KATIBU Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama hicho hakina utamaduni wa kushindana kwenye magazeti.
Maalim Seif aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, katika ukumbi wa Maelezo, Kikwajuni mjini Zanzibar.
Maalim Seif alikuwa akizungumzia kuhusu hali ya mvutano ndani ya chama hicho iliyojitokeza katika siku za hivi karibuni.
Alisema hayuko tayari kujibizana na Mbunge wa Wawi Hamad Rashid, na kusema wataonana kwenye vikao halali vya chama.
Hata hivyo, alisema ndani ya CUF hakuna mgogoro. “CUF tuna katiba na hatuna utamaduni wa kushindana kwenye magazeti, tutaonana kwenye vikao halali vya chama,” alisema Maalim Seif.
Aidha alisema kwa mujibu wa katiba ya chama mwanachama yeyote anaetaka kugombea nafasi ya Ukatibu Mkuu na nafasi nyengine yoyote anaruhusiwa kujitokeza muda utakapofika.
“Haki ya kugombea ipo anaetaka agombee muda utakapofika,” alisema.
“Sijasema siingii (kwenye kinyang’anyiro cha Ukatibu Mkuu) lakini yeyote anaetaka kugombea agombee, tutaonana kwenye Baraza Kuu,” alisema.
Maalim Seif alisema CUF sio chama chake na kukanusha kwa kusema kuwa sio kweli anakataa kuhojiwa.
“Hakuna asiehojiwa ndani ya chama, sio Katibu Mkuu tu lakini hata Mwenyekiti anahojiwa, huu ndio utaratibu wa chama chetu,” alisema.
Aidha alikanusha kuwa amekuwa akimuandaa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu kushika nafasi ya Ukatibu Mkuu.
“Kama watu wana ajenda zao dhidi ya Jussa waseme tu lakini kawambia nani kuwa mimi namtayarisha kuwa Katibu Mkuu, kwani mimi naondoka?,” alihoji Maalim Seif.
Alisema nafasi anayoshika Jussa hivi sasa hakumpendekeza yeye akisema kuwa alichukua fomu kuwania nafasi hiyo yeye na Zakia Omar kwa upande wa Zanzibar na kupigiwa kura ya siri ambapo matokeo yalikuja akiwa ni mshindi.
Uchaguzi mkuu wa CUF unatarajiwa kufanyika mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment