Habari za Punde

KATIBU MKUU WANAWAKE NA WATOTO AFARIKI

Dk. Shein aongoza mazishi

Na Mwantanga Ame

MAKATIBU Wakuu wa serikali ya Zanzibar na Wakurugezi, wamemlilia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Rahma Mohammed Mshangama aliyefariki dunia ghafla usiku wa kuamkia jana.

Katika mazishi hayo yaliyofanyika Mwanakwerekwe na kutanguliwa na sala katika msikiti wa Muembeshauri, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal waliwaongoza viongozi na wananchi.

Wakizungumza na Zanzibar Leo kwa nyakati tofauti Makatibu hao walisema kifo hicho kimewapa mshituko mkubwa na kwa upande wao kimeacha pengo katika Kamati yao ya Makatibu Wakuu, familia yake na serikali kwa jumla.

Taarifa iliyotolewa na Wizara yake ilisema, Katibu Rahma mwenye umri wa miaka 50, alifariki usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Mnazi mmoja ambapo alifikishwa usiku huo kutibiwa maradhi ya shinikizo la damu, lakini hapo awali alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Idara ya Habari Maelezo imeeleza, Rahma alizaliwa Aprili 1961, Mjini Zanzibar na ameolewa lakini hakujaliwa kupata mtoto ambapo jana alizikwa katika makaburi ya Mwanakwerekwe.

Akizungumza na Zanzibar Leo Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk. Khalid Mohammed, alisema msiba wa kiongozi huyo ni mkubwa kwani serikali imepoteza mtu muaminifu katika utumishi wake umma.

Alisema Rahma aliwahi kufanyakazi nae katika kipindi cha miaka minne na ameuona uzoefu wake wa kujituma na kuridhika jinsi dada huyo alivyokuwa akichapa kazi.

Alisema ndani ya Vikao vya Kamati ya Makatibu Wakuu kwa kiasi kikubwa mchango wake ulikuwa ni mkubwa kiasi ambacho uliwezesha kupatikana kwa malengo tofauti ya serikali.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Mshamu Abdalla Khamis alisema msiba huo umewahuzunisha kwani umeacha changamoto kadhaa katika utendaji wa kazi za wizara hiyo.

Alisema Katibu Rahma kabla ya kukutwa na mauti yake alimuaga anataka kuelekea Tanzania bara kwenye kikao, lakini asubuhi ya juzi alimuarifu kuwa hali yake si nzuri na kupatwa na mshituko baada ya kusikia kifo chake.

Nae Mkurugenzi huduma za Utibabu wa Mifugo Zanzibar, Dk.Yussuf Haji Khamis, ambaye alifanya kazi pamoja na Katibu Rahma, alisema kifo hicho kimemsikitisha kwani walipenda kufanya kazi nae kwa muda wote tangu wanaanza kazi katika Wizara ya Kilimo baada ya kumpokea kazini alipomaliza masomo yake ya kidato cha sita.

Alisema katika kipindi chote utumishi wake hakuwa na matatizo na aliweza kushirikiana na watendaji wenzake wanaume na wanawake hata pale alipokuwa akichukua masomo ya elimu ya juu alionekana kufanya vizuri.

Kwa mujibu wa Tarifa ya Idara ya Habari Maelezo imeeleza kuwa Katibu Rahma alifanya kazi katika Idara mbali mbali za serikali ikiwemo Wizara ya Kilimo, na Wizara ya Wanawake na watoto ambayo ameitumikia hadi kifo chake.

Idara hiyo ilisema Rahma alifanya shahada ya kwanza ya kilimo katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, ambapo shahada yake ya Uzamili alifanya katika chuo cha Reading cha nchini Uingereza ambapo alisoma masuala ya wanyama.

Mbali na shahada hizo marehemu pia alipata nafasi za kusoma kozi mbali mbali ndogo ndogo ndani nje ya nchi ambapo pia aliwahi kufanyakazi na mashirika mbali mbali ya kimataifa.

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.