Habari za Punde

MAMA SHEIN AHIMIZA UTUNZAJI WA MAZINGIRA FUKWE ZA BAHARI

Na Mwanajuma Abdi

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein, amewataka wananchi kuhifadhi na kutunza ya mazingira ya fukwe za bahari kwani ni kichocheo kikubwa cha kuvutia watalii na kukuza uchumi.

Alisema hayo jana, alipokutana na wakulima wa mwani kutoka eneo la Hifadhi ya bahari ya kisiwa cha Mnemba na Ghuba ya Chwaka (MIMCA), katika mkutano wa siku moja uliofanyika katika hoteli ya Bwawani mjini hapa.

Mama Mwanamwema Shein alikabidhi zawadi ya shilingi 100,000 kwa kila kikundi ambapo jumla ya vikundi 22 vilikabidhiwa fedha hizo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja na wilaya ya Kati, katika Shehia ya Tumbatu Jongowe, Tumbatu Gomani, Uroa, Potoa, Fukuchani, Kilindi, Tazari, Kiwengwa, Ukongoroni, Kilimani, Kidoti na Matemwe.

Alisema kila mwanachi anapaswa kuwa mlinzi katika kutunza mazao ya baharini na fukwe ili kuendelea kuwa kivutio kwa watalii, ambapo wageni wanatoka kila upande wa dunia wanakuja kutembea nchini, hali ambayo inasaidia kukua kwa uchumi wa nchi na kuwaongezea wananchi kipato.

Alieleza kuna baadhi ya watu wachache wanaharibu mazingira ya mazao ya bahari na fukwe zake, hivyo alitoa wito kwa wakaazi wa ukanda wa pwani kuwa walinzi katika kupambana na uharibifu huo ili kuepusha na madhara ikiwemo mmong’onyoko wa fukwe.

Mama Mwanamwema Shein alisema kuna kilio kikubwa cha wakulima wa mwani kutokana na bei bado kuwa chini, aliwashauri waendelee kilimo hicho, ambapo Serikali imo katika juhudi za kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi ukizingatia tatizo hilo linatokana na hali ya soko la kimataifa.

Aidha aliwashajiisha wakulima hao kutafuta shughuli mbadala katika kukabiliana na ukali wa maisha kwa kuanzisha shughuli za ufugaji wa viumbe vya baharini na nchi kavu ikiwemo kuku, ng’ombe kwa ajili ya kupata tija zaidi.

Sambamba na hayo aliwataka wakulima hao kujikusanya pamoja na kujiunga katika vikundi vya kuweka na kukopa (SACCOS) kwa vile vina tija kubwa katika kupambana na umasikini na kuwaletea maendeleo endelevu, ambapo Serikali iko mstari wa mbele kuhimiza hilo, jambo ambalo limesababisha kuundwa kwa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wananchi Kiuchumi na Ushirika.

Mapema akisoma risala, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakulima wa Mwani wa eneo la Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mnemba na Ghuba ya Chwaka, Pavu Mcha Khamis alisema lengo la kuundwa kwa umoja huo ni kuwawezesha kuwa na sauti ya pamoja ya kutetea haki zao na kuendeleza kilimo cha mwani ili kuweza kuwaongeze zaidi.

Alifahamisha kuwa, matatizo yanayowakabili wanajumuiya hao ni pamoja na kuwa bei ndogo ya mwani mwembamba ukilinganisha na ugumu wa kazi, ambapo kwa kilo moja wanauza shilingi 250, sambamba na kuwa na uhaba wa vifaa vya kupandishia mwani ikiwemo kamba, tai tai na vyombo vya kupakilia wanapoutoa baharini.

Pavu alishauri Serikali kufanya utafiti wa kimazingira mwani mnene kwa vile baadhi ya maeneo haukubali ili waweze kupata tija kutokana na bei yake kuwa juu, ambapo kwa kilo moja ni shilingi 400.

Alisema kilio chao chengine ni uvamizi wa wawekezaji wa mahoteli katika maeneo ya kulimia mwani hali inayochangia kuwepo kwa migogoro kati ya wakulima wa zao hilo na wawekezaji.

Wakulima hao walimshukuru Mama Mwanamwema Shein kwa kuwapa fedha hizo, ambazo zitawasaidia katika kuendeleza kilimo hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.