ambao pia utaokoa zaidi ya shilingi milioni 300 kwa mwaka ambazo hutumika kuchapishia Magazeti ya Shirika hilo.

Akijibu suala la kamati hiyo kwa nini wanashindwa kumudu gharama za uendeshaji wa moja kwa moja Shirika hilo na kulazimika kuitegemea Serikali, Mhariri huyo amesema ni kuanzishwa kwa Shirika hilo bila kupewa mtaji wowote na hadi sasa linatengewa ruzuku kama ilivyokuwa lilivyokuwa Zanzibar Leo, jambo inalolifanya kuendeshwa katika mazingira magumu.

Alisema ili kuondosha hali hiyo ni lazima serikali ilipatie mtaji wa kuanzia kufanya kama Shirika, vyenginevyo litaendelea kuwa Shirika jina na kuchapisha gazeti moja tu la Zanzibar Leo katika mazingira yanayoweza kusababishwa kushindwa hata kutoa gazeti hilo,iwapo hali itaendelea kama ilivyo sasa.

Alifahamisha watalazimika kuliangalia hilo kwa vile haiwezekani kwa gazeti hilo kuchapisha Idara ya Uchapaji, kwani mbali ya kutokuwepo mtambo pia taasisi hiyo ina majukumu mengi ya kuchapisha kazi za Serikali, ambapo huko nyuma ilishindwa kuchapisha magazeti ya zanzibar Leo ysiyo rangi kwa kutingwa na majukumu yake ya msingi, ambayo gazeti halimo.

Naye Mkuu wa Chumba cha Kompyuta Rabia Bakari na Mkuu wa Chumba cha Habari, Juma Masoud, walielezea ni lazima serikali iyaangalie matatizo ya Shirika hilo kwa kuona inalipatia mtaji pamoja na kuangalia maslahi ya wafanyakazi yalingane na uendeshaji wa Shirika.

Ikitoa shukrani zake kamati hiyo iliwapa pole watumishi wa Shirika hilo kutokana na kufanya kazi zao kizalendo kutokana na kuvumilia mazingira ya kazi yao huku wakikosa kulipwa maposho yao kwa wakati.

Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake Asha Bakari Makame, iliwasihi wafanyakazi hao kuendeleza uzalendo na kuahidi kilio chao watakifikisha katika sehemu husika ili kuweza kufanyiwa kazi.

Alisema lengo la kamati hiyo ni kuona kila idara iliyopo chini yake inafanya kazi kwa tija kwa lengo la kuiwezesha serikali kupata maendeleo kwa vile vyombo vya habari ni moja ya sehemu nyeti ya serikali na yenye uwezo mkubwa wa kuongeza mapato ya serikali.

Mapema Kamati hiyo ikitembelea Televisheni Zanzibar na Sauti ya Tanzania Zanzibar, imepokea kuwapo kwa matatizo mbali mbali ikiwemo mitambo na vifaa muhimu vya kufanyia kazi ikiwa pamoja na maslahi duni ya wafanyakazi.

Watendaji katika Idara hizo Ali Muhsin kwa Televisheni Zanzibar na Hassan Vuai kwa Redio Zanzibar, walisema wengi wa watumishi wamekuwa wakikabiliwa na maslahi madogo huku vifaa vya kufanyia kazi vikiwa duni na vimeshapitwa na wakati.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, wakati akitoa shukrani katika majumuisho ya ziara ya Kamati hiyo katika idara ziliomo Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, iliwataka watendaji kutekeleza majukumu yao vyema huku ikishirikiana na taasisi nyengine zitazokuwa na uhusianao katika utoaji wa huduma zao.

Mwenyekiti huyo alilitaja eneo mojawapo ambalo watapaswa kuliangalia ni la kuweka mazingira bora ya utendaji katika taasisi zote hasa katika maeneo yenye kuleta tija kubwa ya taifa ikiwemo sekta ya utalii.

Aidha Mwenyekiti huyo ameipa kipindi cha miezi mitatu Idara ya Makumbusho kufanya mabadiliko ya ofisi zake kwa kuwa na samani kutokana na hivi sasa kutokuwa na thamani za aina yoyote huku jengo wanalotumia likiwa lenye mipasuko.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.