Habari za Punde

DK SHEIN AMTUMIA SALAMU ZA POLE RAIS KIKWETE

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pole Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kufuatia maafa yaliotokana na mafuriko yaliosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha tokea juzi mjini Dar-es-Salaam.

Salamu hizo za pole alizotuma Dk. Shein zilieleza kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa, taarifa ya mafuriko yaliyotokea kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mjini Dar-es-Salaam na kusababisha baadhi ya watu kupoteza maisha na mali zao.


Kutokana na hali hiyo kwa niaba ya Rais Dk. Shein na wananchi wa Zanzibar, ametuma salamu hizo za rambirambi kwa vifo vya watu waliopoteza maisha yao.

Aidha, salamu za pole zimetolewa kwa wote waliopata hasara kwa makaazi yao kukumbwa na maji na kupoteza mali zao pamoja na kupata usumbufu mkubwa wa maisha yao.

Dk. Shein alieleza kuwa yeye pamoja na wananchi wote wa Zanzibar wanaungana na Rais Jakaya Kikwete na ndugu wote wa Tanzania Bara kuomboleza maafa hayo yalioikumba Taifa.

Sambamba na hayo, salamu hizo zimemuomba MwenyeziMungu awarehemu wote waliopoteza maisha na awape subira wafiwa wote. Pia salamu hizo zilitoa pole kwa waathirika na kuwaombea kwa MwenyeziMungu wao na Watanzania wote kwa jumla subira katika kipindi hiki kigumi.

Salamu hizo zilimalizia kwa kumuomba MwenyeziMungu kuleta rehma zaidi katika wakati huu wa mvua zikiwa zinaendelea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.