Na Mwantanga Ame
RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) imebainisha kuwa, bado fedha za umma zinaendelea kutafunwa na baadhi ya wasimamizi wa miradi ya maendeleo, huku wakiiacha miradi hiyo kutomalizika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir, alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akiwasilisha ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali kwa mwaka 2009/2010.
Alisema serikali katika kipindi hicho imetumia fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo ya ujenzi wa skuli, vituo vya afya pamoja na kupeleka huduma za lazima kwa wananchi, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba miradi hiyo imeshindwa kukamilika huku fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wake zikiwa tayari zimetumika na kumalizika.
Alifahamisha kuwa kutokana na hali hiyo bado lipo tatizo sugu katika Idara za serikali kufanya matumizi bila ya kuzingatia kanuni za fedha kwa wajanja hao kubuni mbinu ya kutafuna fedha za miradi ya maendeleo na hali inayochangia kushindwa kukamilika.
Alisema kuwa tatizo hilo limetokea kutokana na kutofuatwa kwa miongozo kwa mujibu wa sheria ya manunuzi hazikufuatwa wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo na kusababisha kutofikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa kwa vile huduma zilizotegemewa kupatikana kwa wananchi kukosekana.
Alisema eneo jengine ambalo limeonesha udhaifu katika ripoti hiyo ya Mdhibiti ni pamoja na udhibiti na utunzaji wa mali za serikali ambapo nyingi zimeonekana hazina udhibiti na utunzaji mzuri wa mali hizo, huku taratibu na miongozo kwa mujibu wa sheria za fedha hazikufuatwa.
Alisema mali nyingi za serikali zimekutwa zikiwa katika hali mbaya huku nyengine zikiwa zinahitaji matengenezo madogo na kuweza kutumika katika taasisi hizo kama zingetengenezwa jambo ambalo limeitia hasara serikali kutokana na kuendelea kugharamia kuzihifadhi mali hizo.
Tatizo jengine ambalo alilitaja waziri huyo ni kwa taasisi za serikali kushindwa kuandaa mpango wa manunuzi wa mwaka kwa mahitaji ya vifaa na huduma mbali mbali kama sheria namba 9 ya manunuzi ya mwaka 2005 inavyoelekeza katika kifungu cha 19 cha sheria hiyo.
Waziri huyo alisema kutokuwepo kwa madaftari ya kuwekea kumbukumbu ya mali za serikali ni dosari nyengine iliyojitokeza katika ripoti hiyo jambo ambalo litasababisha kutofahamika kwa idadi ya thamani na mali za serikali ziliopo katika taasisi za zake.
Waziri huyo pia alisema ukaguzi huo pia umebaini wizara na Taasisi za serikali hazina hatimiliki za majengo yake jambo ambalo linasababisha kutopatikana kwa uhalali wa umiliki wa mali hizo.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato waziri huyo alisema katika kipindi hicho serikali imeonekana kufanya vizuri kwa kuweza kukusanya 213,966 bilioni ikiwa ni ongezeko la shilingi Bilioni 1/= ikiwa ni makadirio ya kukusanya shilingi 212,992 bilioni kwa mwaka huo.
Hata hivyo Waziri huyo alisema bado inaonekana zipo fursa nzuri ya kukusanya mapato zaidi iwapo zitafanyika jitihada za makusudi katika kuimarisha vianzio mbali mbali vya mapato ya ndani.
Hali ya mgawanyo wa fedha Waziri huyo alisema kwa matumizi ya kawaida nayo yameonesha kuwa na mafanikio kwa vile kw mwaka huo yalifikia asilimia 95.07 ya makadirio yaliowekwa.
Matumizi ya maendeleo Waziri huyo alisema yalifikia shilingi 109.308 Bilioni ambapo mchango wa serikali ulikuwa ni shilingi 40.038 Bilioni ambazo ni sawa na asilimia 98.4 ya makadirio na fedha za wahisani ni shilingi 69.269 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 34.8 za makadirio yaliopangwa hapo awali.
Akichanganua matumizi ya fedha hizo za miradi ya maendeleo alisema Mkoa wa Kusini Unguja ulipatiwa shilingi 20,000,000, Mkoa wa Kaskazini Unguja shilingi 20,500,000, Mjini Magharibi shilingi 20,000,000, kaskazini Pemba shilingi, milioni 15,800,000 na Kusini Pemba ni shilingi 11,000,000.
Hata hivyo alilieleza baraza hilo kuwa kuna baadhi ya taasisi zimeshindwa kufanyiwa ukaguzi baada ya kutokamilisha taratibu zake za kupatikana kwa vielelezo muhimu vya matumizi iliyoyafanya.
Akitoa maoni ya Kamati ya Kuchunguza na kudhibiti hesabu za serikali na Mashirika (PAC), Mwakilishi wa Chake Chake, Omar Ali Shehe alisema serikali inapaswa kuona inazifanyia kazi ripoti hizo kwani bila ya kutekeleza hilo linaweza likachangia kuwafanya wananchi kutokuwa na imani na serikali yao.
Shehe ambae ni Mwenyekiti wa PAC, alisema hivi sasa tayari ripoti mbili zimeonesha kuwapo kwa udhaifu kwa watendaji wa serikali kushindwa kuwajibika kwa kujihusisha na ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma huku kukiwa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa jambo ambalo limekuwa likisababisha vitendo hivyo kujirudia.
“Kuepusha hali hiyo isitokee tunaitaka serikali kuzifanyia kazi ripoti hizi kwa ukamilifu wake na ripoti za ofisi ya Mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali pamoja na mapendekezo ya Kamati za baraza hili, msisitizo katika hili ikiwekwa kwa ripoti ya Kamati ya PAC “ alisema Mwakilishi huyo.
Aidha Mwakilishi huyo aliipongeza taasisi ya Mdhibiti kwa kuhakikisha inafanya ukaguzi kwa wakati na kuiomba serikali kuwaangalia watendaji wa Idara hiyo kwa kuwaongezea mishahara yao ikiwa ni hatua itayoweza kudhibiti vitendo vya rushwa.
Ripoti iliyowasilishwa ya mwaka 2008/2009 kuwapo kwa fedha zilizopotea kufikia shilingi milioni 275,767,158 za umma zililiwa kwa kuwepo kwa malipo hewa, safari feki, na stakabadhi za uongo
Suala la ubadhirifu wa mali za umma kwa ZNZ nilikua nalitegemea! na liliachawa liendelee kwa muda mrefu bila ya kuchukuliwa hatua. Kuna mpinzani alihoji,ndege ya serekali ime ...Akaambiwa kwani ya baba ake nani ile? watu wakacheka! Na mmoja akahoji jamani mali za umma..hizo, mheshimiwa mmoja maarufu akajibu ' Anasema nini huyu, yeye alitumia zaidi ya Sh.100,000,000 kutibiwa uingereza!..ah!..wakhti napita wa-allah!
ReplyDelete