Habari za Punde

KUTOKA BARAZANI - JUSSA AHOJI UHALALI WA SERIKALI KUWAN'GAN'GANIA WASTAAFU

SERIKALI imeeleza kuwa itaendelea kuwapa ajira watu waliofikia muda wa kustaafu baada ya kuzingatia utaalamu waliyonao kutokana na kukosekana kwa wataalamu kujaza nafasi hizo.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir, aliyasema hayo wakati akijibu suali la nyongeza la Ismail Jussa Ladhu (Mji Mkongwe), aliyetaka kujua kuna sababu gani kwa serikali kuwaajiri wastaafu hasa wale walioonesha kutokuwa na ufanisi walipokuwa madarakani.

Akijibu suali hilo Waziri alisema serikali inafanya hivyo kwa kuangalia maeneo ambayo yamekosa wataalamu wanaohitajika.


Waziri huyo alisema wataalamu hao hupewa mikataba maalum na sio kama serikali huwarejesha bila ya kuwapo utaratibu.

Kuhusu swali la Mwakilishi wa Kitope, Makame Mshimba alietaka kujua kwanini serikali imeweka kiwango kidogo cha mishahara kama ni sababu inayoafanya wataalamu kukimbia kufanya kazi serikalini, alisema serikali inlifahamu jambo hilo na ndio maana imeamua kufanya mabadiliko ya mishahara ya wafanyakazi.

Alisema mabadiliko hayo serikali inatarajia kuanza kulipa viwango vipya vya mishahara kuanzia mwezi huu na imewaomba wafanyakazi kuridhika na viwango hivyo vipya.

Akijibu suala la msingi la Mwakilishi wa Muyuni Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua kama serikali inazingatia suala la kuwatunza wataalamu kutokana na hivi sasa wamekuwa wakikimbia baada ya kusoma kutokana na mishahara kuwa midogo.

Waziri alisema serikali katik mabadiliko itayoyafanya ya mishahara ya watumishi wa umma imezingatia suala la kuwatunza wataalamu kwa kuzingatia kada wanazozitumikia.

Alisema hivi sasa serikali imekuwa ikikabiliwa na tatizo la ukosefu wa wataalamu katika kada ya udaktari, Kilimo, Mifugo, Wahandisi wa Ujenzi na miundombinu ya barabara.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Waziri huyo alisema serikali imeshaweka utaratibu wa kuwachukulia hatua wale wote ambao watapewa udhamini wa masomo na serikali halafu wakashindwa kurudi kazini.

Alisema utaratibu ambao serikali imeuweka ni kuwawajibisha walioomba fedha hizo kwa kuwataka kulipa gharama zote za masomo kupitia kwa waliowachukulia dhamana.

Alisema lengo la serikali ni kuona viwango vipya vya mishahara kwa wataalamu wa serikali ya Zanzibar hawatofautiani na wale ambao wapo katika utumishi wa umma katika serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Alisema pia serikali imo katika hatua ya kufanya utafiti juu ya suala la ajira nchini kwa kuziangalia changamoto ziliomo katika sekta hiyo ili baadae serikali iweze kutafuta njia za kukabiliana nazo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.