Na Ramadhan Himid, POLISI
WANANCHI mbali mbali wamelalamikia makaburi ya Mwanakwerekwe kugeuzwa maficho ya wahalifu pamoja na kuchimbwa mchanga kiholela hali ambayo inatia hofu kwa wakaazi wanaoishi maeneo hayo.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alieleza hayo wakati akizungumza na kamati za Ulinzi na Usalama katika shehia za Mwanakwerekwe na Meli nne kwa lengo la kujadiliana na kupeana mikakati ya kupunguza uhalifu katika maeneo yao.
Wananchi hao walisema kwamba hivi sasa vijana wakorofi wameyageuza makaburi ya waislamu na wakristo ndio makaazi yao ya kuvuta bangi, kuchimba mchanga pamoja na kupora wapitanjia hasa akina mama nyakati za usiku.
Kadhia hiyo ya kuporwa vitu vya thamani makaburi ya Mwanakwerekwe imedumu kwa muda mrefu hivi sasa na kuwafanya wananchi wanaoishi kando kando ya makaburi hayo kuwa na hofu kutokana na uhalifu wanaofanyiwa.
Akizungumzia hali hiyo mkaazi wa shehia ya Meli nne, Juma Khamis Khatib alisema hali imeshakuwa mbaya kwani ikifika saa 2 usiku watu wengi wanalazimika kuzunguka masafa marefu kuliko kukatiza kwenye makaburi hayo kuhofia maisha yao au kuporwa mali zao.
Aidha Hassan Khamis mkaazi wa Ijitimai Mwanakwerekwe alisema uhalifu mwingi unaofanywa katika maeneo yao unafanywa na watu kutoka sehemu za mbali kutokana na mkusanyiko wa soko la Mwanakwerekwe ambako vijana wengi wamefanya ndio makaazi yao ya kulala.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mwanakwerekwe, Juma Sereweji alisema makaburi ya Mwanakwerekwe yamekuwa yakichimbwa mchanga hadi kukuta sanda za maiti na hiyo yote inatokana na jinsi watu walivyokuwa hawamuogopi Mwenyezi Mungu.
Mbunge huyo aliwataka wananchi hao kushirikiana katika kurejesha malezi ya vijana wao ambao wameporomoka kimaadili.
Nae Kamishna wa Polisi Mussa Ali Mussa alisema dawa ya kupunguza kero za kihalifu katika maeneo yao ni wananchi kujipanga na kuwa tayari kuunda kamati za ulinzi, Usalama na Ustawi wa jamii kwa kufanya vikao vya mara kwa mara, kutoa taarifa na kuzijadili kwa lengo la kupata ufumbuzi wa matatizo yao.
Vikao hivyo vya kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya Shehia ni mfululizo wa ziara za Kamishna Mussa Ali Mussa kuzungumza na wananchi mbali mbali katika Shehia zote za Unguja na Pemba kwa azma ya kupunguza uhalifu ambapo kwa sasa amemaliza ziara yake wilaya ya Mjini na kuendelea na ziara hiyo wilaya ya Magharibi Unguja
No comments:
Post a Comment