Na Mwanaisha Muhammed, MCC
WALIMU wametakiwa waongeze jitihada kuhakikisha kuwa wanafunzi hao wanamaliza mada za masomo yao ili kiwango cha kufaulu kwa wanafunzi kiweze kuongezeka katika mwaka huu wa masomo.
Mshauri na mlezi wa skuli ya Al-hisan, Yusra Juma Khamis alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa skuli hiyo iliyopo iliyopo Magogoni.
Alisema endapo walimu wataongeza jitihada na kuhakikisha wanamaliza mada zao za masomo kwa wanafunzi hakuna sababu ya wanafunzi kufeli.
Mshauri huyo alisema pamoja na walimu kumaliza mada, lakini pia ni wajibu wa wanafunzi kuzingatia masomo yao na kuacha mchezo au kujihusisha na mambo yasiyowahusu.
Alifahamisha kuwa kwa sasa mashirikiano yapo ya kutosha kati ya walimu, wanafunzi na wazazi na pale yanapojitokeza matatizo hutafutiwa ufumbuzi wa pamoja.
Kwa upande wake Mkuu wa skuli hiyo, Rashid Dadi Haji amewataka wanafunzi hao wawe na mwamko zaidi wa ufuatiliaji wa masomo yao pindi wanaporudi majumbani.
Aliwataka wanafunzi hao kuacha kabisa kujiingiza katika vitendo viovu ambavyo vinaweza kuwaharibia maisha kwani wao tegemezi la hapo baadae.
Pia aliwaomba wazazi na walezi wa watoto hao wawafundishe na kuwalea katika maadili ya dini ya kiislam ambayo Mwenyezi Mungu ameyaridhia na kuachana na yale aliyoyakataza.
Sambamba na hayo ameiomba serikali iwaangalie wanafunzi kutokana na unyanyasaji wa makonda katika madaladala jambo ambalo linawafanya wachelewe kuingia madarasani na kurudi nyumbani usiku.
No comments:
Post a Comment