Habari za Punde

CCM, CUF WASHUSHA MZUKA


• Wakubali kuchukua kadi walizorejesha
• Ni baada ya kukatazwa kuvua nyavu mtando

Na Salum Vuai, Maelezo

HATIMAYE wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kile cha CUF wa kijiji cha Jambiani ambao walivisusia na kurejesha kadi, kutokana na hatua ya kuzuiwa kuvua kwa kutumia nyavu za mtando, wamekubali kusahau yaliyopita na kuchukua kadi zao.

Wananchi hao wa Jambiani Kichakanyuki na Kidenga, walifanya uamuzi huo, kupinga amri ya kuwazuia wavuvi wa kijiji hicho kuvua kwa kile kilichoelezwa uvuvi huo unachangia kuua mazalia ya samaki.


Jumla ya wanachama 470 wa CCM na 170 wa CUF, walirejesha kadi hizo kufuatia mvutano huo, sambamba na bendera za matawi ya vyama hivyo huteremshwa, na kusababisha eneo la bahari wanayovua, kuwekwa chini ya ulinzi tangu mwezi Oktoba, mwaka huu.

Muafaka huo umekuja baada ya jitihada za serikali kupitia kamati ya kijiji hicho iliyoundwa kushughulikia mzozo huo ulioanza mwezi Oktoba ambapo vijana tisa wa kijiji hicho walikamatwa na kufunguliwa kesi
mahakamani kwa kupinga amri hiyo, huku wananchi wengine wakiwaunga mkono.

Hatua ya kupigwa marufuku uvuvi katika eneo la Kichakanyuki/Kidenga, imesababisha kutokupatikana kwa samaki, huku wavuvi na familia zao wakiishi katika mazingira magumu.

Jana wananchi wa maeneo hayo waliitwa katika mkutano maalumu uliohutubiwa na Mwenyekiti wa Wazazi wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Haji Ameir, ambae aliwasifu kwa mshikamano wao, huku akiwaomba wafuate maagizo ya serikali, na kuwahakikishia kuwa jitihada zitafanywa ili kuwapatia vifaa bora vya uvuvi.

Aliwaambia kuwa, ameyafikisha matatizo yao serikalini kupitia kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ambaye ameahidi kufika kijijini huko baadae na kuzungumza nao na kuwasikiliza.

Alisema serikali inataka wananchi wake wawe wamoja na kudumisha amani na utulivu nchini ambao kila mtu anauhitaji, awe mwanachama wa CCM, CUF au vyengine na hata wale wasiokuwa na chama.

Kwa sababu hiyo, alisema ni wajibu wa serikali kuwapatia wananchi mahitaji yao na kuhakikisha wanawekewa mazingira mzuri katika kuendesha maisha yao ya kila siku.

Aidha alisema endapo mtu amekerwa, si busara kununa na kurejesha kadi ya chama chake, kwani mambo hayo yamepitwa na wakati na sasa watu wanataka maendeleo, ambayo hayawezi kuja bila kufanya kazi, lakini kwa utaratibu unaokubalika pamoja na kufuata sheria za nchi.

"Kuna matatizo mengi yanayohitaji kutatuliwa ili kuleta maendeleo hapa Jambiani, watu wamezuia bahari, wakulima wanagombana, watu wanashindwa kukosha hata maiti za wenzao, haya si mambo mazuri, katika serikali yetu ya umoja wa kitaifa", alifafanua Ameir.

Hata hivyo, alieleza kuwa, pengine nyavu zinazotumiwa na wavuvi hao si mali yao bali wanaazimwa na matajiri ambao huwapa ujira mdogo, huku wanakijiji hao ndio wanaokamatwa na kukutwa na matatizo, kiasi cha
kufunguliwa kesi mahakamani.

Aliwahakikishia kuwa, kamati yao na viongozi wa serikali, wanafanya utaratibu wa kuwapatia vifaa vya kisasa na vinavyokidhi mahitaji kutoka Idara ya Uvuvi, ambavyo alisema hawatauziwa bali watapewa bila
malipo ili waweze kuvua kwa mujibu wa sheria.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Jambiani Kichakanyuki/Kidenga (KK), Yahya Saburi Simai, akizungumza kwa niaba ya wanakijiji hao, alisema tatizo kubwa linalowakabili ni kuzuiwa maeneo yao tu huku wavuvi wa
maeneo mengine wakiachwa kuendelea na uvuvi kwa nyavu kama hizo wanazokatazwa wao.

Hata hivyo, alidai nyavu wanazotumia si za mtando kwani ni ndogo, ambapo zile za mtando zinafikia mita 75, na wakati wa kuvua lazima wavuvi watumie mitungi ya gesi.

Aidha aliishukuru serikali kwa kusikia kilio chao na kupeleka ujumbe maalumu ambao kwa wiki moja umekuwa ukifanya vikao mfululizo ili kulimaliza tatizo hilo, na kwamba wanasubiri kwa hamu ujio wa Makamu
wa Pili wa Rais, ili waeleze waziwazi matatizo yanayowakabili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.