Habari za Punde

BALOZI WA UTURUKI AAGANA NA DK SHEIN ASITITIZA AZMA YA KUANZISHA SAFARI ZA NDEGE TURKISH AIRLINES IKO PALE PALE

Na Rajab Mkasaba

UTURUKI imeeleza azma ya Shirika lake la ndege la ‘Turkish Air Line’ kuanza safari zake kati ya nchi hiyo na Zanzibar hivi karibuni kuwa ipo pale pale hatua ambayo itaimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi mbili hizo pamoja na kukuza sekta ya utalii.

Balozi wa Uturuki anaemaliza muda wake wa kazi nchini Tanzania Mhe. Sander Gurbuz aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein Ikulu mjini Zanzibar.


Balozi Gurbuz ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kuaga kufuatia kumaliza muda wake wa kazi hapa Tanzania, alimueleza Dk. Shein kuwa Shirika la ndege la Uturuki limo katika mchakato wa kuanza safari zake kati ya Uturuki na Zanzibar hivi karibuni.

Alisema kuwa mbali ya kuanza safari zake kati ya Uturuki na Zanzibar tayari Shirika hilo hivi sasa limezidi kujiimarisha kwa kuleta ndege kubwa zaidi hapa Tanzania sanjari na kuongeza idadi ya safafri zake kwa wiki.

Kutokana na hatua hiyo, Balozi Gurbuz alieleza kuwa ujio wa watalii kutoka nchini Uturuki pamoja na nchi nyengine ambazo zitatumia shirika hilo kuja Zanzibar utaimarika zaidi kutokana na hazma ya Shirika hilo la ndege mara baada ya kuanza safari zake hapa Zanzibar.

Alisema kuwa mbali ya sekta hiyo nchi yake itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo.

Aidha, Balozi huyo alieleza kuwa uhusiano kati ya Uturuki na Tanzania umepelekea kuwepo kwa mashirikiano makubwa ikiwa ni pamoja na ziara mbali mbali za viongozi wa Tanzania waliofanya ziara nchini humo akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais Dk. Shein na Mawaziri wengine mbali mbali.

Alieleza kuwa kutokana na mashirikiano yaliopo safari hizo za viongozi wa Tanzania pamoja na ile ya Rais wa nchi hiyo Mhe. Abdallah Gul ambeye aliwahi kuitembela Tanzania zimezidi kukuza uhusiano na ushirikiano zaidi.

Nae Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Balozi huyo kutokana na juhudi zake alizozifanya katika wakati wote aliofanya kazi hapa Tanzania na kutoa shukurani kwa Uturuki kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania ikiwamo Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo.

Dk. Shein alieleza kuwa Uturuki na Zanzibar ina mambo mengi yakushirikiana kwa pamoja na kueleza kuwa hatua ya Shirika la ndege la nchi hiyo kuwa na azma ya kuanza safafrri zake hapa Zanzibar zitasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uhusiano.

Alieleza kuwa mbali ya kuimarika kwa sekta ya utalii kati ya Uturki na Zanzibar mara baada ya safari za shirika hilo, hata sekta ya biashara nayo itaimaarika.

Wakati huo huo Dk. Shein amefanya mazungumzo na Balozi mdogo wa Oman anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Mhe. Mansoor Nasser Al-Busaidi ambaye alikuja kwa ajili ya kujitambulisha ambapo katika mazunguzmo yao viongozi hao walieleza haja ya kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.

Kwa upande wake Balozi Al-Busaidi alimueleza Dk. Shein kuwa Oman itaendelea na juhudi zake za kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika sekta ya elimu, afya, utalii, utamaduni na nyenginezo.

Aidha, Dk. Shein kwa upande wake alisisitiza haja ya kuimarisha uhusiano wa kidugu uliopo baina ya nchini mbili hizo na kueleza kwamba Zanzibar na Oman zina historia ya karne hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kukuzwa na kuimarishwa kwa manufaa ya pande zote mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.