Habari za Punde

BALOZI SEIF AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA MIUNDOMBINU

Mratibu Wa Mradi Wa Bara Bara Za Amani-Dunga Na Mfenesini-Bumbwini Kutoka Smz Nd. Peter Jumanne Magese Akimpatia Maelezo Ya Ujemzi Wa Bara Bara Hizo Makamu Wa Pili Wa Rais Wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Alipofanya Ziara Ya Kuangalia Maendeleo Ya Ujenzi Huo.


Makamu Wa Pili Wa Rais Wa Zanzibar Balozi Seif Na Waziri Wa Mawasiliano Na Miundo Mbinu Mh. Hamad Masoud Wakifurahia Maendeleo Ya Ujenzi Wa Daraja La Mwera Linalojengwa Na Kampuni Ya Mecco.
Makamu Wa Pili Wa Rais Wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Akikagua Bara Bara Ya Mfenesini-Bumbwini Huku Akipatia Ufafanuzi Wa Ujenzi Huo Kutoka Kwa Waziri Wa Mawasiliano Na Miundo Mbinu Mh. Hamad Masoud.


Ujenzi wa Bara Bara za Dunga Mitini hadi Amani na ule wa Mfenesini hadi Bumbwini unatazamiwa kukamilika ifikapo mwezi wa tatu mwaka 2012.

Kauli hiyo imetolewa na Wajenzi wa Bara bara hizo kutoka Kampuni ya Mecco chini ya Mmiliki wake Bwana Mohd Bujet wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara ya kukagua Maendeleo ya ujenzi wa Bara bara hizo.


Wajenzi hao walimueleza Balozi Seif kwamba hatua kubwa ya ujenzi wa bara bara hizo yakiwemo yale Madaraja ya Mwanakombo , Tinga tinga na Mwera yatakuwa yamekamilika mwishoni mwa mwezi wa Febuari Mwakani.

Walisema kitakachobakia zaidi ni zile kazi ndogo ndogo za umaliziaji wa bara bara hizo.

Mratibu wa Mradi huo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Nd. Peter Jumanne Magese alisema ujenzi wa Bara bara hizo unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Bilioni 19.9.

Nd. Peter alimueleza Balozi Seif kwamba gharama hiyo zimejumuisha pia yale madaraja manne makubwa yaliyoko katika mradi huo.

Akizungumzia suala la malipo ya fidia Waziri wa Mawasiliano na Miundo mbinu Zanzibar Mh. Hamad Masoud alisema Serikali imekuwa na utaratibu wa kufanya tathmini kwa nyumba zinazoathirika kwenye ujenzi wa bara bara na baadaye wahusika kulipwa fidia zao.

Mh. Masoud alisema mpango wa malipo hayo huandaliwa mapema kadri uwezo wa serikali unavyoruhusu ukienda sambamba na wananchi wanaoathirika kwa vipando vyao ikiwemo miti ya kudumu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameelezea kuridhika kwake na hatua nzuri iliyofikiwa ya ujenzi wa bara bara hizo.

Balozi Seif alisema anaamini kwamba Kampuni hiyo ina uwezo wa ujenzi lakini kinachohitajika zaidi ni kwa wajenzi hao kuhakikisha wanazingatia umadhubuti wa bara bara hizo.

Aliwanasihi Wananchi na watumia bara bara hizo kujenga Utamaduni wa kuzitunza kwa lengo la kudumu zaidi.

“ Hatuna Utamaduni wa matunzaji katika mambo yetu mengi. Na hili limekuwa likituathiri kila mara ”. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliitembelea Bara bara ya Mfenesini hadi Bumbwini yenye urefu wa Kilo mita 13.2 pamoja na Bara bara ya Dunga hadi Amani yenye urefu wa kilomita 12.7 zinazogharamiwa na SMZ kwa mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika { ADB } wenye gharama ya shilingi Bilioni 19.9.

Balozi Seif pia aliangalia Ujenzi wa Bara bara ya Pili na Amani hadi Mtoni Jeshini ambayo inagharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikipata kuungwa mkono na Serikali ya Jamuhiri ya Muungano wa Tanzania.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
19/12/2011.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.