Na Khamis Haji, Zanzibar
ZANZIBAR kama zilivyo jamii nyIngine katika Tanzania imekuwa ikikumbwa na matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu, hali inayosababisha jamii ya wasomi na wanasiasa waumize vichwa vyao kutaka kujua chanzo cha kukithiri kwa vitendo hivyo vinavyokiuka misingi ya ubinaadamu.
Ukubwa na tatizo hili na kukithiri kwa matukio ya unyama na ukatili dhidi ya ubinadamu ulionekana takribani miaka miwili iliyopita, zaidi kwa upande wa Tanzania Bara, pale walipojitokeza watu wanaojihusisha na biashara ya viungo vya binaadamu wenye ulemavu wa ngozi, maarufu albino.
Matukio kama ya watu wenye ulemavu kusakwa na kukatwa viungo kwa ajili ya biashara na imani za kishirikina sio tu yanachafua hadhi, heshima na rekodi ya nchi katika haki za binadamu mbele ya uso wa kimataifa, bali yanamaanisha ni kwa kiwango kikubwa jamii zetu zinavyokosa kuthamini utu.
Kwa upande wa Zanzibar, matatizo makubwa wanayokumbana nayo watu wenye ulemavu ni kama vile udhalilishwaji kijinsia ambapo kuna matukio ya baadhi yao kubakwa, kukosa haki zao mahakamani wakati kesi zinazowahusu zinapoendeshwa kwa sababu wengi wao hushindwa kujieleza vizuri na hata kushindwa kuripotiwa vizuri kesi hizo zinapofika Polisi.
Malalamiko mengine kutoka kwa watu wenye ulemavu Zanzibar ni kukoseshwa elimu, matunzo duni katika familia ambapo kumeripotiwa matukio kadhaa ya watu wenye ulemavu kufungiwa ndani ili wasitoke nje ya nyumba zao, kutopatiwa huduma za matibabu, kutopatiwa nafasi katika vyombo vya kutoa maamuzi pamoja na kutokuwepo mipango rafiki katika majengo, yakiwemo yanayotoa huduma kwa jamii.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ofisi yake ndiyo yenye dhamana ya masuala ya watu wenye ulemavu, hivi karibuni amewafumbua macho wanajamii kuhusu chanzo na kushika kasi ya udhalilishaji dhidi ya watu wenye ulemavu katika jamii zetu.
Maalim Seif alikiri kujitokeza kwa matukio ya kunyanyaswa na kudhalilishwa watu wenye ulemavu, ikiwamo kudhalilishwa kijinsia, kutendewa matendo ya kikatili, na baya zaidi baadhi ya wakati matendo hayo hufanyiwa na jamaa kwenye familia zao.
Kwa mujibu wa Maalim Seif kuna malalamiko pia watu wenye ulemavu hawashughulikiwi ipasavyo na taasisi za serikali zenye majukumu ya kuwalinda raia na mali zao, ambapo uonevu wanaofanyiwa mara nyingi hupuuzwa au hudharauliwa na baadhi ya wale wenye dhima na majukumu ya kulinda haki za raia.
“Haya yote sababu zake za msingi ni kuporomoka kwa maadili katika jamii, watu tumepuuza mafunzo mema ya dini, mila na desturi njema za Mzanzibari zimewekwa kando, matokeo yake baadhi yetu tumekuwa fukara wa utu, fukara wa wema na hata ukarimu kwa wenzetu hasa watu wenye ulemavu”, alisema wakati akizindua baraza jipya na taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar.
Lakini, kwa upande mwingine, jamii pia haikosi kubeba lawama juu ya kukithiri kwa matendo maovu dhidi ya watu wenye ulemavu kutokana na baadhi ya wanajamii kuhusika katika kuwatumikisha kwa kazi nzito nzito watu wenye ulemavu hasa wa akili.
Pia, jamii yetu imekuwa na tabia ya kukaa kimya na kuyafumbia macho pale wanaposhuhudia maovu hayo yakifanyika na badala yake hushindwa hata kukemea vitendo hivyo.
