Habari za Punde

TUWATAYARISHE WANANCHI KUTUMIA MKONGA WA MAWASILIANO

Na Abdulla Mohammed Juma
 ZANZIBAR ikiwa miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia Tanzania nayo karibuni itafaidika na kutumia mkonga wa mawasiliano ‘Fibre Optic’ ambao unaendelea kutandazwa katika eneo hilo.

 Matumizi ya mfumo huo mpya wa teknolojia ya mawasiliano (TEKNOHAMA) yataifanya Zanzibar kupiga hatua kubwa katika matumizi ya mfumo huo ambao ni rahisi si tu kigharama bali pia kimatumizi, hivyo utaweza kutumiwa na idadi kubwa zaidi ya wananchi.
 Huku tukifurahia na kupongeza hatua hiyo kubwa kimaendeleo katika ulimwengu wa sasa, ambao unategemea zaidi teknolojia ya mawasiliano ya habari katika kufanikisha mipango mbali mbali ya maendeleo ya nchi na mwananchi mmoja mmoja, tunapaswa kujitathmini na kujipanga vipi tunaweza kupata faida.
Umuhimu wa kujipanga ni kutokana na nguvu za TEKNOHAMA kuweza kuchafua na kuathiri maendeleo ya nchi pale itapotumiwa vibaya au kufanywa kama chombo cha starehe, ambapo kinaweza kuleta mabadiliko mabaya, kuliko mabadiliko mazuri yanayotegemewa kuleta maendeleo nchini.
 Tunashuhudia hivi sasa matumizi ya mitandao hapa nchini ni makubwa, lakini ni wachache wenye kutumia teknolojia hiyo kimaendeleo, huku vijana wengine wakiitumia kwa kujistarehesha.
 Matumizi ya mitandao ya kompyuta yamekuwa yakishutumiwa kuchangia kuharibu maadili, mila, silka na utamaduni wa Zanzibar kwa vijana wengi kuiga mambo yanayofanywa na vijana wa nchi za magharibi.
 Hata hivyo mbali ya changamoto nyingi zilizopo katika matumizi ya TEKNOHAMA, Zanzibar haiwezi kujitenga na matumizi ya tekonolojia ya habari, ambapo mkonga huo utasaidia sana kufikia malengo hayo.
 Jamii ya kizanzibari hivi sasa imepiga hatua kubwa katika matumizi ya mitandao ya mawasiliano ikiwemo kompyuta na simu za mkononi, jambo ambalo litawarahisishia kutumia mkonga huo mara hatua za kuutandaza zitapokamilika.
 Tukichukua mfano hivi sasa wananchi wengi wa Zanzibar wana simu zaidi ya moja za mkononi ambazo hutumika kwa kazi na mawasiliano na nyengine ni kutukania watu, huku kompyuta zikitumika kuangalia picha za ngono na kuchati na marafiki.
 Hilo ni jambo moja ambalo lina faida kwa kuwepo mkonga Zanzibar, lakini pia ndilo lenye kuzaa umuhimu mkubwa wa wananchi kupewa elimu ya kutayarishwa na matumizi ya TEKNOHAMA kupitia mkonga huo vyenginevyo watautumia vibaya.
 Inatia moyo kuona Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya Saba, inajitayarisha kuingia katika matumzi ya e-government kwa kuweka mtandao na kuwapa majukumu maafisa maalum kusimamia suala hilo, pamoja na  mawasiliano ya taasisi zake na wananchi kwa jumla, hilo likikamilishwa linaweza kuwa mwanzo mzuri wa matumzi ya mkonga.
 Aidha hatua nyengine nzuri ambayo inategemewa kutekelezwa Zanzibar ni kueneza taaluma ya kompyuta na matumizi ya inateneti kwa skuli zote za Zanzibar, kupitia Mradi wa pamoja na kati ya SMZ na Shirika la misaada la Marekani (USAID), ambao utawawezesha wanafunzi kuweza kutumia tekolojia hiyo kwa matumizi mengi zaidi.
 Katika upande huu wa wanafunzi kufundishwa matumizi ya mtandao tahadhari kubwa ya kisera inahitajika, kwani kutokana na umri na utundu wa watoto na vijana wetu, inaweza kuiweka jamii pabaya badala ya lengo la kuipa jamii nyendo ya kuendelea kama ilivyokusudiwa.
