Habari za Punde

WASIFU WA MAREHEMU MAULID HAMAD MAULID

Marehemu Maulid Hamad Maulid alizaliwa Kisiwani Zanzibar mnamo mwaka 1957, na kufariki jana asubuhi nyumbani kwake Jang'ombe baada ya kuugua kwa wiki kadhaa akisumbuliwa na maradhi ya moyo.

Taarifa za kifamilia zimefahamisha kuwa, marehemu Maulid Hamad alipata elimu yake ya msingi katika skuli ya Kiungani mwanzoni mwa miaka ya sitini, na kusoma elimu ya sekondari katika skuli ya Fidel Castro kisiwani Pemba.


Baada ya kumaliza masomo yake, aliajiriwa katika ofisi ya mkaguzi wa hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akiwa mkaguzi wa hesabu ( Auditor) , baadae aliamua kuacha kazi na kuajiriwa katika soko kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam, akiwa mshika fedha wa soko hilo.

Mbali na kazi hiyo katika vipindi tafauti alikua Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mabaharia Tanzania (Tanzania Seaman Union-TSU).

Marehemu Maulid Hamad alikuwa na taaluma ya uandishi wa habari na hadi anafariki alikuwa mwandishi wa habari anayefanyia kazi Kituo cha Televisheni cha ITV pamoja na Redio One akiwa hapa Zanzibar.

Marehemu pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo, Tanzania-Zanzibar (TASWA-ZANZIBAR), ambacho kimeundwa kwa min ajil ya kutoa mchango wake katika kuimarisha michezo visiwani Zanzibar kupitia vyombo vya habari.cheo ambacho hadi mauti yanamkuta alikua nacho.

Kazi yake hiyo ya uandishi wa habari ilimpatia umaarufu kutokana na ujasiri na moyo wa kujituma, ambapo pia aliitwa kuvifanyia kazi vituo mbalimbali ikiwemo redio ya Zenj FM, Hits FM, iliyokuwa Sauti ya Tanzania Zanzibar (sasa shirika la habari Zanzibar-ZBC) katika kipindi chake kinachopendwa na wengi cha Mawio.

Mbali ya hayo, pia alikuwa mchezaji mahiri wa mpira wa miguu ambaye kwa nyakati tafauti alizichezea klabu za Kikwajuni hapa Zanzibar pamoja na Nyota Nyekundu ya Dar es Salaam.

Kwa mapenzi makubwa aliyokuwa nayo, marehemu alikuwa miongoni mwa waasisi wa timu ya Taifa ya Jang'ombe ambayo aliiongoza kwa mafanikio makubwa hadi kucheza ligi kuu ya Zanzibar na kujipatia jina la 'Wakombozi wa Ng'ambo', akiwa Rais wa timu hiyo.

Aidha kwa miaka kadhaa alikuwa Msemaji wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), nafasi iliyomfanya kuwemo katika kamati ya habari ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), na pia muasisi wa Umoja wa Vilabu vya Soka hapa Nchini.

Marehemu atakumbukwa kwa ushirikiano mkubwa aliokuwa nao na wanahabari wenzake, wanamichezo pamoja na wana jamii wote, ambapo alitumia taaluma yake ya habari kuiunganisha jamii, bila woga, chuki wala upendeleo.

Kamwe hakuweza kustahmili pale alipoona watu wenye nafasi kubwa katika jamii wakiwanyanyasa na kuwadhulumu wananchi walio wanyonge, hivyo akawa tayari daima kupitia kalamu yake kuwatetea na kuwasemea wale ambao sauti zao hazikuweza kusikika, na kuhakikisha wanapata haki zao.

Kwa haya na mengine mengi, ni wazi kuwa tasnia ya habari, sekta ya michezo na jamii kwa jumla imepata pigo kubwa kwa kupoteza shujaa na mtetezi wa wanyonge.

Marehemu Maulid Hamad Maulid, ameacha Mke na watoto saba.
Kwa kuwa sote tumeguswa na msiba huu, tunawaomba wanafamilia wawe na moyo wa subra, na kutambua kuwa hiyo ni njia yetu sote, lililobaki tumuombee mapokezi mazuri na maghufira kwa Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi . AMIN.

Tanzia hii imetolewa na Chama cha Waandishi wa habari za Michezo Tanzania Zanzibar (TASWA-ZANZIBAR)
19/10/2011.

--------------
Mwinyimvua Abdi Nzukwi,
Mwenyekiti TASWA-ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.