Habari za Punde

HOTUBA YA MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR KATIKA MAHAFALI YA SABA TAREHE 24 DISEMBA 201

HOTUBA YA MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR KATIKA MAHAFALI YA SABA TAREHE 24 DISEMBA 2011

Mh. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar;
Mh. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mh. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar;
Mh. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali;
Wah. Mawaziri;
Wah. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi;
Wah. Wabunge;
Mh. Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar;
Nd. Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana.

Assalaamu aleykum.

Kwanza nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa wazima na wenye afya njema.

Pili napenda kuchukua fursa hii adhimu kukushukuru wewe mheshimiwa kuwa pamoja nasi leo hii. Pamoja na majukumu anuwai ya kitaifa na ya kimataifa uliyonayo, lakini umemega muda wako na kuwa pamoja nasi katika hafla yetu hii ya mahafali ya saba, kwa hilo tunakushukuru na tunasema ahsante sana.


Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Mbele yako ni wahitimu wa SUZA wa mwaka 2010/2011 ambao wamekamilisha masomo yao katika ngazi tofauti. Wote ni 327 wakiwemo 172 wanaume na 155 wanawake. 213 kati yao utawatunukia shahada zikiwemo:

- shahada za Sanaa na Ualimu (139)
- shahada za Sayansi na Ualimu (63)
- shahada za Sayansi ya Kompyuta (Computer) (11)

82 ya wahitimu utawatunukia stashahada za Lugha na Ualimu,
18 utawatunukia stashahada za Sayansi ya Kompyuta, na
14 utawatunukia vyeti vya Sayansi ya Kompyuta.

Leo ni siku muhimu sana kwa wahitimu wetu. Wanasubiri kwa hamu kutopea tunuku zao, lakini pia wanahamu kubwa kusikiliza mawaidha yako juu ya maisha ya kazi yaliyowakabili mbele yao.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Mwanzoni mwa mwezi huu ulitutembelea chuoni na kukutana na wafanyakazi wa Chuo. Napenda kukujuilisha kwamba wafanyakazi wote wa SUZA tulifurahishwa na tulifarajika sana na ziara yako. Ulitupa changamoto nyingi za kukiendeleza Chuo, lakini pia ulitupa matumaini makubwa sana.

Ulitutaka tufanye kazi kwa bidii, tukikuze na tukijenge Chuo chetu kifikie hadhi ya kimataifa, na ulituahidi utakuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunafanikisha malengo haya katika kipindi kisichozidi miaka mitano ijayo. Tunakushukuru sana kwa azma yako hii.

Napenda kukuhakikishia, na kuihakikisha jamii ya wazanzibari kwa ujumla, Wana-SUZA tuko nyuma yako katika kuhakikisha kwamba hili litafanikiwa. Na napenda kukujuilisha kwamba tumeanza kulifanyia kazi kwa vitendo.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Mahafali haya pia yameambatana na kilele cha sherehe za SUZA za kutimia miaka 10 tokea chuo chetu kifunguliwe rasmi mwaka 2001. Dhamira kuu ya Chuo wakati kilipoanzishwa ilikuwa ni kutayarisha walimu wenye sifa ili kukuza elimu ya msingi na sekondari Zanzibar, na baadae kukitanua na kusomesha masomo mengine tofauti.

Bila ya shaka kwenye miaka 10 ya SUZA, hili limefanikiwa kwa asimilia zaidi 100. Kwa mfano, kati ya wahitimu 327 mbele yako, 284 wamesomea ualimu. Hii ni sawa na asilimia 87 ya wahitimu wote. Kwa muda wa miaka 10 ya SUZA tayari wamehitimu walimu 1260 sawa na asilimia 88% ya wahitimu wote wa SUZA.

Hii ni ishara ya kutosha kwamba wakati wa SUZA kusonga mbele umewadia. Na ndio maana katika kusherehekea miaka 10 ya SUZA, kauli mbiu yetu inasema – ni wakati wa kukua.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo
Sote tunashuhudia upanuzi mkubwa wa elimu ya juu barani Africa, lakini hususan kwa majirani zetu Afrika Mashariki. Tanzania pekee ina vyuo zaidi ya 40, Uganda zaidi ya 30, na Kenya hali ni hiyo hiyo. Ukuaji huu wa ghafla wa elimu ya juu kwa wenzetu inawezwekana unatokana na kulifikiria suala hili kwa kina na kulifanyia kazi kwa makusudi, au pengine hali hii imetokezea tu.

