Na Mwanajuma Abdi
MAKADIRIO ya Mapato na Matumzi ya Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano yalipitishwa jana huku kukijitokeza mvutano kuhusu baadhi ya vipengele ambavyo baadhi ya wawakilishi hawakuridhika na maelezo yake.
Waziri wa Wizara huyo, Hamad Masoud akalazimika kufanya kazi ya ziada kuikwamua bajeti yake ya mwaka wa fedha 2011/2012 na kupitishwa baada ya saa kadhaa kutumika kutolewa maelezo ya ufafanuzi.
Mvutano huo ulitokea ilipofika wakati wa upitishaji wa vifungu, hali iliyowafanya Mawaziri wa Serikali kutoa ufafanuzi mara kwa mara na hatimae kupita bila ya mabadiliko.
Mwakilishi Hamza Hassan Juma (Kwamtipura), alishauri iundwe Tume teule kuchunguza kasoro mbali mbali zilizojitokeza katika Idara ya Anga ikiwemo uajiri uliofanyika kinyume cha sheria kwa kuajiriwa baadhi ya vijana ambao bado wapo masomoni lakini huku tayari wameshapewa ajira hiyo.
Alisema kutokana na kasoro mbali mbali katika Idara hiyo ikiwa pamoja na uonevu uliofanywa wa kubadilishwa kada mfanyakazi na kupelekwa eneo jengine ambalo sio la taaluma yake kutokana na kitendo chake cha kuomba tenda akishirikiana na mume kuanzisha kampuni ya ubebaji wa mizigo katika uwanja wa ndege, ambapo licha ya taratibu zote kuzifuata mwisho wa siku hakupewa na matokeo yake ndio hayo yaliyomfika.
Alieleza Idara hiyo inakabiliwa na kasoro nyingi hivyo, alitaka iundwe Tume Teule ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ili kuchunguza mambo hayo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary, alilazimika kusimama kwa kumueleza Mwakilishi huyo kwamba kazi hiyo itafanywa na kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ambayo inawajumuisha wajumbe wa Baraza hilo, jambo ambalo lilikuwa na mvutano na hatimae alikubaliana nalo.
Mwakilishi wa Mkwajuni, Mbarouk Wadi Mussa (Mtando), alihoji kwamba ujenzi wa Makao Makuu ya Wizara hiyo awali ulikuwa ufanyike Mtoni lakini ulihaulishwa na kupewa mtu mwengine kwa shilingi milioni 200, ambapo alionesha wasiwasi kama taratibu na sheria zimefuatwa katika uhaulishwaji huo na sasa jengo hilo litajengwa Mazizini na kutaka kujua fedha hizo ziko wapi.
Waziri Hamad Masoud alieleza kwamba baada ya kuonekana kasoro mbali mbali katika eneo la Mtoni, Idara ya Ardhi iliamua kupima kiwanja Mazizini, ambako kutajengwa Makao Makuu na litakuwa na Wizara mbili, lakini hadi sasa ujenzi haujaanza kutokana kutotayarishwa michoro.
Kutokana na majibu hayo, Mtando hakuridhika hadi Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Issa Haji Ussi (Gavu), alipofafanua kuwa, uhaulishwaji huo umefanyika kisheria kwa vile Rais wa Zanzibar katika awamu iliyopita alikubali ombi hilo.
Nae Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alisema kuna baadhi ya gari za abiria zinazokatisha ruti kwa kukataa kuwafikisha abiria katika eneo wanalokwenda licha ya kupewa kibali cha kwenda huko, jambo ambalo linasababisha ajali.
Waziri Masoud alisema Idara ya Leseni inawaelekeza madereva na makondata hususani wa daladala, ambao wanakiuka taratibu hizo wakibainika wataadhibiwa ikiwa ni pamoja na kunyang'anywa leseni, kwani wanasababisha ajali.
Mapema akifanya majumuisho alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha inaimarisha ujenzi wa barabara zote za Unguja na Pemba ili kuwaondoshea usumbufu wananchi, ambapo katika bajeti ya mwaka huu alimuahidi Mwakilishi wa Kiwani Hija Hassan kujengwa barabara ya Jimbo hilo kwa kutengewa shilingi milioni 300.
Aidha alisema ujenzi wa jengo la abiria la Bandari yanafanyika mazungumzo na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), ili ijenge jengo hilo kuwawekea mazingira mazuri abiria.
Baraza hilo linajadili makadirio na mapato ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali iliyowasilishwa jana na Waziri wa Wizara hiyo, Ramadhan Abdalla Shaaban.
No comments:
Post a Comment