Habari za Punde

FEREJ AKWAMA KUMPENYEZA BAUSI ZFA

Apendekeza apewe dhamana kuongoza kamati ya ligi, akataliwa

Na Salum Vuai, Maelezo

JARIBIO la Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Ali Ferej Tamim kuunda kamati ya kuendesha ligi kuu na kumpa mwanasoka veterani Salum Bausi dhamana ya kuisimamia, limegonga ukuta.

Katika mkutano wa wajumbe wa Kamati Tendaji ya chama hicho uliofanyika Disemba 25, mwaka huu kwenye ofisi za chama hicho hoteli ya Bwawani, Ferej alitoa pendekezo la kuundwa kwa kamati maalumu ya kuendesha ligi kuu na usajili kwa lengo la kuiimarisha.


Mjumbe mmoja wa kamati hiyo, ameiambia Zanzibar Leo kuwa, katika maelezo yake kwa wajumbe hao, Ferej aliwaambia kuwa, alishawahi kumsikia Bausi kupitia kituo kimoja cha redio hapa nchini, akisema
iwapo ZFA itaunda kamati hiyo na kumpa jukumu la kuiendesha, atafanya kazi hiyo kwa ufanisi.

"Sisi tumekataa pendekezo hilo kwa sababu ligi yetu haina mdhamini wakati tunahitaji fedha kutokana na mapato ya milangoni, tukiunda kamati na kumpa mtu, itabidi akusanye fedha hizo kwa niaba ya ZFA,
pengine yapo madhara yanayoweza kutokea baadae", alifafanua mjumbe huyo.

Aidha alieleza kuwa, kama chama kitaona iko haja ya kufanya hivyo, ni lazima kwanza kifanye marekebisho ya katiba, kwani haielezi kwamba ligi kuu iendeshwe kwa kupitia kampuni au kamati maalumu.

Mjumbe huyo alidai, haifai kumuamini mtu kwa kusema redioni, wala kuilinganisha ligi kuu ya Tanzania Bara, kwani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lina mdhamini wakati ile ya Zanzibar inaendeshwa bila
kudhaminiwa na hivyo haina chanzo cha uhakika cha kuingiza mapato.

Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wa mkutano huo waliozungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema kukataliwa kwa pendekezo la kuundwa kamati ya ligi kulitokana na Rais kutaka Bausi
ndio awe kiongozi wake, huku akifahamika kwa msimamo wake wa kukikosoa chama hicho hadharani.

Aidha, wajumbe hao walisema suala hilo halikuwa miongoni mwa ajenda za kikao hicho, na hivyo baada ya kupingwa, halikuchukua mjadala mrefu na wajumbe wakaendelea kujadili mambo mengine.

Kwa miaka kadhaa sasa, ligi kuu ya soka Zanzibar imekuwa ikichezwa bila udhamini, ambapo msimu huu, kampuni ya usafiri wa baharini 'Sea gull', ilitangaza kubeba dhamana hiyo, lakini hadi ligi hiyo ikiingia
mzunguko wa saba, hakuna kilichofanyika kuzihudumia timu zinazoshiriki kwa vifaa wala usafiri wa kwenda na kurudi kati ya Pemba na Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.