Habari za Punde

CCM MJINI WATAKIWA KUANZISHA VITEGA UCHUMI

Na Mwandishi wetu

VIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuanzisha vitega uchumi katika ngazi mbali mbali ili kukiondosha chama hicho katika utegemezi.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alipozungumza na Wajumbe wa Kamati za siasa za Mkoa wa Mjini Magharibi na wilaya zake huko Amani juzi, akiwa katika siku ya mwanzo ya ziara yake kukaguwa uhai wa chama kwa Mikoa ya Unguja.

Amesema iwapo viongozi wa CCM hasa ngazi ya Taifa na Mikoa watabuni na kuanzisha vitega uchumi madhubuti ndani ya maeneo yao, vitasaidia kukuza mapato yao na hivyo kumaliza tatizo la utegemezi ndani ya chama hicho.

Vuai amesifu uongozi wa CCM wa Mikoa ya Kaskazini na Kusini Unguja, ambayo tayari imeshaanzisha vitega uchumi, ambapo pamoja na kukabiliwa na matatizo madogo madogo ya kiutendaji, bado wanaendelea vizuri.

Akizungumzia kujivua gamba, amesema chama hicho kimefikia maamuzi hayo makubwa kwa lengo la kufanya mageuzi makubwa kiutendaji ili kuinua kiwango cha ufanisi katika utekelezaji malengo yake.

Alisema kujivua gamba, sawa na mwenge wa uhuru unaotembezwa nchi nzima, lengo kubwa likiwa ni kuleta heshima, kuondoa chuki na dharau miongoni mwa jamii ya Watanzania na kuongeza kuwa mabadiliko hayo yataendelea kufanyika katika ngazi zote za chama ikiwemo mikoa, wilaya, majimbo, Wadi na matawi kwa maslahi ya chama na Taifa kwa jumla.
Aidha alisema CCM imo katika mchakato wa kuwaendeleza watumishi wake kwa kuwapatia katika fani mbali mbali sambamba na kuwapatia mafunzo, vitendea kazi vya kisasa na kuboresha maslahi yao

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.