Na Salum Vuai, Maelezo
ZANZIBAR inatarajiwa kuwakilishwa na wachezaji watatu wa mchezo wa kunyanyua vitu vizito ya Afrika kwa timu za vijana yaliyopangwa kufanyika nchini Uganda kuanzia Novemba 21.
Wachezaji hao ambao waliagwa na Kamishna wa Michezo na Utamaduni Hamad Bakari Mshindo katika ofisi za kamisheni yake zilizoko Mwanakwerekwe, waliondoka jana kuelekea Kampala.
Vijana hao watakaoshiriki kunyanyua uzito tafauti ni Abdulrahman Said Simai ambaye ni nahodha wa timu, Abdallah Shaib pamoja na Ali Shaaban, ambao wataongozwa na Jalinus Issa, mwalimu na mjumbe wa kamati tendaji ya Chama cha Kunyanyua Vitu Vizito Zanzibar (ZAWEA).
Katika hafla ya kuwaaga wanamichezo hao, Kamishna Mshindo aliwataka kuhakikisha wanapeperusha vyema bendera ya Zanzibar kwa ushindi utakaoipa heshima nchi yao.
Aliwakumbusha kwa kuwataka wafahamu kuwa, watakapokuwa mashindanoni, hawawakilishi chama chao, bali wanaiwakilisha nchi ambayo ndiyo yenye bendera inayotambulisha hadhi na heshima yake.
“Eleweni kuwa, lolote mtakalolifanya huko litakuwa linaakisi wasfu wa Zanzibar, liwe zuri au baya, kwa hivyo muwe makini msije mkafanya mambo yatakayouvua uanamichezo wenu, kwa maneno au vitendo”, alisema Kamishna Mshindo.
“Msifanye mambo maovu yatakayowekwa katika kumbukumbu kuonesha hali ya Zanzibar”, aliongeza.
Aidha aliwaeleza kuwa, siri ya mafanikio katika mashindano, ni pamoja na kujiamini na kuzingatia nidhamu, sambama na kusoma mbinu za wapinzani kwa nia ya kuwapiku kwa mbinu mbadala.
Naye kiongozi wa msafara huo Jalinus Issa pamoja na nahodha Abdulrahman Said, walimuhakikishia Kamishna huyo kuwa, kinachowapeleka Uganda ni kulinda heshima ya nchi kwa kushindana na kuiletea medali Zanzibar.
No comments:
Post a Comment