Habari za Punde

UHARIBIFU WA MAZINGIRA WATISHA KASKAZINI, MICHEWENI

Na Haji Nassor, ZJMMC

MTAALAMU wa mazingira kutoka Idara ya Mazingira Zanzibar , Hamza Zubeir Rijali amesmea kwamba jamii itapaswa kujilaumu yenyewe endapo haitaona umuhimu wa kuyalinda, kuyatunza na kuyahifadhi mazingira ya nchi kavu, kwa vile huduma kadhaa ikiwa ni pamoja na maji safi na salama zinaweza kupotea baadae.

Alisema kwamba mazingira ya nchi kavu ndio chachu ya kupatikana kwa huduma mbali mbali za kijamii ,ikiwa ni pamoja na chakula, hewa, maji safi na salama na vivuli ambapo hilo kama halikupewa kipaumbele Zanzibar itaingia katika hasara kubwa.

Mtaalamu huyo alitoa rai hiyo jana ,Ofisini kwake Maruhubi mjini Zanzibar, alipozungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya hali halisi ya kimazingira ilivyo Zanzibar.

Rijali alisema shughuli kuu zinazofanywa na Wazanzibari wenyewe ambazo ndio adui wa uharibifu wa mazingira ya nchi kavu, ni pamoja na uchimbaji mchanga,mawe, matofali,ukataji wa miti, utupaji na kushindwa kudhibiti taka katika maeneo mbali mbali.

Alifafanua kwa sasa Kisiwa cha Unguja kinaongoza kwa shughuli hiyo ,hasa Mkoa wa Kaskazini ambako huko kumeshamiri uchimbaji wa mchanga usiozingatia kanuni na kusababisha hali kuwa mbaya na ya kutisha.

Aidha, Rijali aliitaja wilaya ya Micheweni na ukanda wa Mashariki wa Kisiwa cha Pemba, kwamba nako huko hali si nzuri kwa kuwepo kwa uchimbaji wa mawe, matofali pamoja na mchanga.

Aliongeza kuwa yote hayo yanaweza kudhibitiwa na kufanywa kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa mazingira, ambapo kunaweza kukaepusha hali mbaya ya sasa.

''Tatizo lililopo hapa ni kwamba sio kuzuia moja kwa moja lakini hawa wanaofanya shughuli hizi ni vyema wakakubali ushauri wanaopewa na wataalamu wa kimazingira ili kuepusha athari kubwa zaidi'', alifafanua.

Wakati huo huo, ripoti iliyotolewa na Idara ya mazingira ya mwaka 2004/2005 ilionesha hali 'halisi ya Mazingira ya Zanzibar' ilionesha kuwa kiasi cha hekta 500 za msitu wa maweni hukatwa kila mwaka hapa Zanzibar.

Aidha ripoti hiyo ilionesha kuwa ,asilimia 41 ya mbao zinazovunwa hutokana na msitu wa asili ya maweni na asilimia 51 hutokana na miti ya kigeni.

Hata hivyo, ripoti hiyo imeonesha kuwa mambo mbali mbali yemefanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa Mradi Endelevu wa Ardhi na Mazingira (SMOLE), pamoja na kuishawishi jamii kuanzisha jumuia za kiraia ili kuyatunza na kuyahifadhi mazingira.

Idara ya Mazingira Zanzibar siku hadi siku imekuwa ikipiga kelele kwamba suala la kulinda na kuhifadhi mazingira ni jukumu la kila mmoja na huku Idara hiyo ikiwa ndio msimamizi mkuu, kwa kutoa elimu kwa jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.