Na Salum Vuai, Maelezo
BAADA ya timu ya Taifa ya Jang'ombe kuitikisha Mtibwa Sugar ya Morogoro juu ya usajili wa mchezaji wake Awadh Juma Issa, imebainika kuwa Mkurugenzi wa wakata miwa hao Jamal Bayser, anajiandaa kuja kisiwani hapa kwa nia ya kulipatia ufumbuzi sakata hilo.
Msaidizi Katibu wa Taifa Peter Augostino, ameliambia gazeti hili kuwa, Bayser amemuhakikishia kwamba yuko njiani ingawa hakuweka wazi siku atakayowasili Zanzibar.
Awali, Zanzibar Leo lilimuuliza Augostino juu ya hatua waliyokusudia kuchukua kukilalamikia kwa barua Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kama kilivyotakiwa kufanya na uongozi wa chama hicho ili nao uwasilishe madai hayo TFF.
"Nimewasiliana na Bayser kwa simu na ameniambia anafanya safari kuja hapa ili tuone namna ya kumalizana juu ya usajili wa Awadh, kwa hivyo, tumeamua tusiwasilishe barua ZFA mpaka tuone hatima ya mazungumzo yetu na Mtibwa", alisema kwa njia ya simu.
Alifahamisha kuwa kwa hatua hiyo inayokusudiwa kuchukuliwa na Mkurugenzi wa Mtibwa Sugar, uongozi wa timu yake umaemua kusitisha kwa muda dhamira ya kuishtaki timu hiyo ZFA, kwa ajili ya kuangalia njia za busara watakazoweza kutumia kufikia muafaka wa kadhia ya Awadh.
Itakumbukwa kuwa Taifa ya Jang'ombe ilikuwa ikilishutumu Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), kwa kile ilichodai kukiuka kanuni za uhamisho na usajili kwa kumuuza mchezaji Awadh Juma Issa akiwa mwanafunzi katika chuo chake cha kuendeleza vipaji (TSA).
Katika madai yake, Taifa iliegemeza hoja kwamba Awadh asingeweza kusajiliwa bila ya idhini ya timu hiyo kwa kuwa ndiyo anayochezea hadi wakati huu akiwa chuoni, na kwamba TSA si klabu na hivyo haina haki ya kuwamiliki wachezaji inaowasomesha ambao tayari wanazo timu zilizowasajili kabla kujiunga huko.
Hata hivyo, baada ya Taifa kuibua hoja hiyo, TFF ilijibu mapigo kupitia Ofisa Habari wake Boniface Wambura aliyedai kuwa mwanandinga huyo ni mali ya chuo hicho kinachomilikiwa na TFF, na kuitaka Taifa ifunge mdomo wake.
Kabla kujiunga na TSA kwa ajili ya mafunzo ya kukuza kiwango, Awadh Juma Issa amekuwa mchezaji wa Taifa ya Jang'ombe pamoja na timu ya taifa ya Zanzibar, 'Zanzibar Heroes
No comments:
Post a Comment