Maalim Seif, Zanzibar anaeleza kluwa amejizatiti kusimamia misingi ya haki za binadamu, ikiwamo kuhakikisha haki za raia wote wakiwamo wenye ulemavu.
Anasema katika kutekeleza hilo, baraza hilo la wenye ulemavu litapaswa kusimamia vyema majukumu yake na kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa na watu wenye ulemavu wapate haki zao kwa ukamilifu na waondokane na mawazo potofu kwamba ubinadamu wao una kasoro na hatimaye wajisikie na wao ni binadamu kamili sawa na wengine.
Kiongozi huyo anasema changamoto kubwa zinazohitajika kufanyiwa kazi na baraza hilo kwa sasa ni kubuni mikakati itakayoweza kutekelezeka katika kutatua matatizo yanayowakabili wenye ulemavu, kazi ambayo itaweza kutekelezwa vizuri pale baraza hilo litakapokuwa na mpango mkakati uliokamilika.
“Sera ya watu wenye ulemavu ya 2004, pamoja na sheria ya watu wenye ulemavu namba 9 ya 2006 ndizo ziwe zana na dira yenu na mtalazimika kuzisoma na kuzielewa kwa makini, na kama mtaona kuna haja ya kuzifanyia marekebisho msisite kuishauri serikali, serikali itayafanyia kazi mapendekezo yenu”, anasema Maalim Seif.
Anasema ni wajibu wa baraza hilo na wanajamii kwa ujumla kuwekeza katika fursa na haki za watu wenye ulemavu kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kujiwekezea wenyewe kwa kutambua kuwa ulemavu unaweza kutokea wakati wowote.
“Tukumbuke kwamba kila mmoja wetu ni kama mtahiniwa katika uwezekano wa kukumbana na mazingira yatakayosababisha kupata ulemavu, tukumbuke maneno ya hekima , ‘Kabla hujafa hujaumbika’, kila mmoja wetu ni mtu mwenye ulemavu mtarajiwa,” anakumbusha.
Katibu wa Baraza la Taifa la watu wenye Ulemavu Zanzibar, Abeida Rashid Abdallah anaeleza kuwa kazi kubwa inayofanywa na baraza hilo hivi sasa ni kuzunguuka Zanzibar katika zoezi la kusajili watu wenye ulemavu lenye madhumuni ya kupata takwimu halisi na sahihi za wenye ulemavu.
Kazi hiyo ya kusajili watu wenye ulemavu inatarajiwa kuendelea kisiwani Pemba, baada ya kukamilika katika vijiji 65 katika wilaya mbili za Mkoa wa Kaskazini Unguja ambazo ni Kaskazini A na B.
Katika zoezi hilo la uwekaji kumbukumbu za watu wenye ulemavu hadi kufikia Julai mwaka huu, watu 3,007 walikwishasajiliwa, baada ya kazi kubwa ya kuhamasisha jamii, pamoja na viongozi wa serikali za mitaa kwa nia ya kufanikisha kazi hiyo.
Katibu huyo anasema wamefanya juhudi kubwa ya kutembelea ofisi za umma kwa lengo la kuhimiza kuzingatiwa hali za watu wenye ulemavu pale wanapotaka kwenda kupata mahitaji katika sehemu hizo.
Kutokana na majengo mengi kujengwa bila ya kuzingatiwa watu wenye mahitaji maalum kama vile wenye ulemavu mara nyingi inakuwa vigumu kwao kuwafikia wahusika na kufanikiwa kupata huduma wanazozihitaji katika sehemu hizo, hasa ofisi na maeneo yanayotoa huduma kwa umma, ikiwemo matibabu.
“Tumepata moyo kuona kuna taasisi nyingi hasa zile za serikali wanatupa ushirikiano, ingawa baadhi ya ofisi hadi sasa bado zina uelewa finyu kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu,” anasema Abeida ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar.
Katika kukuza ustawi wa watu wenye ulemavu mipango inaendelea kuwahamasisha wanajamii juu ya haki na fursa kwa watu hao kwa nia ya kuwawezesha kujumuika na wanajamii wengine katika nyanja zote, ikiwamo kielimu ,kiuchumi na kuwawezesha kuinua hali za vipato vyao na kuondokana na utegemezi.
CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment