Habari za Punde

BALOZI SEIF AKEMEA UKATILI DHIDI YA WATOTO

Othman Khamis, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amekemea kasi vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto inayoonekana kuendelea kushamiri nchini akisema inatishia amani ndani ya jamii na hapana budi kupigwa vita na makundi ya rika zote.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto yaliyofanyika Mkokotoni mkoa wa Kaskazini Unguja.



Alisema takwimu za udhalilishaji dhidi ya wanawake zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili kwa wanawake mwaka huu wa 2011 ikilinganishwa na mwaka 2010.

Alisisitiza kwamba serikali katika jitihada zake za kupambana na vitendo hivyo itahakikisha sheria zinazowalinda wanawake na watoto zinakwenda na wakati na kutoa fursa ya haki kutendeka.

“Naamini siku ambayo sisi wanaume tutaamua kuachana na vitendo hivi vya ukatili dhidi ya wanawake itakuwa ndio mwisho wa maadhmisho hayo hapa kwetu. Kwa nini tuadhimishe kitu ambacho hakipo?”. alihoji Balozi Seif.

“Suala langu kwa wanaume wenzangu tuliohudhuria hapa na wanaotusikiliza, lini tutaamua kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto?” aliuliza Balozi Seif.

Alitahadharisha kwamba wanaoendesha vitendo hivyo waelewe kwamba huo ni uovu sawa na kutangaza vita dhidi ya taifa.


Balozi Seif alisisitiza kwamba maazimio na matamko mbali mbali ya kitaifa na kimataifa yamekuwa yakitolewa na kuridhiwa na nchi mbali mbali duniani ikiwemo Tanazania ya kukomesha aina zote za unyanyasaji na ukandamizaji wa wanawake na watoto.

Balozi Seif aliliagiza jeshi la polisi kuandaa utaratibu maalum kwa watu wanaohusika na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia hasa ubakaji ili kudhibiti kuongezeka kwa vitendo hivyo.

Alisema utaratibu huo ulenge kuwaondolea dhamana wabakaji hao na kuwaagiza polisi na mahakama kuacha kutoa dhamana kwa wakorofi hao.

Akitoa taarifa Mratibu wa Polisi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamanda Hasina Ramadhan Taufiq alisema matendo ya udhalilishaji wa kijinsia ndani ya mkoa huo yamepanda kutoka 52 mwaka 2010 hadi 103 mwaka huu.

Kamanda Hasina alisema hali hiyo inazidi kila kukicha kutokana na kukosekana kwa mapungufu mengi likiwemo lile la utolewaji wa ushahidi mahakamani na kupelekea kutolewa hukumu kwa washitakiwa wawili tu mwaka uliopita na mshitakiwa mmoja mwaka huu.

Naye Mratibu wa shirika la Misaada ya Maendeleo la Action Aid, Khadija Ali Juma akitoa salamu za shirika hilo ambalo ni mshirika mkuu wa kundi la wanawake alisema taasisi yake itaendelea kusaidia wanawake kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiamini katika mazimngira wanayoishi.

Alisema Action Aid imeongeza nguvu zake zaidi za huduma kaskazini Unguja kwa vile ni mkoa ulioathiriwa na matendo ya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Katika risala yao wana jumuiya ya wanawake Mkoa huo, iliyosomwa na Katibu wake, Siti Ali Makamae walisema udhallishaji mkoani humo unaongezeka kutokana na ucheleweshaji wa hukumu kwa washitakiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.