MARA nyingi kupitia gazeti hili na mengine na vituo vya radio na televisheni vya nchini na nje nimelezea uoza uliopo Zanzibar juu ya usafiri wa baharini.
Katika makala moja ndani ya gazeti hili kufuatia zaidi ya watu 30 kupoteza maisha yao walipokuwa wakisafiri kati ya Pemba na Tanga nilisema: “Zanzibar haitajifunza juu ya haja ya kuchukuwa tahadhari za usalama wa baharini hadi kaburini”.
Katika wakati wa msiba mkubwa kama huu uliotokea wa meli ya mv Spice Islander kuzama na kupelekea zaidi ya watu 240 kupoteza maisha yao si vema kukumbusha kilio matangani. Lakini ukichelea kumtonesha mwenye kidonda hutaweza kusaidia kumtibu.
Ukweli ni kwamba maisha ya watu wanaosafiri kwa njia ya bahari kati ya Dar es Salaam, Unguja, Pemba na Tanga yanachezewa kama mpira, karata, kete za bao au karata. Kwa ufupi unaweza kusema hata mnyama anathaminiwa zaidi kuliko watu wanaotumia usafiri huu.
Yafuatayo ambayo yamekuwa mambo ya kawaida katika safari za hizi meli yanaweza kutoa sura jinsi usalama wa abiria ulivyokuwa hautiliwi maanani:
Ni kawaida kuona meli imesheheni abiria na mizigo na kuelemea upande mmoja. Hata meli inapozuiliwa isiondoke banadarini manahodha hufanya jeuri na kibri. Mfano ni wa meli ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mv Mapinduzi, ilizuwiwa Dar es Salaam isifanye safari ya kwenda Mtwara, lakini nahodha hakujali na alifanya safari hio. Mhusika hakuwajibishwa.
Baadhi ya wakati utasikia meli imeishiwa mafuta ikiwa katikati ya bahari na husubiri kwa masaa kupelekewa mafuta katika mapipa kutoka bandari ya karibu.
Wakati mwengine watu husafiri katika meli hizi zikiwa hazina maji. Hali za vyoo za baadhi ya hizi meli inatisha, yaani usafi haupo katika orodha ya mambo muhimu ya wamiliki wa vyombo hivi. Kwa wao pesa tu ndiyo muhimu na siyo maisha ya watu.
Ratiba za meli hazifuatwi na mamlaka za bandari Zanzibar, Dar es Salaam na Pemba hazina ubavu wa kuwakemea wamiliki wa meli hizi au manahodha wao. Hapa huenda rushwa ikawa inahusika. Badhi ya wakati utaona meli imekawia kuondoka na unapouliza unaambiwa ilikuwa inawasubiri wana wa familia wa mmiliki wa meli akiwa njiani kwenda bandarini.
Meli hizi zinazopakia abiria 300 na zaidi zinafanya safari bila ya daktari au wauguzi. Wengi wa mabaharia wanajuwa kuogelea, lakini hawana mafunzo ya uokozi.
Hapana uhakika wa kuwepo ukaguzi wa angalu kila mwezi juu ya usalama wa hizi meli na kutolewa hati inaonyesha ni salama kusafirisha abiria.
Kinachoshangaza ni kuona bandari zetu, hasa za Unguja na Pemba, zimesheheni askari wa vikosi vya ulinzi vya Muungano na Zanzibar, forodha, KMKM, usalama wa taifa, lakini hakuna hatua za kuhakikisha usalama zinazoonekana kuchukuliwa.
Kinachopewa umuhimu hapo ni mambo binafsi na kuyapa umuhimu mambo madogo na kufumbia macho yale muhimu yanayohusu usalama wa wasafiri.
Matokeo ya maafa kama ya mv Bukoba miaka 12 iliyopita ambapo watu wapatao 800 walikufa na ajali za majahazi na meli kuzama bandarini na kuchukuwa zaidi ya masaa 24 kwa kazi ya uokozi kuanza yanaonekana hayakutoa mafunzo.
Niliuliza lini Wazanzibari tutajifunza. Au ndio tunangojea kufika katika nyumba zetu za kudumu, yaani makaburini, ndio tutajifunza?
Tatizo liliopo Zanzibar ni serikali kujali muhali na kuonea watu haya na matokeo yake ni kuwa sheria na kanuni za uwajibikaji kufumbiwa macho. Utasikia zinaundwa tume za uchunguzi, lakini huoni wahusika kuwajibishwa.
Wakati umefika kwa serikali zote mbili, ya Muungano na ya Zanzibar , kujitokeza kufanyakazi ya kulinda maisha ya watu wake na kutokubali kuona yanachezewa. Ni vizuri kusimamia sheria ziliopo na kuona kanuni za uwajibikaji zinafuatwa.
Nchi yetu imeshapata maafa makubwa ya usafiri wa baharini na msiba mkubwa uliotokea Zanzibar unapaswa uwe somo jengine. Ni vizuri tukajifunza na sio kungojea tumefika makaburini ndio tukaanza kujifunza kusoma mambo tuliyoyaacha duniani.
Kila mmoja wetu lazima atekeleze wajibu wake na asiyetekeleza awajibishwe. Nyakati za kulindana kwa misingi ya huyu ni mwenzetu, baba yake tumetoka naye mbali au nimesoma naye shule zimepitwa na wakati.
Ni lazima maisha ya watu wakati wote, iwe ardhini au baharini, yapewe umuhimu kuliko siasa na urafiki. Watu hilindana kwa mema na sio maovu. Wenzetu ni wale wanotenda mema na ni lazima tuwatenge na kuwalaani wale wanaohatarisha maisha ya watu wetu. Hatuna njia ya mkato na tuanze sasa kuhakisha uwajibikaji unachukuwa mkondo wake.
Miongoni mwa njia nzuri za kurekebisha hali hii ya kusikitisha na kutisha ya usafiri wa baharini visiwani ni kuondoa wafanyakazi wote wazembe waliopo bandarini hivi sasa.
Lakini hao wataochukuwa nafasi zao sio tu wawe watu ambao wanajuwa kazi wanayotarajiwa kufanya, bali ni waadilifu na wanaoheshimu maisha ya binadamu. Safari ni safari, lakini ni vyema tuhakikishe safari zetu si za hatari.
CHANZO : Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment