SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), jana alasiri iliwasilisha katika Baraza la Wawakilishi mapendekezo yake kuhusu mapato na matumizi katika mwaka wa fedha 2011/12. Katika hotuba hiyo ya makadirio iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Mipango na Uchumi, Omar Yussuf Mzee, SMZ ililiomba Baraza hilo liidhinishe jumla ya Sh613 bilioni kwa shughuli za maendeleo na za kawaida.
Lazima tukiri kwanza kuwa, wakati muafaka wa kutoa hukumu iwapo Bajeti hiyo ni endelevu au yenye kusheheni ahadi tu za kisiasa zilizolundikwa katikati ya takwimu zisizotafsirika haujafika, kutokana na ukweli kwamba unahitajika muda wa kutosha kuyapitia mapendekezo hayo ya SMZ kwa mapana na marefu, vinginevyo tutakuwa hatuitendei haki hoja hiyo ya SMZ.
Lakini hilo halituzuii hata kidogo kuitathmini na kufanya majumuisho ya jumla kuhusu maudhui na mwelekeo wa Bajeti hiyo ya SMZ, kwa maana ya kuangalia vipaumbele vilivyowekwa na kuvilinganisha na hali halisi katika muktadha wa uchumi wa nchi zinazozungukwa na bahari kama Zanzibar ilivyo. Yatakuwa makosa makubwa, kwa mfano, kwa nchi hizo kupuuza kigezo cha eneo lao kijiografia kama moja ya mambo muhimu ya kuzingatia katika kuandaa bajeti za serikali hizo.
Hilo ndilo kosa ambalo SMZ, tofauti na nchi zinazozungukwa na bahari kama Mauritius, Comoro, Seychelles, Cuba, Jamaica na nyinginezo, imekuwa ikilifanya katika kuandaa bajeti zake na mipango yake ya maendeleo. Badala ya kuzingatia kigezo hicho na kupanga bajeti kwa mujibu wa vipaumbele, SMZ imekuwa ikijaribu kuiga nchi nyingine zilizo nchi kavu kama Tanzania Bara, ambazo zina ardhi ya kutosha kwa kilimo na mambo mengine ya maendeleo.
Tumemsikia Waziri Mzee akisema kuwa, Bajeti ya SMZ imeongezeka kutoka Sh444 bilioni mwaka wa fedha uliopita hadi Sh613 bilioni mwaka ujao kutokana na dhamira ya serikali hiyo kutoa kipaumbele katika sekta ya kilimo kwa kuweka mazingira bora ya kuifanya jamii kuvutika nayo, hivyo inakusudia kununua matrekta mapya, kuwapatia wakulima mbegu bora na kutengeneza barabara za mashambani ili wakulima waweze kuyafikia masoko kwa urahisi.
Pamoja na kwamba hatupingi wakulima kusaidiwa kuboresha kilimo, hasa cha mazao ya chakula, hatuoni kama misingi ya uchumi inaipa Zanzibar uwezo wa ushindani (competitive advantage) katika sekta hiyo kwa sababu zipo nchi jirani na visiwa hivyo zilizo na uwezo wa kuendesha kilimo kwa faida kubwa na kwa gharama ndogo.
Zanzibar ingewekeza katika sekta nyingine ambazo zinaipa nchi hiyo uwezo wa kushindana vizuri zaidi na nchi nyingine zilizo katika ukanda wa Afrika Mashariki, zikiwamo, utalii, uvuvi na kilimo cha zao la karafuu. Huko ndiko SMZ ingewekeza kwa kuwasaidia wakulima kuinua zao la karafuu, kuendeleza sekta ya utalii na kuifanya ya kisasa kwa kuweka miundombinu ya barabara, mawasiliano, kuendeleza Mji Mkongwe, kujenga hoteli za kisasa na kuwekeza katika fukwe za bahari na sehemu nyingine muhimu.
SMZ imesema itatilia mkazo suala la ajira, lakini ingeonyesha mikakati ya kupanua wigo wa kufanya hivyo. Tukizingatia kuwa suala la vijana kukosa ajira ni bomu linalosubiri kulipuka visiwani humo, SMZ ingeona umuhimu wa kujenga viwanda na kufufua vilivyokufa ili vijana wapate ajira za uhakika. Idadi kubwa ya vijana walioathirika kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya ni ishara tosha kuwa vijana hao wamekata tamaa kwa kukosa ajira.
Pamoja na ahadi za SMZ kuongeza mapato, hotuba ya Waziri Mzee ingekwenda zaidi katika kubainisha namna Bandari za Zanzibar na Pemba zitakavyoinua mapato hayo ya Serikali na kuainisha mikakati ya kufanya hivyo hata kwa viwanja vya ndege visiwani humo katika juhudi za kukuza sekta ya biashara.
Sisi tunatambua nia nzuri ya SMZ na juhudi zinazofanywa na viongozi wa serikali hiyo katika kuwaletea Wazanzibari maendeleo. Hata hivyo, tunadhani uchumi wa Zanzibar unaweza ukaboreshwa iwapo mipango ya maendeleo itazingatia vipaumbele halisi.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment