Na Nafisa Madai Maelezo Zanzibar
Waziri wa Miundo Mbinu na Mawasiliano Mhe Hamad Masoud Hamadi amesema wakati umefika sasa kwa madereva na matingo kuwa na mikataba maalumu ili iweze kualinda katika kazi zao za kila siku.
Amesema hayo alipokua akifungua kongamano la kuanzimisha wiki ya kimataifa ya wafanya kazi wa sekta ya usafiri kwa njia ya barabara huko katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazimmoja mjini Zanzibar
Waziri Masoud amesema si wakati tena huu kwa matingo na madereva wa daladala na tex kufanya kazi kwa kubahatisha kwani nao wanapaswa kisheria kufanyiwa mikataba ya kazi kwa vile wanategemea na familia zao
Aidha amesema kutokana na umuhimu wa mikataba ya kazi wizara yake italishughulikia suala la madereva na matingo wa daladala na kuweza kuona kuwa wanamikataba ya ajira ili kuwa na uhakika wa kazi wanayoifanya.
Aidha alisema mikataba hiyo itawawezesha madereva hao na matingo kupata mapumziko na kufanya kazi kwa mujibu wa kufuata sheria za kazi na kusaidia kupunguza uchovu na kuondosha ajali barabarani za mara kwa mara.
Hata hivyo alisema wizara yake pia itachukua juhudi ya kuimarisha ofisi ya ukakuzi wa magari kwa kuipatia vifaa vya kisasa vya ukaguzi wa magari ili iweze kulingana na teknolojia mpya inayokwenda sambamba duniani kote.
Sambamba na hayo waziri huyo amesema utaratibu maalum unaandaliwa na wizara wa kutoa mafunzo ya kutosha kwa matingo na madereva ili waweze kufanya kazi bora na kwajali wateja wao na kulinda mali za matajiri zao.
Hata hivyo amesema wizara itaimarisha alama za barabarani, taa,sehemu za kuegesha magari na kusimamia vituo vya uhakika ili kupunguza misongamano isiyo ya lazima.
Waziri Masoud aliwataka madereva kuwacha kutumia lugha chafu, dharau na kejeli na kuondosha gari kabla abiria hajakaa kwenye kiti hali ambayo imekua ikiwakatisha tama abiria wao na mara nyengine kuwasababishia vilema vya maisha.
Kwa upande wake katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa sekta ya usafirishaji bwana Muhamedi Ali Salum amesema chama chao kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa mikataba jambo ambalo limekua likiwarejesha nyuma kimaendeleo.
Hata hivyo alisema kutokuwa na mikataba ya kazi wa madereva hao na matingo ndiko kunakosababisha kufanya kazi kinyume na sheria za barabara na kusababisha ajali za mara kwa mara.
Aidha amesema lengo la kufanya kongamano hilo ni kuweza kupata fursa ya kukaa pamoja kama wadau kutafakari,kujadiliana namna ya kutafuta mbinu mali mbali za kutatua matatizo yanayoikabili katika sekta hiyo.
Kongamano hilo limewashirikisha wadau mbalimbali kupitia jumuia zao wakiwemo madereva, matingo wa daladala na madereva wa magari ya mizigo na matingo wao madereva wa gari za shamba na matingo wao pamoja na madereva wa taxi ambapo ujumbe wa mwaka huu kimataifa ni usalama sasa (SAFETY NOW)
No comments:
Post a Comment