Habari za Punde

SMZ KUWASHUGHULIKIA VIONGOZI WANAOHUSIKA MIGOGORO YA ARDHI

Na Mwantanga Ame

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ametangaza dhamira ya serikali kuwachukulia hatua viongozi na watendaji wataobainika kusababisha migogoro ya Ardhi katika visiwa vya Unguja na Pemba.


Hayo aliyaeleza jana alipowasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara na Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif, alisema serikali inachotaka kuona hivi sasa viongozi katika mikoa wanachukua hatua za haraka kuimaliza migogoro ya ardhi iliyojitokeza katika mikoa yao na ataeshindwa watahakikisha wanawachukulia hatua.

“Serikali inatoa wito kwa viongozi katika ngazi zote kuyashughulikia matatizo ya ardhi kwa haraka iwezekanavyo na viongozi kujiepusha kuwa chanzo cha migogoro” alisema Makamu huyo.

Akiendelea alisema itachokifanya hivi sasa ni kuona inawachukulia hatua viongozi wote ama watendaji wataosababisha kutokea kwa migogoro ya aina hiyo kwa kuwanyang’anya wananchi ardhi zao.

Alisema uamuzi wa kuchukua hatua hiyo ni kuona serikali inaandaa mazingira mazuri ya matumizi ya ardhi na kuondosha migogoro isiyo ya lazima kwani inachotaka kuona inakuwa endelevu.

Ili kulitekeleza hilo makamu huyo alisema serikali inakamilisha sera ya ardhi ikiwa ni hatua ya kuifanya kwenda na wakati pamoja na kuona vizazi vijavyo vinafaidika nayo.

Akizungumzia mambo ya Muungano alisema serikali itahakikisha marekebisho ya katiba yajayo yatawapa fursa wananchi wote kutoa maoni yao kwa uhuru ili kuweza kupatikana kwa katiba nzuri itayokidhi matakwa ya wananchi.

Alisema katika matayarisho ya upatikanaji wa maoni hayo serikali itahakikisha inaendelea kushirikiana na serikali ya Muungano katika maandalizi yake ambapo hivi sasa mchakato wake upo katika hali nzuri.

Alisema tayari hivi sasa yapo mambo kadhaa yameweza kufanyiwa kazi katika kutatua kero za muungano likiwemo suala la kodi kwa wafanyabiashara huku ikiendeleza suala la mgawanyo wa fedha katika mapato ya Muungano ambapo Zanzibar hupewa asilimia 4.5.

Kuhusu suala rushwa kwa watmishi wa Umma, alisema serikali haitamuonea haya mtumishi yoyote ambaye atabainika kula rushwa kwa kuhakikisha mkondo wa sheria unawawajibikia.

Alisema itachofanya serikali juu ya suala hilo kuona inawajibika kisheria kwa kuziba mianya yote ya ubadhirifu na kuwaondoa mara moja wale wote wanaojihusisha na vitendo vya hujuma katika utumishi wa umma.

Aidha Balozi Seif alisema kuwa hali ya ukuwaji wa uchumi wa Zanzibar unaendelea kujitokeza katika sekta mbali mbali ambapo serikali itahakikisha inauendeleza  ikiwemo sekta ya utalii, uwezeshaji wananchi, kukabiliana na tatizo la mazingira, kukuza sekta binafsi na kukuza uwezo katika taasisi za serikali.

Alisema hivi sasa serikali imo katika kufuata mabadiliko ya teknolojia kwa kuwa na mpango wa kuweka miundombinu ya mawasiliano yatayowezesha kuwepo kwa uratibu wa shughuli za umma.

Makamu huyo aliwataka wananchi kushirikiana na serikali yao ili kuielekeza jinsi watavyoweza kubuni njia za ajira mpya.

Suala jengine ambalo Balozi Seif, alilitaja ni dhamira ya serikali kupata mitambo mipya kwa ajili ya Kituo cha Televisheni Zanzibar, Redio Zanzibar na Idara ya Upigaji Chapa ambapo hivi sasa kinatarajiwa kuhamia katika majengo ya Amani viwanda vidogo vidogo.

Makamu huyo alisema nia ya serikali kuona inayaendeleza makundi yote ya kijamii katika kuona wanakuwa na hali nzuri ya kimaisha ambapo serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kupitia Wizara hiyo inakusudia kutumia shilingi 12,501,925,000 kwa Afisi zake na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Baraza la Wawakilishi.

Kati ya fedha hizo alisema matumizi ya shughuli za Maendeleo kwa ajili ya Afisi hiyo wanatarajia kutumia  shilingi 715,000,000.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.