Habari za Punde

KUZAMA MV SPICE - DK SHEIN AONGOZA MAELFU KATIKA DUA

 Kikwete: Ni msiba wetu sote
Balozi Seif:Waliozembea kukiona
Maalim Seif apongeza zoezi la uokoaji
Tume ya uchunguzi kutangazwa
Mbowe ataka meli zenye viwango

Na Mwantanga Ame

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein leo jioni aliongoza maelfu ya wananchi wa Zanzibar, Tanzania na nchi jirani, katika dua maalum ya kuwaombea waliofariki katika ajali ya kuzama meli ya Mv.Spice Islanders 1, iliyofanyika viwanja vya Maisara Mjini Zanzibar.

Dua hiyo iliyoongozwa na Sheikh pia ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda.


Wengine Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi, Mabalozi, Wawakilishi wa Jumuiya za kitaifa na kimataifa, pamoja na wageni kutoka Tanzania Bara, Kenya na Uganda.

Baadae Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhadi Mussa Salum kwa niaba ya Mufti Mkuu wa Tanzania, aliomba dua kwa niaba ya wananchi wa Tanzania na kufuatiwa na viongozi wa Kikristo nao waliomba dua iliyosomwa na Father Damas ya kuwaombea mahali pema marehemu, uzima waliojeruhiwa na subira kwa wafiwa.

Aidha kiongozi wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania ambao wote walihudhuria, Balozi Juma Khalfan Mpango kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nae alitoa salamu za mataifa ya nje kufuatia msiaba huo.

Nyuso za wananchi walioshiriki katika dua hiyo walionekana kuwa na nyuso zenye msiba kutokana na ajali hiyo kubwa zaidi kuikumba Zanzibar na kugusa kila familia ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Akizungumza katika dua hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amewataka waliopoteza ndugu na jamaa kuwa na subira na kuelewa kuwa Watanzania wenzao wako pamoja nao kwenye msiba huo.

Alisema yeye binafsi na kwa niaba ya Watanzania wote wanawaombea dua waliofariki Mungu awaingize peponi na kuwaombea waliojeruhiwa wapone ili waweze kufanya kazi zao kikawaida.

Rais Kikwete amesema kuwa ushirikiano mkubwa uliofanyika, baina ya taasisi za ulinzi za Tanzania na zile za Zanzibar, pamoja na wananchi umesaidia sana kufanikisha kuokoa idadi kubwa ya maisha ya watu, pamoja na maiti ambao walipatiwa maziko ya heshima.

Dk.Kikwete amempongeza Dk.Shein, maalim Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Ali Iddi kwa kusimama thabiti ili kuiwezesha nchi kukabiliana na janga hili kubwa.

Wakati huo huo SMZ imesema kuwa muda wowote kuanzia leo itatangaza majina yatakayounda tume ya kuchunguza kadhia ya kuzama ya kuzama Mv Spice Islander I.

Meli hiyo ilizama usiku wa kuamkia Jumamosi katika mkondo wa bahari ya Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo hadi jana watu 197 wamethibitika kupoteza maisha na wengine 619 wakifanikiwa kuokolewa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alibainisha hayo alipokuwa akizungumza na mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe aliyefika Zanzibar kumpa pole kufuatia ajali hiyo.

Kauli ya Balozi Seif ya kuunda tume hiyo imekuja kufuatia, mwenyekiti huyo wa CHADEMA kuiomba serikali ona isishindwe kuwachukulia hatua za sheria na kuwawajibisha wote waliohusika kusababisha janga hilo la msiba.

Mbowe alisema pamoja na ajali hiyo kutokea kunatokana na jaala ya Mwenyezi Mungu, lakini haiwezekani serikali ikakaa kimya dhidi ya wale wanaoonekana wamesababisha kutokana na uzembe.

Alisema ni tabia ya baadhi ya watendaji kushindwa kuwajibika kwa kutii sheria za nchi ni moja ya jambo kubwa ambalo limekuwa likiiumiza sana Tanzania, ambapo haiwezekani serikali ikailea tabia hiyo kwa kuwafumbia macho wazembe hao.

“Mungu hatutumi tufanye uzembe kama Mamlaka husika ikibainika kufanya uzembe hatua za kisheria zichukuliwe bila ya kujali, ili kudhibiti mambo haya yasitokee”, alisema Mwenyekiti huyo.

Aidha Mbowe alitoa pendekezo kwa kusema kuwa ipo haja kwa serikali kuhakikisha inatoa leseni za kumiliki boti kwa kuhakikisha vyombo watavyoletwa ni salama katika kufanya kazi zake.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa Chama chao kimeguswa kwa kiasi kikubwa na msiba huo, na kuwapa pole Watanzania wote na kuahidi kushirikiana na serikali ya Zanzibar katika kipindi hichi cha maombelezi.

CHADEMA, kilimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais shilingi milioni 5,000,000 na kuwataka wananchi kuwa na subira katika kipindi hicho cha msiba huo.

Akizungumzia hali hiyo, Balozi Seif, alisema serikali kwa kuthamini maisha ya wananchi wa Zanzibar, itahakikisha inaunda kamati hiyo na kutoa matokeo ya uchunguzi na haitasita kumchukulia hatua mtendaji atakayebainishwa amezembea.

