Habari za Punde

KUTOKA BARAZANI - KODI WATUMISHI TAASISI ZA MUUNGANO WALIOPO ZANZIBAR

Haiingii hazina SMZ hadi sheria irekebishwe

Na Mwantanga Ame

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema bado serikali ya Jamhuri ya Muungano, imeshindwa kutekeleza pendekezo la Kamati ya kujadili Kero za Muungano, inayotaka kodi ya mshahara kwa watumishi wa Muungano wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar iingie katika mfuko wa hazina wa Zanzibar.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi, Mipango na Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, wakati akijibu suala la nyongeza la Mwakilishi wa Magomeni Salmin Awadh aliyetaka kujua hatua iliyofikiwa juu ya utekelezaji wa pendekezo hilo baada ya kamati ya kero za Muungano kutaka litekelezwe hivyo.


Waziri huyo alisema ingawa kamati hiyo imeweza kutoa pendekezo hilo kwa muda sasa lakini bado utekelezaji wake haujafanyika kutokana na sheria iliyopo ya fedha ya serikali ya Muungano bado haijabadilishwa.

Alisema kwa mujibu wa taarifa aliyopewa na Idara ya hazina ya Tanzania bara, serikali hiyo ya Muungano inatarajia kuwasilisha sheria hiyo katika kikao kijacho cha Bunge ili iweze kurekebishwa na ndipo utaratibu huo uanze kutumika hapa Zanzibar.

Alisema mpango utapoanza, unatarajia kuipatia serikali ya Zanzibar fedha zitazotokana na kodi hiyo ni shilingi bilioni 18 kwa mwaka kwa wastani wa bilioni 1.5.

Alisema serikali ya Zanzibar hivi sasa imekuwa ikisubiri kwa hamu kukamilika kwa sheria hiyo ili kuweza kukusanya kodi za watumishi wa Muungano wanaotekeleza majukumu yao wakiwa Zanzibar.

Taasisi ambazo zipo chini ya Muungano ni pamoja na Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Uhamiaji, Mashirika ya Posta, Simu, Benki Kuu na Makampuni ya Simu.

Akizungumzia juu ya suala la msingi lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu, alietaka kujua ni kwa nini serikali imekuwa inashindwa kuziingizia fedha Wizara za serikali wakati ikiwa tayari Baraza hilo limepitisha kasma zao jambo ambalo linachangia kutotekelezwa vyema kwa majukumu ya serikali.

Waziri Omar, alisema ni kweli tatizo hilo limejitokeza lakini lilitokana na kuchelewa kuingia kwa fedha za wafadhili kwani hadi sasa bado hawajaingiza mchango wao licha ya kuahidi kuchangia bajeti ya Zanzibar.

Alisema katika robo ya kwanza ya utekelezaji wa bajeti hiyo imeonesha hali ya ukusanyaji wa mapato ya ndani imeimarika kwa vile serikali imeweza kukusanya shilingi bilioni 48.6 ikiwa ni sawa na asilimia 90 ya lengo la shilingi 53.4 bilioni.

Alisema kati ya mapato hayo Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), imeweza kukusanya shilingi bilioni 25.9 ikiwa ni sawa na asilimia 96 ya lengo la shilingi bilioni 26.8 na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya shilingi bilioni 19.7 ikiwa ni sawa na asilimia 80.5 kwa lengo la shilingi bilioni 24.5.

Kuhusu Mapato ya Mawizara fedha zilizokusanywa Waziri huyo alisema ni shilingi bilioni 2.9 ikiwa ni sawa na asilimia 140 ya lengo la shilingi Bilioni 2.0 na kuingiza matumizi ya bakaa yake ya mwaka jana ya shilingi bilioni 4.0 ili kukidhi matumizi ya serikali.

Alisema hadi sasa serikali ya Zanzibar kwa robo ya bajeti hiyo imetumia shilingi bilioni 49.9 ambazo ni sawa na asilimia 99.5 ya lengo la shilingi bilioni 49.8 huku matumizi ya mishahara kwa muda huo imefikia shilingi bilioni 21.9 sawa na asilimia 99.6 ya lengo la shilingi bilioni 22.0.

Waziri huyo alisema kwa upande wa matumizi ya miradi ya maendeleo Waziri huyo alisema mchango wa serikali haujawa wa kuridhisha kutokana na kutoingizwa kwa fedha za wafadhili jambo lililoifanya serikali kutumia mapato yake kwa baadhi ya mambo ambayo hayawezi kusubiri.

Fedha zilizotumika katika kutekeleza hilo Waziri huyo alisema ni jumla ya shilingi bilioni 3.6 ambazo ziliingizwa katika Mawizara ya serikali ambapo kwa robo ya kwanza fedha zilizoingizwa ni shilingi bilioni 12.0.
Waziri huyo alisema tayari wamekutana na watendaji wa Benki ya Dunia kwa dhamira ya kuwaomba kuheshimu makubaliano yao ili kuweza kutekeleza maamuzi yao.

Wakati huo huo Wajumbe wa baraza la wawakilishi wameupitisha Mswada wa sheria ya kuanzishwa kwa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), na kuweka mazingira bora kwa ajili ya kusarifu, uendelezaji, Uzalishaji Biashara na Ukuzaji Karafuu na Mazao mengine ya Kilimo na mambo yanayohusiana na hayo.

Kabla ya kupitisha sheria hiyo Wajumbe hao waliendelea na kuijadili na kuhoji kwa nini serikali imeuza maghala ya kuhifadhia karafuu jambo ambalo serikali imesema suala hilo halipo na maghala yote yapo chini ya usimamizi wa Shirika hilo.

Hata hivyo Waziri, huyo aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo, kuwa haijaweka bei ya shilingi 1000 inayodaiwa kutozwa wananchi kila pale wanapokwenda kuuza karafuu zao suala ambalo limelalamikiwa na Mwakilishi wa Mtambwe, Salim Abdalla Hamad, ambapo fedha hizo hutozwa wananchi na wanunuzi wa karafuu katika vituo bila ya kuwepo maelezo yoyote.

Aidha wawakilishi hao waliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuweka vyoo katika vituo vya karafuu kutokana na huduma hizo kukosekana hasa katika vituo vya kisiwani Pemba jambo ambalo limekuwa likiwasumbua wakulima wa karafuu waendapo vituoni.

2 comments:

  1. Ehee..namna hiyo! Visiwa vinavyosifiwa kwa ustaarabu lkn vyoo havionekani kua muhimu ktk maeneo ya public?... wakumbusheni, ustaarabu sio kanzu tuu na kofia!

    ReplyDelete
  2. Huu, ni ushahidi wa wazi, kua awamu zilizopita hazikua serious ktk kutatua kero za muungano. kumbe kama wangeweza kupigia kelele suala hili la kodi za wafanyakazi wa sekata za muungano waliopo znz na likafanikiwa, mbona tungekua mbali na isingefikia leo hii kudharauliana bungeni. kwanza suala lenyewe lina 'logic' na wenzetu ni waelewa. lkn viongozi wetu(zenj) waliopita waliona bora kuomba vikosi wakati wa uchaguzi na kusahau mambo ya msingi!..Baada ya kumaliza mda wao, sasa wanashawishi w'nchi wachukie umoja wa nchi yetu...Washidwe! kwa nguvu za Mungu!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.