Habari za Punde

BODI KUZISHUGHULIKIA HOTELI ZENYE KUTOA TIBA

Na Fatma Kassim, Maelezo

BODI ya Ushauri ya Hospitali Binafsi imewataka wamiliki wa hoteli za kitalii nchini kufuata utaratibu wa kisheria wanapotaka kufungua sehemu ya utoaji tiba kwenye hoteli zao.

Hatua ya Bodi hiyo imekuja kufuatia baadhi ya hoteli za kitalii hapa nchini kufungua hospitali ambazo zimekuwa zikitoa huduma ya kutolea tiba kwa wafanyakazi wa hoteli hizo.

Msaidizi Mrajis wa Bodi hiyo Dk. Shaaban Seif Mohammed alisema hoteli zenye hospitali zenye kutoa huduma kwa wageni na wafanyakazi ni kinyume na sheria.

Alifahamisha kuwa Bodi yake itafanya msako wa kuzitembelea hoteli zote na wakigundua hospitali ndani ya hoteli hizo ambazo hazisajiliwa kutoa huduma watazifungia.

Alisema kusajiliwa kwa hospitali kunasaidia kutambua wafanyakazi wanaotoa huduma kuwa ni wenye sifa pamoja na huduma zinazotolewa kuwa ni zenye ubora na sio kubahatisha kwani afya za wanadamu zinahitaji uangalifu wa hali ya juu.

Wakati huo huo Bodi hiyo imeifungia Kiembesamaki ‘Dispensary’, baada ya kubainika kuwepo kwa uchafu ndani na nje pamoja na kuwa haina wafanyakazi wa kutosha wa kutoa huduma katika hospitali hiyo.

Alisema katika hospitali hiyo wanamtumia muuguzi kama ni daktari ambae anatibu wagonjwa jambo ambalo si sahihi na linahatarisha afya za wananchi.

Aliwataka wananchi kutoitumia hospitali hiyo kwa wakati huu mpaka pale watakaporekebisha kwa kutafuta daktari, pamoja na kufanya usafi ili kutoa huduma zinazostahiki kwa jamii.

Mapema Bodi imezifungulia hospitali ya Altabibu ‘Dispensary’ iliyopo maeneo ya Magogoni, Sanasa ‘Dispensary’ iliyopo maeneo ya Meli nne pamoja Fayu Clinic iliyopo Amani baada ya kukamilisha taratibu zote zinazotakiwa na Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi.

Awali Hospitali hizo zilifungiwa kutokana na kuwa hakuna wafanyakazi wa kutosha, uchafu pamoja wafanyakazi wasiokuwa na sifa wa kuendesha hospitali hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.