Habari za Punde

LUGHA HURAHISISHA USHINDANI SOKO LA AJIRA - WAZIRI

Mwashamba Juma na Kauthar Abdalla

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdalla Shaaban, amesema Zanzibar na Ivory Coast zina nafasi nzuri ya kushirikiana katika lugha ili kuwajenga vijana wa nchi hizo kumudu ushindani wa soko la ajira.

Waziri huyo alieleza hayo jana huko ofisini kwake Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar kwenye hafla fupi ya kuagana na Carna Sorro Mwakilishi wa UNDP Zanzibar anayemaliza muda wake wa utumishi.


Alisema Zanzibar inaweza kuitumia Ivory Coast nchi ambayo ni nyumbani kwa muwakilishi huyo kwa vijana wake kujifunza lugha ya kifaransa na wale wa Ivory Coast kuja Zanzibar kujifunza lugha ya Kiswahili.

Waziri Shaaban, alisema hatua hiyo ikifikiwa kwa kiasi kikubwa vijana watakuwa na upeo mkubwa wa lugha ambao utawawezesha kumudu ushindani wa soko la ajira.

Alisema vijana wengi wa Zanzibar wamekuwa wakikosa fursa muhimu ikiwemo ajira kutokana na kutofahamu vyema lugha ya kifaransa.

Waziri alisema kuwa ni wakati muafaka kwa wazanzibari kujifunza lugha mbali mbali ili kuboresha maendeleo ya nchi pamoja na kuinua vipato vyao.

Alimtaka mwakilishi huyo kuandaa programu za kielimu kati ya nchi mbili hizo ili kuliwezesha somo hilo la kifaransa kufahamika kwa urahisi kwa wanafunzi wa Zanzibar kupitia vyuo na taasisi mbali mbali.

Waziri huyo alimuahidi mwakilishi huyo kuwa atatoa ushirikiano kwa mwakilishi atakayeteuliwa kuja kuchukua nafasi yake.

Nae Mwakilishi wa UNDP, Carna Sorro, alisema amefurahishwa sana na mashirikiano mazuri aliyopewa na serikali ya Zanzibar ambayo yamemuonesha sura nzuri kwa Zanzibar na kuweza kufanya kazi kwa pamoja.

Hata hivyo alisema kuwa nchi yao inahitaji mashirikiano ya pamoja na Zanzibar na kusema kuwa hawatasita kuja kuendeleza umoja wao ulioanza kwa maslahi ya taifa.

Mwakilishi huyo wa UNDP ambae pia ni mshauri wa Rais wa Ivory Cost, amemaliza muda wake wa miaka minne wa kutumikia shirika la umoja wa kimataifa la UNDP hapa Zanzibar.

1 comment:

  1. kwanza kifundisheni vizuri hicho kiengereza, sio kuandika na kusoma tu, kuzungumza ndio kupewe kipaumbele, walimu wote wawe na uwezo wakuzungumza kiengereza, sasa hivi utaona huyo mwalimu wa somo hilo la kiegereza basi hajui kuzungumza, just ni sentences zake mbili basi anaunganisha kiswahili. KIENGEREZA NDIO LUGHA MUNAYOFUNDISHIA SKULI (SEKONDARI) ili wanafunzi waweze kufaulu mujitahidi kwa hili, kwani watoto wetu wanafeli sio kwa sababu hawana uwezo lugha ndio kikwazo kikubwa.baadae ndio mutafute hizo lugha nyingine inshaallah

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.