Na Ali Mohamed, Maelezo
WAZIRI wa Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman amesema kuwa Zanzibar ni nchi kamili yenye mamlaka ambayo iliungana na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 1964.
Ufafanuzi huo aliutoa jana wakati akizungumza na Naibu Mhariri Mkuu wa gazeti la kila siku la Misri Hossam Diab, katika mahojiano maalum yaliyofanyika makao makuu ya wizara hiyo.
“Zanzibar ni nchi kamili yenye mamlaka na serikali yake ambayo ni serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ina mihimili yote ya serikali yaani rais, katiba, Baraza la Mawaziri, Mahakama na Baraza la kutunga sheria”,alisema alifafanua waziri Haroun.
Mhariri huyo alifuatana na Balozi Mkaazi wa Misri hapa Zanzibar Walid Ismail pamoja na kutaka kujua historia na uchumi wa Zanzibar alijikita zaidi kutaka kujua nafasi ya Zanzibar katika Juamhuri ya Muungano wa Tanzania na kimataifa.
Alisema Zanzibar inaingia katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa baadhi ya mambo ambayo aliyataja kuwa ni masula ya kimataifa, ulinzi na usalama, fedha na uchumi na elimu ya juu na mambo yaliyobaki Zanzibar inajitegemea.
Alisema hakuna sababu ya Zanzibar kujitoa katika Muungano huo kwani inafaidika na malengo ya Muungano huo ukiwemo umoja, amani na utulivu pamoja na masuala ya kiuchumi ambapo wananchi wa Zanzibar wamewekeza Tanzania Bara.
Aidha alisema kuundwa kwa serikali yenye Mfumo ya Umoja wa Kitaifa kufuatia maridhiano ya kisiasa kati ya Rais Mtaafu wa awamu ya sita Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad Zanzibar imekuwa katika hali nzuri na maelewano miongoni mwa wananchi.
Akizungumzia historia na utamaduni waziri huyo alisema Zanzibar imekuwa na mahusiano na mashirikino na nchi za mashiriki ya kati akitolea mfano wa Oman ilikuwa ni sehemu ya Zanzibar na makao makuu yake yalikuwa Zanzibar.
Alisema asilimia kubwa ya wananchi wa Zanzibar ni waislamu na kwa jumla wananchi wake wana tabia ya ukarimu, upole na uadilifu na wanaunganishwa na lugha moja ya Kiswahili kama lugha ya Taifa ambayo chimbuko lake ni Zanzibar.
Kwa upande wa uchumi alisema uchumi wa Zanzibar unakuwa kwa asilimia 6.7 na inajulikana kuwa ni visiwa vyenye ardhi ya rutuba ambayo ni maarufu kwa kilimo cha minazi na mikarafuu na sekta ya utalii inachangia kwa asilimia kubwa uchumi wa Zanzibar kutokana na kuwa ni nchi yenye vivutio vingi vya utalii.
Aidha Waziri Haroun aliainisha kuwa sekta ya elimu hasa katika nyanja ya sayansi, kilimo na utalii ni maeneo muhimu ambayo Zanzibar na Mistri wanaweze kushirikiana zaidi kwa maslahi ya wananchi wa nchi mbili hizo.
No comments:
Post a Comment