 Ni lazima tuelewe kuwa matumizi ya mkonga huo hayatokuwa kwa mitandao ya intaneti tu, bali pia wananchi watalazimika kuutumia katika kupata huduma mbali mbali ikiwemo za afya, malipo ya ada za umeme, huduma za polisi na masuala yote ya kifedha nchini na ndani ya nchi.
 Iwapo wananchi hawa hawatoelimishwa kuna hatari ya kuweza kuibiwa hata fedha na mali zao kupitia wajanja wa kibiashara na matumizi ya mitandao ambayo itakuwa inatumika sana kupitia ushirikiano wa kikanda kama ule wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambao uko hivi sasa.
 Matayarisho mengine muhimu ya kufanywa ni kuwasomesha wataalamu wataokuwa wakisimamia mkonga huo, pamoja na kuufanyia matengenezo kutapotokea hitilafu, badala ya kuja kulazimika kutumia fedha nyingi kuita wataalamu kutengeneza.
 Tayari hatua za kutayarisha vijana wa kusimamia mkonga zimechukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupeleka masomoni vijana wengi kutayarishwa maalum kwa kazi hiyo.
 Aidha taaluma ya uwekaji kumbukumbu inapaswa kutolewa kwa watendaji wa ngazi zote zenye kuhusika na nyaraka hivi sasa, tukizingatia kuwa mawasiliano ‘correspondent’ nyingi zitakuwa zikifanywa kwa njia za mtandao kupitia mkonga na au e-government.
 Suala la elimu kuhusiana na usalama wa matumizi ya mkonga, pamoja na e-goverment, pamoja na mitandao ni muhimu kupewa watendaji wa ngazi mbali mbali kwa kuzingatia hatari iliyopo ya kuweza kufanyika iwapo hakutokuwa na matumizi ya njia za kulinda dhidi ya wezi wa kimtandao ambao wameenea hivi sasa.
 Ni dhahiri kwamba serikali itatumia fedha nyingi katika kukamilisha uwekaji wa mkonga huo, jambo ambalo linazaa umuhimu wa watumiaji na wananchi wa kwa jumla kupewa ABCD ya matumizi bora kwa kutolewa vipindi na makala mbali mbali kwenye vya habari nchini.
 Jengine muhimu ni kuwekwa sera ya matumizi ya TEKNOHAMA Zanzibar ambayo hadi leo haijatungwa, ili iweze kusaidia kutungwa sheria ya kuongoza na kusimamia suala hilo akutokana na unyeti wake.
 Hapa tunapaswa kuzingatia kuwa wakati Zanzibar inaingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni hatari sana kuachia suala la TEKNOHAMA kuendeshwa nchini bila kuwepo miongozo ambayo ni sera na sheria.
 Zanzibar inapaswa kuelewa kwamba wananchi katika nchi nyengine wanachama wa EAC ni wazuri na wanatumia mitandao hiyo kwa muda mrefu kiasi cha kubobea, hivyo kuachwa kuja kutumia hapa nchini bila ya muongozo wa sheria wala sera, itakuwa hatari badala ya faida kwa nchi na wananchi.
 Haitokuwa busara kama Zanzibar itasubiri hadi kutandikwa mkonga huo na kuanza kutumika ndipo iandae wananchi wake kuhusiana na matumizi, kwani hapo itakuwa imechelewa sana na itaachwa nyuma na wenzao wa EAC ambao wamechangamka mno kufikia matumizi ya mtandao.

Inawezekana.

0777 471199
abdulladulla@hotmail.com

1 comment:

  1. Hii ni hatua nzuri kwa maendeleo ila kama ulivyosema bwana mwandishi ELIMU ya matumizi ya hii teknolojia ni muhimu sana,kwani kuna wezi wengi sana ambao hutumia njia hii
    kuhusu swala la kutizama ngono kwenye mtandao ..hiyo nio sera ya nchi katika suala hilo..tizama OMAN au FALME ZA KIARABAU, serikali imezuiwa kutizama ngono kwenye mtandao...kama serikali itajali kabisa basi inawezekana.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.