Alisema serikali inaamini hadi sasa upo uzembe uliofanyika katika ajali hiyo kutokana na kujionesha kuwapo kwa idadi ya watu iliyozidi zaidi ya kiwango halisi cha kubeba abiria na mizigo.

Alisema hivi sasa serikali inajiandaa kuitangaza Tume hiyo wakati wowote ambapo itatakiwa kufanya uchunguzi wa haraka ili matokeo yake yaweze kufanyiwa kazi.

Alisema hivi sasa inachoamini serikali kuwa kuna idadi ya watu ambao bado hawajaokolewa, na tayari wameshafariki kutokana na kuzama na meli hiyo.

Alisema kutokana na hivi sasa kuja kwa wataalamu kutoka nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya uokozi inatarajiwa huenda serikali ikapata maiti zaidi.

Alisema tayari kikosi cha uokozi kutoka nchini Afrika Kusini kimeshaanza kazi ambapo watachunguza kama bado kuna watu waliomo ndani ya meli hiyo kwa kutumia njia mbali mbali kutokana na meli hiyo kuzama katika kina kirefu.

Hata hivyo alisema inawezekana hata kuipasua meli hiyo kwa ajili ya kuwawezesha waokozi ambao watashirikiana na waokozi wa Zanzibar pamoja na vikosi vya Ulinzi na Usalama kuweza kufanikisha kazi hiyo.

Balozi Seif alisema serikali imefarajika na michango inayotolewa na watu mbali mbali kwa ajili ya maafa hayo na itahakikisha inatumiwa ipasavyo kwa vile bado kuna mambo mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi.

Mapema Meneja Masoko na Utafiti wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa, alimkabidhi Makamu wa Pili Balozi Seif Ali Iddi, shilingi milioni 10 kwa ajili ya maafa hayo.

Mwakilishi huyo wa CRDB, alisema benki yao inawapa pole watanzania wote na Wazanzibari wote wakiwemo walioathirika na janga hilo ambapo benki yao itakuwa pamoja nao.

Msaada mwengine ambao ulitolewa kwa tukio hilo ulihusisha Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo ambapo walichangia shilingi 500,000.

Mwakilishi wa Jumuiya hiyo Talib Juma Ali, akizungumza kabla ya kuwasilisha mchango huo alisema Jumuiya yao imesikitishwa sana na msiba huo kwani umeweza kupoteza wazanzibari wengi.

Alisema kutokana na vifo na maafa hayo Jumuiya yao itakuwa tayari kuona inashirikiana na serikali katika kuomboleza kifo hicho na kuwatakia pole familia zote zilizofikwa na msiba huo.

Katika hatua nyengine, Mbowe alikutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ambae amepongeza ujasiri na mshikamano uliooneshwa na vikosi vya ulinzi na usalama, madaktari na wananchi wa Zanzibar katika kuokoa maisha ya watu baada ya kutokea ajali hiyo.

Maalim Seif alisema kutokana na ujasiri na mshikamano huo ndio maana kuna idadi kubwa ya abiria waliokuwemo kwenye meli hiyo walioweza kuokolewa maisha yao pamoja na wale waliopoteza maisha kuweza kutambuliwa haraka na jamaa zao na wengine kuzikwa na serikali.

Makamu wa Kwanza wa Rais alisema baada ya kupatikana taarifa za kuzama kwa meli hiyo majira ya saa 8:30 usiku Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilifanyakazi ya ziada kuhakikisha maisha ya watu yanaokolewa, juhudi ambazo zilipata mafanikio makubwa kutokana na mwitikio wa hali ya juu wa vyombo vya serikali pamoja na nidhamu kubwa iliyooneshwa na wananchi wote.

“Serikali ilifanyakazi ya ziada, wananchi walikuwa na nidhamu na utulivu wa hali ya juu, askari nao walifanya kazi nzuri sana na hata mabalozi na viongozi wote kwa jumla waliweza kushiriki kikamilifu na kutoa mchango wao baada ya kutokea maafa haya”, alisema Maalim Seif.

Alisema tukio la ajali ya meli hiyo likumbusha wajibu wa taifa kujiandaa na kuhakikisha linaondokana na kasoro zote zinazoweza kusababiha kutoka kwa maafa ya aina hiyo ambapo roho za watu wengi hupotea.

Alisema serikali ina wajibu wa kujenga uwezo katika suala la uokozi kwa kuwa na vifaa vya kisasa pamoja na kusomesha wananchi masuala ya uokozi majini ili kukabiliana kikamilivu na hali kama hiyo pale inapotokea kwa dhamira ya kuokoa maisha ya watu.

Katika mazungumzo hayo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema maafa yaliosababishwa na kuzama kwa meli hiyo yamewagusa Watanzania wote na ndio maana viongozi wa chama chake wameamua kuwapa pole kwa yaliyotokea na kuwashukuru wananachi wa Zanzibar kwa juhudi kubwa walizofanya kuokoa maisha ya abiria na kuwahudumia waliopoteza maisha.

Mbowe alisema kuna haja kianzishwe kikosi maalum cha uokozi wa baharini ili kutoa huduma za haraka na za uhakika mara inapojitokeza haja kama hiyo.

Alisema maafa yaliyotokea Zanzibar si jambo jepesi na lazima hatua za uchunguzi zifanywe kujua nani alizembea katika kutekeleza majukumu na ili watu wawe na utamaduni wa kuogopa na kusimamia majukumu yao ipasavyo.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.