Na Halima Abdalla
WATU wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tafauti na wengine wawili kukamatwa kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya na pombe ya kienyeji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Azizi Juma Mohammed, amesema matukio hayo yalitokea Machi 18 majira ya saa 5:58 usiku katika maeneo ya Muembe makumbi, ambapo, Masoud Mganda Ame (18) aliokotwa akiwa ameshambuliwa vibaya kwa mawe kichwani na watu wasiojulikana na kusababisha kifo chake kwenye hosipitali kuu ya Mnazimmoja.
Kamanda Aziz, alisema marehemu alionekana na majirani akiwa katika hali mbaya karibu na eneo la nyumba anayoishi ndipo walipotokea wazee wake na kumpeleka hospitali ambapo alifariki muda mfupi baadae.
Alisema chanzo cha tukio hilo bado hakijafahamika na jeshi hilo limeanzisha upelelezi kuhusiana na tukio hilo.
Wakati huo huo, Kamanda huyo alisema katika mtaa wa Darajani mjini Unguja Machi 20 mwaka huu, mtu mmoja aliyejulikana kwa umaarufu Fide Kuu ambae umri wake haukupatikana alifariki baada ya kupigwa kigongo kimoja cha kichwa na Kaema Ramadhan Magoya (22) na kusababisha kifo chake mara alipofikishwa mahakamani.
Marehemu kabla ya kifo chake alipata majeraha makubwa ya kichwa alipofikishwa hospitalini alifariki dunia.
Kulingana na Kamanda Aziz, mauaji hayo yalitokana na watu hao wawili kugombana lakini akasema chanzo cha ugomvi huo hakijafahamika.Alisema mtuhumiwa wa mauaji hayo anatafutwa na polisi ili afikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Zanzibar linamshikilia mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Ali Mtwana Dachi (46) Mkaazi wa Ziwatuwe kwa kosa la kupatikana na kete 16 za dawa za kulevya baada ya kutiliwa mashaka na kupekuliwa mwilini mwake.
Tukio hilo lilitokea Machi 17 eneo la Soko kuu Mwanakwerekwe ambapo kwa sasa upelelezi unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa upelelezi.
Katika tukio jengine, mtu mmoja, Luti Simon Lazaro (29) Mkaazi wa Mwanyanya inadaiwa Machi 18, juzi alipatikana na dumu moja la lita 20 la pombe aina ya gongo nyumbani kwake Mwanyanya.
Mtuhumiwa kwa sasa amepewa dhamana na polisi na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Kamanda Aziz alitoa wito kwa wananchi kuwa karibu na Polisi yanapotokea matukio kama hayo na kuwa tayari kuwafichua wahalifu mara tu tukio linapotokea ili kusaidia jeshi la Polisi kuweka amani na utulivu na kulinda mali ya wananchi.
No comments:
Post a Comment