Na Mwanajuma Abdi
WAZIRI wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Zainab Omar amesema sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto ya ongezeko la mimba na ndoa za mapema kwa wanafunzi wa kike.
Waziri huyo alieleza hayo jana kwenye uzinduzi juma la elimu kwa wote liloloanza jana hadi Mei 8, ambapo ujumbe wa mwaka huu, ‘Elimu kwa watoto wa kike na wanawake ni haki na tuifanye kuwa ni haki’.
Alisema vikwazo vinavyowakabili mtoto wa kike ni ndoa za mapema na mimba za utotoni mambo ambayo huwanyima fursa ya kupata elimu ikilinganishwa na wenzao wa jinsia ya kiume.
Alieleza sheria ya mtoto iliyoandaliwa na Wizara yake pindi itakaposainiwa na Rais wa Zanzibar, masuala hayo yatafanyiwa kazi ipasavyo kwa kuondoshwa kasoro hizo zinazomkumba mtoto wa kike akiwa bado anamuda wa kuendelea na elimu ya lazima.
Waziri Zainab aliwataka wanafunzi kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kujilinda na gonjwa la UKIMWI na badala yake wajikite zaidi katika masomo ambayo ndio mkombozi kwa maisha ya baadae.
Alisema kauli mbiu ya mwaka huu, ichukuliwe kama kichocheo cha kuhakikisha elimu inayotolewa iwe sawa kwa jinsia na kwa rika zote kwa kuzingatia wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Alisema malengo makuu ya maadhimisho hayo ni pamoja na kufuta ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika kwa kupunguza idadi ya wanawake wasiojua kusoma, ambapo alisisitiza maendeleo ya mtoto ni kupanua upatikanaji wa elimu ya malezi na maandalizi.
Aidha alifahamisha kuwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Wizara ya Elimu, Mafunzo ya Amali ni pamoja na kuongezeka idadi ya wanafunzi waliojiunga na elimu ya maandalizi kutoka wanafunzi 13,156 kwa mwaka 2001 hadi kufikia wanafunzi 29,732 mwaka jana, sambamba na kuongezeka kwa uandikishaji hadi kufikia asilimia 33.9 mwaka 2010.
Alieleza Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima imejitahidi kufuta ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika kwa kupunguza idadi , ambapo mwaka 2009/2010 jumla wanakisoma 6,980 walikuwemo madarasani na watoto walioandikishwa darasa la kwana mwaka jana walikuwa ni 31,092.
Waziri Zainab alifafanua kwa upande wa sekondari kwa mwaka jana walikuwa ni wanafunzi 48,883 (sawa na asilimia 84.3) katika ngazi ya awali kidato cha kwanza na cha pili, ambapo kwa kidato cha tatu, nne na elimu ya ufundi kwa mwaka 2010/2011 wanafunzi 35,453.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mwanaidi Saleh alisema maadhimisho hayo yanayofanyika kimataifa duniani kote ambapo yametokana na UNESCO utasaidia kuwa kichocheoa kikubwa cha kufikia malengo ya elimu kwa wote mwaka 2015, ambapo kipao mbele wanawake na wasichana wapatie taaluma bora.
Akisoma risala katika juma hilo la elimu, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tunguu Zanzibar, Ruwaida Shaaban (mwenye ulemavu asieona) alishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa jitihadakubwa za kukuza elimu viwango vya elimu mjumuisho kwa kuwashirikisha wanafunzi wa kawaida na wenye ulemavu.
Alisema sera ya elimu ya mwaka 2006 ya elimu ya lazima kidato cha nne itasaidia kukuza kiwango cha taaluma pamoja na kuomba Serikali kuchapicha vitabu kwa alama ya nukta nundu ili viwasaidia wasiona kusoma bila ya matatizo kama wengine.
No comments:
Post a Comment