Vyovyote vile -- hali hii italeta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu ya juu Afrika Mashariki, pia katika soko la Ajira hasa tukizingatia mikataba yetu ya Shirikisho la Afrika Mashariki. SUALA la kulitafakari kwa kina -- sisi Zanzibar kama nchi pia tufanye nini? – tuendelee sambamba na wenzetu kutanua elimu ya juu au tusubiri kwanza??

Lakini pia tunashuhudia baadhi ya vyuo vikongwe kuwa na azma ya kuleta huduma zake Zanzibar. Hili ni wazo zuri sana, na linafaa kupongezwa. Kama Makamu Mkuu wa Chuo, lakini, najaribu kutazama kama hili linaweza kuleta athari zozote kwa Chuo kichanga kama SUZA au la:
- Tuchukuwe mfano, Chuo kutoka nje kuanzisha masomo ya Kilimo Zanzibar, kwa udogo wa visiwa vyetu kweli kutakuwa na haja ya SUZA pia kuanzisha masomo hayo?. Mfano mzuri – ni masomo ya Sheria – SUZA tulichelewa!
- Jee nitaweza kuwazuia walimu wangu SUZA ikiwa vyuo kama hivi vitakuja na mishahara yao mikubwa zaidi ya ile ya SUZA?
- Lakini la mwisho, serikali ina uwezo wa kutoa masomo ya SUZA kwa wananchi wake hata bure, jee fursa udhibiti wa ada kwa vyuo hivi utakuwepo ili wengi wafaidike?.

Nadhani na haya pia ni ya kuyawaza. Lakini sisi SUZA tunasema – TUSICHELEWE -- huu ndio wakati muafaka kabisa wa SUZA kukua.

Huu si wakati tena wa Chuo Kikuu cha Taifa kuendelea kuwa na vitengo viwili tu vya taaluma, au kuendelea kusomesha ualimu tu!


Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Katika kutekeleza kivitendo kauli yako uliyoitoa ulipotutembelea hivi karibuni ya kukikuza Chuo, SUZA tumeanza kuzingatia masomo mengine, yasiyokuwa ya ualimu, ambayo ni muhimu sana katika kuleta maendeleo ya nchi yetu kwa kasi zaidi, na katika kuwasidia vijana wetu kuweza kunufaika na ajira nyengine ndani na nnje ya nchi.

Muda si mrefu, Chuo chetu kinatarajia kuanzisha
- Skuli ya Elimu
- Skuli ya Sayansi za Maumbile na Sayansi Jamii
- Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni
- Skuli ya Elimu Endelevu na Ujuzi.

Vilevile, tunadhamiria kuanzisha
- Kituo cha Kuendeleza na Kukuza Kiswahili
- Kituo cha Tafiti za Mambo ya Bahari na Mazingira
- Kituo cha Utafiti na Masomo ya Uzamili na Uzamivu

Mapendekezo ya mabadiliko haya yatakuwa ni awamu ya kwanza ya kukikuza Chuo. Katika awamu nyengine, ambazo hatutegemei kutokea muda mrefu kutoka sasa, tunatarajia kuanzisha masomo mapya mengine kama vile masomo ya Kilimo, Udaktari na Sayansi za Afya, Teknolojia za Mawasiliano na Habari, Utalii, na Biashara, nk. Mabadiliko haya yatafanyika kwa kuzingatia ushauri na maelekezo yako, na miongozo ya baraza letu la Chuo.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Kwa kutekeleza majukumu yetu katika jamii, pia inatoa masomo ya muda mfuki kupitia Taasisi ya Elimu Endelevu ya SUZA. Kwa mfano, wahitimu wa taasisi hii kwa mwaka huu pekee wamefikia 3128. Huu ni mchango mkubwa kwa jamii na utaendelea kuhitajika. Ili kukuza mchango huu, SUZA itaandaa mipango mahsusi ya kujidhatiti katika kutoa masomo haya kwani wengi kati ya vijana na jamii ya wazanzibari, kwa sasa, huwa hawana uwezo wa kujiunga na masomo ya juu moja kwa moja.

