Habari za Punde

WANAHABARI WAPONGEZWA KUFANIKISHA UCHAGUZI

Na Mwantanga Ame

VYOMBO vya habari vya Zanzibar vimetajwa kufanya vizuri katika kutoa taarifa za uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliopita ambapo mgombea wa chama cha CCM, Dk. Ali Mohammed Shein aliibuka kuwa mshindi.

Wahadhiri waandamizi wa tasnia ya vyombo vya habari vya hapa nchini walieleza hayo jana wakati wakiwasilisha mada mbali mbali zilizokuwa zikiangalia suala la maadili ya vyombo vya habari katika uchaguzi Mkuu uliopita.

Waandamizi hao waliyaeleza hayo jana katika semina ya siku moja iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Ocean View, Kilimani Mjini Zanzibar.

Ali Saleh (Albato), akitoa mada yake juu ya mada ya maadili alisema uchaguzi uliopita vyombo vya habari vya hapa nchini vimeonesha uwajibikaji wa hali ya juu katika kufuata maadili ya fani ya habari ikilinganishwa na miaka iliopita.

Alisema asilimia kubwa ya taarifa zilizokuwa zikitolewa katika vyombo vya habari vya serikali na binafsi havikuonekana kuvunja maadili ya fani hiyo na badala yake viliweza kutoa taarifa zake kwa kuzingatia uzalendo zaidi bila ya kuwepo uchochezi uliosababisha uvunjifu wa amani.

Alisema ushahidi wa hilo ni kutokana na hata mabaraza yanayosimamia maadili ya fani ya habari hayakuweza kupokea kesi ya aina yoyote katika baraza la Habari Tanzania tawi lake la Zanzibar inayoonesha kuwepo kwa malalamiko yaliyowasilishwa na vyama kuvishtaki vyombo vya habari.

Hali hiyo alisema ilionekana kufanya vizuri zaidi katika upigaji wa kura ya maoni iliyosababisha kuwepo kwa mabadiliko ya katiba ya Zanzibar katika kuundwa kwa serikali ya Umoja wa kitaifa ambapo vyombo vyote vya habari vilitekeleza wajibu wa kuhamasisha jamii na kusababisha kutokea matokeo mazuri.

Eneo jengine alilolitaja kupata maafanikio ni katika uendeshaji wa kampeni za vyama ambapo walifanya kazi zao bila ya kuwapo kwa upendeleo na kutoonesha kuwapo kwa uhasama wa vyama bali waliandika zaidi sera za vyama badala kutukanana kwa tabia iliozoeleka hapo awali.

Kuhusu mahusiano ya kuifikia jamii alisema sehemu kubwa ya vyombo vya habari viliweza kuwafikia na kuwawezesha kutoa maoni yao, huku wengine waliweza kuvifikia vyombo hivyo bila ya kupata matatizo kwa kuelezea mitazamo yao.

Akitoa sababu ya kuwepo kwa mabadiliko hayo, Albato alisema yamechangiwa na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa na viongozi wakuu wa nchi waliopita akiwemo rais Mstaafu Amani Abeid Karume, na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad.

Alisema tangu kuwepo kwa maridhiano hayo yameweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa sekta ya habari katika kuripoti taarifa za uchaguzi kwa kuzuiya kuwapo kwa hisia za kisiasa haata kwa wale ambao walionekana hapo awali kujawa na jazba wakiwa kazini.

“Vyombo vya habari vya serikali asilimia 90 waligeuka na kusaidia kura ya maoni kufanikiwa waliipenda nchi yao na kujawa na uzalendo zaidi” alisema mtoa mada huyo.

Nae mtoa mada iliyokuwa ikihusiana nafasi ya ushiriki wa wadau katika mchakato wa uchaguzi kwa vyombo vya habari John Mireny, alisema ingawa baadhi ya vyombo vya habari viliweza kufanya vizuri lakini vilionekana kutawaliwa na njaa kwa kutumiwa na vyama kufanya biashara zaidi.

Akitoa mfano alisema baadhi ya vyombo vya habari vilikubali kuuza kurasa za mbele kwa kutoa toleo maalum na kuweza kufunika taarifa za wagombea wa vyama vyengine ikiwa ni ujanja wa biashara jambo ambalo lilionesha wazi kuendekeza njaa ya biashara.

Mapema mtoa mada ya maadili ya vyombo vya habari katika uchaguzi Mkuu, Ali Rashid, waandishi wa habari walioshiriki katika mchakato wa uchaguzi Mkuu bado wanahitaji kupewa sifa kutokana na kazi yao nzuri waliyoifanya.

Alisema elimu waliyoitoa kupitia vyombo vyao kwa kiasi kikubwa iliiwezesha jamii kudumisha amani na utulivu katika uchaguzi uliopita jambo ambalo limeufanya kuwa huru.

Wengi wa washiriki katika mjadala huo walieleza kuwa ipo haja ya kuwepo kwa muendelezo wa kutoa taarifa za uchaguzi bila ya upendeleo, jambo ambalo linaweza kusaidia kufanya vizuri zaidi ikiwa pamoja na kuundwa kamati maalum ya Zanzibar itayoweza kusimamia kazi za waandishi wa habari katika uchaguzi Mkuu ujao.

Semina hiyo ya siku moja imeandaliwa na Tume ya Utangazaji ya Zanzibar kwa ufadhili na ushirikiano na UNDP

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.