Habari za Punde

MTUMISHI ALIYESHIKWA NA KARAFUU AJITETEA

Na Abdi Suleiman, Pemba

KUFUATIA tuhuma za kutaka kusafirisha karafuu nje ya nchi kimagendo, Mhasibu wa wizara ya Afya Pemba, Mbarouk Juma Ali, ameibuka na kudai hakuwa na lengo la kuzisafirisha karafuu hizo kinyume na matakwa ya serikali.

Mhasibu huyo, alisema kuwa, kuchelewa kuzipeleka karafuu hizo ZSTC, ni kutokana na kuchelewa kumalizika kwa zoezi la chanjo kwa watoto wadogo ambalo limemalizika hivi karibuni.


Hayo aliyaeleza alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, kufuatia shutuma zilizoelekezwa kwake za kutaka kusafirisha karafuu kwa njia ya magendo.

“Mimi ni muhasibu wa wizara ya Afya na wizara yangu ndiyo inayohusika nilikuwa nikishiriki katika chanjo kikamilifu hapa Pemba na ndio sababu iliyonifanya nichelewea kuzipeleka karafuu zangu ZSTC, sikuwa na lengo hilo”, alifafanua mhasibu huyo.

Mbarouk alifafanua kuwa, yeye hawezi kuuchukuwa uchumi wa nchi yake na kuupeleka katika nchi nyengine, kwani kufanya hivyo ni kuikosesha serikali mapato ambapo mapato hayo ndiyo yanayosaidia katika huduma mbali mbali kama miundombinu, maji safi na salama, matibabu, skuli na kilimo.

“Sitegemei hata siku moja kufanya hivyo, kwani mimi najua hali ya nchi yangu kwani nitaikosesha nchi yangu mapato”, alisisitiza Mbarouk.

Aidha alisema kuwa, shutuma zilizotolewa kwake zilikuwa na lengo la kumchafulia jina, sambamba na kukiuka majukumu yao ya kikazi kutokana na ubinafsi, choyo, utakaji wa madaraka, kujisafisha na mabaya yanayotendeka na husda.

Awali kikosi maalumu cha udhibiti wa magendo ya karafuu kisiwani Pemba, kilifanya kazi ya upekuzi nyumbani kwa mhasibu huyo na kuzikuta gunia 24 za karafuu kavu ndani ya nyumba hiyo.

Alifahamisha kuwa, Oktoba 5 mwaka huu, ameuza gunia 14 za karafuu kavu katika kituo cha ZSTC Wete, kwa risiti No: 30473 zenye kilo 659.0 zikiwa na thamani ya shilingi 9,675.000/= za kitanzania, ambapo pia anamiliki mashamba mawili makubwa ya karafuu na kambi ya vibarua katika maeneo ya Mtambwe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.