Lakini pia SUZA inafungua milango yake ili tuwe karibu zaidi na jamii. Tunaandaa mikakati ya kushirikiana na jumuiya za kiserikali na zisizo za kiserikali katika kutatua changamoto zetu kwa kufanya tafiti.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;

Mbele yetu kunachangamoto mbalimbali. Kati ya changamoto hizo kubwa zaidi inayotukabili ni ya rasilimali watu hasa upande wa Taaluma. Nyengine ni uhaba wa majengo. Kwa mfano, ni vyema sana Skuli ya Elimu Endelevu na Ujuzi iwepo karibu na jamii ili waweze kuifikia kirahisi na kunufaika nayo. Hapa Vuga tayari tuna uhaba wa majengo kwa ajili ya Skuli hii.

Hata hivyo, kuhamia kwenye Kampasi mpya Tunguu kutaweza kusaidia kupunguzana hatimae kuondosha tatizo hili. Lakini pia ni imani yetu kwamba kwa mashirikiano ya pamoja baina yetu, na kwa kizingatia nia yako ya dhati katika kukiendeleza Chuo, tutaweza kukabiliana na changamoto hizi na pia kuvishinda vikwazo vyengine vitakavyojitokeza kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;

Si muda mrefu utawatunuku vyeti, stashahada na shahada wahitimu wa mkupuo wa saba wa mwaka 2011 na kutoa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi, wafanyakazi bora, wafanyakazi waanzilishi wa Chuo, na wahisani mbali mbali waliokisaidia Chuo katika miaka 10 iliyopita.

Kwa kumalizia napenda kuwapongeza wahitimu wetu leo hii, haya ni matunda ya juhudi zenu. Pia sitowasahau watunukiwa wa shahada za heshima za Udaktari -- Hii ni mara ya kwanza kwa SUZA kutoa shahada za aina hii. Na tumelazilazimika kufanya hivi kwa kuthamini michango yenu mikubwa kwa Chuo na jamii kwa ujumla.

Nasaha zangu kwa wahitimu wetu wa SUZA: Baada ya hatua hii, mtaingia katika ulimwengu na mazingira ya kazi. Ile bidii mliyoifanya wakati wa masomo, uaminifu, na moyo wa kufanyakazi mliokuwa nao, lazima muendelee kuwa nayo katika sehemu zenu za kazi ili na huko mfanikiwe. Lakini pia muondoshe ile dhana ya kuletewa ajira. Katika karne hii ya 21, upatikanwaji wa ajira imekuwa ni changamoto kubwa ulimwenguni kote. Ni wajibu wenu kuwa na mawazo ya kujitengenezea kazi zenu wenyewe. Na mnapopata fursa za kazi, basi musiwe wachaguzi wa kazi hizo!.

Kabla sijamaliza, napenda kutoa shukrani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wake mkubwa katika kukiendeleza Chuo, na pia kwa taasisi na wahisani wote wanaochangia kwenye shughuli za Chuo. Wapo wengi, na nitawataja wachache waliokuwa pamoja nasi kwa muda mrefu, nao ni; Benki ya Dunia, Kundi la Makampuni ya Bakhresa, UNESCO, Ubalozi wa Marekani, Ubalozi wa Ufaransa, Mamlaka ya Elimu Tanzania, DFID, COTUL, UNDP, American Council, Book Aid, nk

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;

Mwisho, kwa mara nyengine tena tunakushukuru kwa dhati kabisa kwa kuwa nasi kwenye Mahafali haya ya Saba.

Ahsanteni sana.

2 comments:

  1. TUMEONA JUHUDI ZAKO PROFESSA RAI,TUNATARAJIA MENGI ZAIDI YA HAYO BADAE MUNGU AKIPENDA
    ILA CHUO TUNATAKA KIWE NA WIGO KATIKA KUWEKEZA CAMPUS ZAKE KATIKA PEMBE ZOTE ZA ZANZIBAR ILI KUONDOA USUMBUFU KWA WANAFUNZI,
    KUTOKANA NA HUDUMA DUNI ZA USAFIRI KATIKA NCHI YETU.
    MUNGU IBARIKI ZANZIBAR

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.