Habari za Punde

SERIKALI INAJITAHIDI KUDHIBITI DAWA ZA KULEVYA - DK BILAL

Na Mwandishi Maalum – Dar es salaam

Jumapili – Juni 26, 2011

Jumla ya watuhumiwa 30,830 walikamatwa katika kipindi cha mwaka 2005 mpaka 2010 kwa makosa mbalimbali ya biashara ya dawa za kulevya na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani yaliyofanyika leo katika viwanja vya Mwembe Yanga Jijini Dar es salaam Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal alisema hatua hiyo inatokana na jitihada za Serikali katika kudhibiti dawa za kulevya nchini.

“Bangi imeendelea kuwa tatizo kubwa kwa vile inastawi katika maeneo mengi  ya nchi yetu. Kutokana na kushamiri kwa kilimo hicho, jitihada zimeelekezwa katika uteketezaji wa mashamba ya bangi.  Kwa  mfano, katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010 jumla ya ekari 2,166 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika baadhi ya mikoa hapa nchini.” Alieleza.

Akizungumzia  waathirika wa dawa za kulevya Dk. Bilal alisema serikali imekuwa ikitoa tiba kwa waathirika hao katika hospitali mbalimbali hapa nchini na kuwataka waathirika wa dawa hizo kujitokeza kwa wingi katika vituo vya afya kupata matibabu.

Aidha, alisema katika katika jitihada hizo Serikali iko katika mchakato wa kuunda chombo mahsusi  huru na chenye nguvu cha kupambana na janga la dawa za kulevya nchini.

Alimtaka kila mwananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pale anapobaini kuwepo kwa watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kuwa vita dhidi ya biashara hiyo ni ngumu kutokana na watu hao kuwa na mitandao ikiwemo ya kimataifa.

“Vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya si rahisi, ni ngumu sana kutokana na ukweli kwamba katika mapambano haya tunashindana na watu hatari sana, wajanja na wenye mitandao ikiwemo ya kimataifa. Kutokana na hali hiyo, vyombo vya ulinzi na usalama vinahitaji ushirikiano kutoka kwa kila mmoja wetu,” alisema.

Aidha aliwaagiza wadau wa elimu kuhakikisha kuwa maeneo ya shule zote nchini yanakuwa salama bila dawa za kulevya na kupendekeza suala la madawa ya kulevya na athari zake liingizwe katika mitaala ya shule za msingi na sekondari.

Awali, akizungumza katika maadhimisho hayo Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya Christopher Shekiondo alisema pamoja na mafanikio wanayoyapata bado changamoto kubwa inayowakabili ni nchi kutumika kama njia ya kupitishia dawa za kulevya.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Miaka 50 ya Uhuru” Tanzania huru bila dawa za kulevya inawezekana; ujumbe ambao unahimiza Watanzania kuongeza nguvu za udhibiti wa dawa za kulevya hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inajiandaa kuadhimisha miaka 50 ya uhuru

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.