Habari za Punde

WAZIRI JIHAD AONGOZA KUPANDA 'GREAT WALL' CHINA

Ni moja ya maajabu ya dunia yaliyoko China
Asema vitu vya kihistoria chanzo cha mapato
Maofisa SMZ wasisitiza utunzwaji wa mazingira

Na Mwanajuma Abdi, Beijing
UTUNZAJI wa mazingira katika ukuta mkuu wa China (Great Wall), uliopo Magharibi ya jiji la Beijing, ambapo ni moja ya eneo tengefu la kiuchumi umechangia kukuza mapato ya nchi hiyo kutokana na kutembelewa na watalii kutoka nchi mbali mbali.


Hayo yamelezwa jana kwa wajumbe wa warsha iliyowashirikisha Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Mwanasheria Mkuu wa serikali na watendaji wa wilaya, maofisa wadhamini wa wizara mbali mbali na waandishi wa habari kutoka SMZ, waliopanda ukuta huo na kujionea ukuta hup ambao ni moja ya maajabu ya dunia.

Walisema utunzaji wa mazingira katika ukuta huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza nguvu ya uchumi wa China kutokana na idadi kubwa ya watalii kwenda kupanda na kujifunza historia kubwa ya ujenzi wa ukuta huo uliotumika kama kinga ya vita baina ya China na Mongolia, ambao waliakua na ugomvi wa mara kwa mara miaka 2000 iliyopita.

Walieleza licha ya ukuta huo kujengwa miaka 2000 iliyopita lakini hadi sasa upo katika hali nzuri kama uliojengwa miaka michache iliyopita, sambamba na kuwepo haiba nzuri ya miti na mikahawa ya kupata chakula kila eneo lenye mapumziko, jambo ambalo watu wengi hulifurahia eneo hilo.

Nae Mkuu wa msaafa aliyeongoza kupanda ukuta huo hadi kufikia kileleni, waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilah Jihadi Hassan alisema ukuta huo unahistoria kubwa ambayo ni moja kati ya maajabu saba ya dunia na unaisaidia serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kujikisanyia mapato makubwa yanayochangia uchumi wa nchi hiyo.

Alisema ameamua kuupanda hadi juu ili kuweka rikodi nzuri katika maisha yake, sambamba na kujifunza vivutio vinavyopatikana vya kitalii katika ukuta huo ili kuweza kusaidia kunyanyua sekta hiyo Zanzibar kwa vile ndio muhusika wa taasisi hiyo, inayochangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Aidha aliwapongeza waandishi wa habari kwa kuungananao hadi kufikia hatua ya mwisho wa ukuta huo, ambapo alisisitiza mazoezi ni kitu muhimu katika kujenga afya ya binaadamu.

Nae Waziri asiye na wizara Maalum, Machano Othman Said ambae aliishia kati kati ya ukuta huo alisema Tanzania ina nafasi kubwa ya kupanua uchumi wao kwa vile ina urithi mkubwa wa milima kama hiyo, hivyo alishauri juhudi zichukuliwe katika kutengeneza vitu vizuri vinavyoweza kuwavutia watalii kuutembelea na nchi ikakusanya mapato.

Alifahamisha kuwa, China inaingiza fedha nyingi katika mlima huo, ambapo mtu mmoja hulazimika kulipa dola 10 za Marekani, ambapo watu karibu 20,000 hadi 50,000 wanapanda mlima huo kila siku.

Nae Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura, Hamza Hassan Juma (aliyepanda hadi juu ya kilele cha mlima huo), alieleza utunzaji wa mazingira ni kitu muhimu sana, ambapo ukuta huo laiti ungalikuwa haujatunzwa tokea miaka iliyojengwa na wazee, vizazi vya sasa na vijavyo wakaurithi usingekuwepo na badala yake kungekuwa ni gofu.

Aliongeza kusema kwamba, Zanzibar ina vitu vingi na vyenye urithi wa kihistoria, hali ambayo hadi kuingizwa katika miji yenye urithio duniani, hivyo kuna kila sababu ya kuenziwa na kuacha tabia ya kuondosha majengo au miti ya asili kwani kufanya hivyo ni kupotesha historia hiyo, ambayo ingewasaidia kuja kurithi utajiri huo vizazi vijavyo.

Aliwapongeza China kwa kupandisha miti kwa wingi, ambayo inakuwa ni kichocheo kikubwa cha kuwavutia watalii, kuja kujionea uhalisia wa asili ya sehemu hiyo tegefu ya uchumi, ambapo alitoa rai kwa wakati umefika kwa Zanzibar kubadilika ili kudhibiti uharibifu wa mazingira ili kuweza kupanda daraja la juu katika kuimarisha uchumi kupitia katika sekya ya utalii.

Nae Naibu Waziri wa Elimu, Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamad alijitapa kwamba wanawake nao wanaweza licha kutomaliza hadi juu lakini wamevuka kiwango walichopangiwa na mkufunzi wa mafunzo hayo.

Aidha alitilia mkazo umuhimu wa utunzaji wa mazingira, kwa kusema kinachomfaa mtu ni chake, hivyo kuna kila sababu ya Zanzibar kubadilika katika kutilia mkazo suala la utunzaji wa mazingira na historia yenye utajiri mkubwa katika visiwa hivyo kuenziwa na kutunza bila ya kuharibiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo katika jitihada za kukuza uchumi na maendeleo ya nchi kupitia sekta ya utalii, ambayo imekuwa ni tegemeo katika kuongeza pato la taifa.

Alidokeza kwamba, unapotunza mazingira pamoja na upandaji wa miti kwa wingi kunasaidia kuongeza kasi ya kuwepo kwa mvua za kila mara, ambapo hilo limeonyesha kwa nchi ya China kila wakati inanyesha mvua hali inayosababisha kila watu wanapotembea wanachukuwa miavuli njiani.

Nae Mwakilishi wa Kitope, Makame Mshimba Mbarouk alionyesha mfano kwa watu wenye jamii yake ya vibonge kwa kuweza kupanda hadi juu ya Great Wall, sambamba na kuhimiza jamii umuhimu wa kufanya mazoezi na kutunza mazingira na vitu vya asili ili vibakie katika ramani ya dunia milele na milele.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.