Habari za Punde

WAKULIMA, WAPINZANI WAMFAGILIA DK SHEIN

Na Mwantanga Ame

UTARATIBU wa serikali wa kuweka ruzuku kwa wakulima na kushusha bei za pembejeo za kilimo umepongezwa na vyama vya upinzani  na wakulima lakini wameiomba serikali kulishughulikia tatizo la baadhi ya wakubwa kumiliki konde.


Wakizungumza na Zanzibar Leo kwa nyakati tofauti viongozi hao walisema serikali imefanya jambo kubwa ambalo litawawezesha vijana kubadili mwelekeo wao wa kimaisha pamoja na wakulima kuongezeka.

Mwanajuma Salmin Mcha, mkulima wa bonde la Cheju, alisema hatua ya serikali kushusha bei wameipokea kwa faraja kubwa lakini bado serikali italazimika kulishughulikia tatizo la baadhi ya wakubwa kuhodhi konde.

Alisema tatizo kubwa ambalo hivi sasa wanakabiliwa nalo ni la baadhi ya viongozi kuchukua konde za wakulima jambo ambalo huwafanya kukosa maeneo ya kufanyia kazi hizo.

Alisema ili mpango wa serikali wa kutoa ruzuku kwa wakulima uweze kuwanufaisha ni vyema serikali ikaliona tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi kutokana na vijana wengi kutaka kushiriki kazi za kilimo lakini wamekosa maeneo ya kufanyia kazi.

Alisema bei zilizokuwa zikitumika hapo awali zilikuwa zikiwauwa wakulima wengi, kwani walilazimika kutumia shilingi 40,800 kwa eka moja  kwa kazi za kuchimbiwa jambo ambalo wengi wao hawakuwa wakimudu.

Aidha, mkulima huyo alisema kazi nyengine ambayo serikali itapaswa kuizingatia ni kuona vipi watawasaidia kuongeza upatikanaji wa majembe kwa ajili ya kuburuga na kuchimbiwa ili wasipitwe na wakati.

Mkulima huyo alitoa rai kwa serikali kufikiria kuweka utaratibu wa kuwa na majembe hayo ambayo watayasambaza kwa kila wilaya kuwa na jembe lake.

Juma Ali Khatib, Katibu wa Chama cha TADEA Zanzibar, alisema hatua ya serikali kutangaza kuwapa wakulima ruzuku itaweza kuongeza nguvu kazi kwa vijana kushiriki kazi za kilimo.

Alisema chama chao kinaamini kuwa hapo awali vijana wengi walikimbia kufanya kazi za kilimo kutokana na gharama zilizopo wasingezimudu kutokana na kuwa hawana kazi.

Alisema kinachohitajika hivi sasa viongozi katika majimbo wakiwemo masheha, Wabunge na Wawakilishi, kufanya kazi ya kuwahamasisha vijana kuunda vikundi vya wakulima ili washirikiane kufanya kazi za kilimo.

Alisema ikiwa vijana wataweza kujiunga pamoja na kufanya shughuli hizo kwa kiasi kikubwa wataweza kuongeza kiwango cha chakula hapa nchini na kupunguza kula mapembe.

“Serikali na Wizara naipongeza sana kwa kubuni utaratibu huu kwani sasa ni mwanzo wa kupunguza kula mapembe maana tunakula michele mibovu kwa sababu ya lazima tununue kutoka nje lakini tunaamini sasa haya yataondoka” alisema kiongozi huyo.

Akiendelea  alisema kuwa wanaamini kuwa mpango huo pia utaweza kusaidia kuondoa tatizo la njaa ambalo huyakumba baadhi ya maeneo ya Zanzibar.

Wakulima wengine walieleza ipo haja kwa serikali kuanza kutoa elimu kwa wakulima juu ya utekelezaji wa mpango huo kwani si wakulima wote wanaouelewa.

Salum Ahmed, mkulima katika maeneo ya bonde la Mwera, alisema tangu kutolewa taarifa hiyo baadhi ya wakulima bado hawajaufahamu utekelezaji wake na wanahitaji kuelimishwa.

Hata hivyo, mkulima huyo aliipongeza serikali kwa hatua hiyo na kuiomba kuhakikisha utekelezaji wa uamuzi huo unafanyika kwa wakati ili kuwafanya wakulima kufaidika nao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.