Donisya Thomas
KOCHA wa timu ya netiboli ya Polisi wanaume Zanzibar, Kibabu Haji Hassan, amesema, ukosefu wa umakini hasa katika kuzingatia muda kuliigharimu timu yake na kupelekea kukosa taji la ubingwa wa michuano ya Afrika Mashariki iliyomalizika wiki iliyopita visiwani hapa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, kocha huyo alisema, hicho ndicho kilichotokea na kuifanya timu hiyo kukosa taji hilo kwa mwaka wa pili mfululizo.
Polisi Zanzibar ililishikilia taji la Afrika Mashariki kwa miaka sita mfululizo na hivyo kuonekana kukosa mpinzani katika ukanda huo.
Aidha kocha huyo alieleza, chengine kilichowagharimu ni kwa wachezaji kuridhika baada ya kuongoza kwa tofauti ya magoli matano mbele ya wapinzani wao, hivyo kujisahau na kuanza kucheza bila ya kujilinda.
Akizungumzia hali nzima ya mchezo huo, kocha huyo, alisema, ulikuwa mzuri na kukisifu kikosi chake kwa kucheza vizuri licha ya kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza.
Alisema, wapinzani wao Kenya Prisons hawakuwazidi kimchezo ila wachezaji wake walikuwa wakizidiwa nguvu na zaidi nafasi ya GD na GK.
" Wachezaji wa Kenya wana nguvu sana kuliko wachezaji wetu, lakini pamoja na hayo walicheza vizuri na kushindwa ni sehemu ya mchezo", alisema Kibabu.
Kuhusiana na umri mkubwa kwa wachezaji wake, alisema, hilo halina ukweli kwani wachezaji wangali na umri mdogo na uwezo mkubwa wa kucheza, hivyo kuwataka wale wenye imani hiyo kuifuta mara moja.
" Wachezaji wako imara na hakuna mwenye umri wa kupindukia, ila mambo madogo yalitugharimu na baada ya mchezo, kocha wa Prisons alitufuata na kutuambia timu yetu ni nzuri sana na kuipongeza" alieleza.
Alisema sasa timu yake inajipanga kwa ajili ya ligi ya Zanzibar pamoja na kuhakikisha michuano ijayo ya Afrika Mashariki wanarudisha hashima kwa kubeba kombe hilo.
“ Sasa akili yetu tunaielekeza katika ligi ya Zanzibar na kuunda mikakati ili mwaka ujao tuweze kulirudisha taji tulilokuwa tunalishikilia kwa miaka sita mfululizo", alieleza, kocha huyo.
Polisi ilishindwa kutwaa ubingwa ikipitwa kwa goli moja dhidi ya Kenya Prisons baada ya kutoka sare ya kufungana magoli 44-44, katika mchezo wa fainali uliochezwa Mei 2 mwaka huu katika kiwanja cha Gymkhana mjini Unguja.
No comments:
Post a Comment