Habari za Punde

TAFITI ZITUMIKE SIO KUBAKIA MAKABATINI

Na Ramadhan Makame

MKUU wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha Zanzibar (ZIFA) kilichopo Chwaka, Kamal Kombo Bakari, amesema Zanzibar itapiga hatua kubwa za kimaendeleo endapo tafiti zitatumika kikamilifu badala ya kuishia
katika makabati ya ofisini.

Kamal alieleza hayo hoteli ya Visitors Inn, iliyopo Jambiani baada ya ufunguzi wa semina kuwafundisha njia za kisasa za ufanyaji utafiti walimu wa Vyuo vya Elimu ya Juu vya Zanzibar.

Alisema utafiti wowote unaofanywa, ni lazima ulenge kusaidia matatizo ya wananchi na hakutakuwa na maana ya kuendeleza kufanywa kwa tafiti kama zitaendelea kuishia kwenye makabati ya ofisini.

“Tafiti zinazofanywa zisaidie maendeleo ya nchi na uondoke utamaduni wa kuishia katika makabati ya maofisini”, alisema Mkuu huyo.

Mkuu huyo alisema kufanyika kwa mafunzo hayo kutasaidia kuamsha ari ya ufanyaji tafiti katika vyuo vya Zanzibar ambayo vimekuwa vikijikita zaidi kutoa taaluma kuliko ufanyaji wa utafiti.

Bakari alisema mataifa ya nje hasa Ulaya yamepiga hatua za kimaendeleo kutokana na matumizi ya tafiti za vyuo vikuu.

Akifungua mafunzo hayo, Mratibu wa shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Karna Soro, alisema tafiti ni nyenzo na muhimili muhimu katika kuharakisha maendeleo ya nchi.

Mratibu huyo alisema utafiti husaidia kutoa maamuzi sahihi ya kimaendeleo na kisiasa sambamba na kuonesha hali halisi ya tatizo lililopo katika muda uliopo na njia bora za kukabiliana na matatizo hayo.

“Matatizo ya kimaendeleo yanayoikabili nchi kwenye uchumi na siasa yataondoka endapo watoa maamuzi watajikita katika kuyafumbua matatizo hayo wakitumia tafiti zilizofanywa”, alisema Soro.

Alifahamisha kuwa mara nyingi wanasiasa wamekuwa wakikwepa kuzitumia tafiti kama njia ya kujikinga kutokana na dhana kuwa zimekuwa zikiwakosoa, jambo ambalo alisema limepitwa na wakati.

Mafunzo hayo ya siku tano yanayoendeshwa na Chuo cha Usimamizi wa Fedha Zanzibar (ZIFA), yanawashirikisha wahadhiri kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu vya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.