Sasa kusubiri daraja la pili msimu ujao
Wadau watabiri mtikisiko mkubwa
Na Salum Vuai, Maelezo
BAADA ya kukivimbia Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kwa kususia mechi tatu mfululizo za ligi daraja la kwanba taifa, klabu ya Malindi imeondolewa katika mashindano hayo.
Barua ya ZFA Taifa iliyoandikwa Oktoba 25, 2011 kwenda kwa klabu 11 za ligi daraja la kwanza taifa, yenye kichwa cha habari "Ushiriki wa timu ya Malindi katika ligi daraja la kwanza 2011/2012", ambayo nakala yake tunayo, imethibitisha kuwa timu hiyo imeteremshwa madaraja mawili kutokana na kitendo hicho.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho Mzee Zam Ali, ilielezwa kuwa, ZFA ilipokea barua ya klabu ya Malindi ya Oktoba 6, mwaka huu, iliyolenga kuomba radhi kwa kitendo cha kutofika uwanjani ilipopangwa kucheza na timu ya Mtende.
ZFA ilifahamisha kuwa, Malindi ilieleza sababu kadhaa za kushindwa kufika dimbani, ambazo zilitokana na matatizo yaliyomo ndani ya klabu hiyo kongwe iliyoshuka daraja kutoka ligi ngazi ya Premiar msimu uliopita.
Kufuatia kuombwa radhi, ZFA ilisema, kutokana na ubinadamu, ilikubali sababu hiyo, ikiamini kuwa uongozi wa timu hiyo itayatatua matatizo yake katika kipindi kifupi, sambamba na mengine muhimu yaliyoikabili timu yao.
Hata hivyo, ZFA ilidai kuwa katika kusubiri kuona mambo yanarekebishwa, klabu hiyo haikuonekana kufanya juhudi zozote za kuondoa kasoro zake, bali iliendelea kuvikimbia viwanja na kutopeleka kikosi chake katika mechi nyengine mbili, dhidi ya Kijichi, na Ngome.
Aidha, Malindi imetiwa hatiani kwa kushindwa kurejesha ZFA fomu za usajili wala kulipia ada ya mashindano ambazo kwa mujibu wa kanuni za ZFA, ilitakuwa itoe si zaidi ya siku 20, na kama haikutekeleza, iondolewe kwenye mashindano.
"Siku hizo zimepita na klabu ya Malindi imeondolewa kwenye mashindano. Hivyo mechi zote za timu hiyo kuanzia tarehe ya barua hii zimefutwa", ilimalizia barua hiyo ambayo nakala zake pia zimetumwa kwa Katibu wa BTMZ, Kamati ya Rufaa na Usuluhishi, pamoja na Kamati ya Waamuzi Zanzibar.
Hata hivyo, Meneja wa klabu ya Malindi Mohammed Masoud, alisema pamoja na uamuzi huo wa ZFA, klabu yake inaendelea na msimamo wake wa kutotamnbua kanuni iliyotumika kuiteremsha daraja, na kwamba iko katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kufikisha mahakamani ZFA pomoja na viongozi wake kwa kutowajibika ipasavyo katika majukumu yao.
Baadhi ya wadau wa soka waliozungumzia uamuzi wa ZFA, wamesema pamoja na kuwa imefuata kanuni, lakini hatua hiyo inashiria kuwepo kwa bomu ambalo wakati wowote linaweza kuripuka, na hivyo kusababisha mtikisiko mkubwa katika soka la Zanzibar.
Kwa mambo yetu ya ZNZ, hayo maamuzi yatabatilishwa. atafatwa hata Rais! au tutatishia kura zetu! ss hatuna utamaduni wa kufata au kusimamia sheria...ni 'uyakhe kwenda mbele!'..na mtakuja kuniambia.
ReplyDelete