Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohammed Shein jana amefanya uteuzi wa nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk Abdulhamid Yahya Mzee Rais amewateuwa Sheikh Saleh Omar Kabhi kuwa Mufti Mkuu wa Zanzibar,Sheikh Khamis Haji Khamis kuwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar ambapo Sheikh Hassan Othman Ngwali kuwa Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar.
Aidha Dk Shein amemteuwa Muumin Khamis Kombo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Zanzibar,Khalifa Hassan Choum kuwa Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar, Abdulrahman Mwinyi Jumbe kuwa Mshauri wa Rais Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi .Pia Mwinyi Jumbe ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Watu wa Zanzibar.
Vile vile Rais amewateuwa Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa kuwa Mshauri wake katika mambo ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uwekezaji. Ramia aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania Nchini Sweden na India pia alikamata nafasi mbali mbali za Uwaziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Burhani Saadati Haji ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makaazi. Kabla ya Uteuzi huo Burhani aliwahi kuwa Waziri wa Kilimo pia Waziri wa Ardhi,Maji na Nishati.Pia Dk Shein amemteuwa Issa Ahmed Othman kuwa Mshauri wa Rais Utalii. Issa aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar.
Uteuzi huo unaanza jana.
No comments:
Post a Comment