Wananchi wa Mkoa wa Lindi wakimkaribisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kwa ngoma ya asili mara baada ya kuwasili Mkoani humo kwa ziara ya siku nne.
Hassan Hamad (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar ina nafasi nzuri ya kujiendeleza kiuchumi baada ya kufanikiwa kumaliza migogoro ya kisiasa iliyokuwa ikiikabili kwa muda mrefu.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar ina nafasi nzuri ya kujiendeleza kiuchumi baada ya kufanikiwa kumaliza migogoro ya kisiasa iliyokuwa ikiikabili kwa muda mrefu.
Amesema Zanzibar ilikuwa ikitumia muda mrefu na fedha nyingi kushughulikia migogoro ya kisiasa jambo ambalo kwa sasa halina nafasi, na kwamba ni muda mzuri wa kushugulikia maendeleo ya nchi.
Maalim Seif ameeleza hayo katika Hoteli ya Oceanic Mkoa wa Lindi mara baada ya kuwasili katika Mkoa huo kwa ziara ya siku nne na kupokea taarifa ya Mkoa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe.LUDOVICK MWANANZILA.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesema katika kipindi kifupi tangu kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa za maendeleo ikiwa ni pamoja kunyanyua kiwango cha mishahara kwa watumishi wa umma sambamba na kuongeza bei ya zao la karafuu kutoka shilingi 3000 hadi 15,000 kwa kilo.
Amefahamisha kuwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla inazo fursa nyingi za kukuza uchumi wake kutokana na rasilimali nyingi zilizopo zikiwemo bahari, ardhi yenye rutba na misitu, na kuwataka wananchi wa Lindi kuunda vikundi vya ushirika ili waweze kupatiwa misaada ya kujiendeleza kiuchumi.
“Tuna kila sababu ya Tanzania kuendelea ikiwa tutajipanga vizuri kutokana na rasilimali tulizonazo”, alisema.
Ameongeza kuwa uwezekano wa kupiga hatua za haraka za maendeleo upo iwapo watendaji watajipanga na kuweka mikakati imara ambayo pia itasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana kwa kuwawezesha kufanya kazi katika sekta tofauti zikiwemo viwanda, kilimo na uvuvi.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe.LUDOVICK MWANANZILA amesema mkoa huo una rasilimali nyingi lakini bado hazijawanufaisha ipasavyo wananchi wa mkoa huo, na kutoa mfano wa gesi ya Ngorongoro ambayo imekuwa ikiunufaisha zaidi Mkoa wa Dar es Salaam.
Rasilimali nyengine muhimu alizozibainisha ni pamoja na mbuga ya Seluu “Seluu Game Reserve” ambayo imekuwa na wanyamapori wengi ambao ni kivutio kikubwa cha watalii, pamoja na kuwa na madini mengi na misitu ambayo inahitajika sana katika soko la ndani na nje.
Amesema Mkoa huo umekuwa ukikumbwa na migogoro hasa kwa wakulima wakati unapofika msimu wa mauzo ya korosho na Ufuta, na kwamba watajifunza kutoka Zanzibar ili kuondosha migogoro hiyo ambayo haina manufaa kwa upande wowote.
Amesema wananchi wa Mkoa huo ambao asilimia 85 wanategemea kilimo hasa cha korosho na ufuta, wamekuwa wakikabiliwa na matatizo kadhaa yakiwemo kipato kidogo na kupelekea wakaazi wake kuendelea kuwa maskini .
Amefahamisha kuwa wananchi wa mkoa huo bado wanatumia zana duni za kilimo, uvuvi na teknolojia, mambo yanayopaswa kuzingatiwa ili kwenda sambamba na wakati ulipo wa maendeleo ya sayansi na Teknolojia.
Aidha Mhe. MWANANZILA amesema serikali ya Mkoa inaendelea na juhudi za kuwahamasisha wananchi kuongeza maeneo ya kilimo na uzalishaji kwa lengo la kuwakomboa na umaskini unaowakabili.
Hata hivyo Mkuu huyo wa mkoa amesema kumekuwa na maendeleo mazuri katika baadhi ya maeneo hasa katika sekta ya elimu na uhifadhi wa mazingira ya bahari na ardhini.
Kuhusu siasa Mhe. MWANANZILA amesema Serikali ya Mkoa huo itajifunza kutoka Zanzibar kutokana na mafanikio yaliyopatikana baada ya vyama vikuu vya kisiasa kuamua kukaa pamoja na kufanya kazi kwa pamoja.
Amesema Mkoa huo umekuwa ukikumbwa na migogoro hasa kwa wakulima wakati unapofika msimu wa mauzo ya korosho na Ufuta, na kwamba watajifunza kutoka Zanzibar ili kuondosha migogoro hiyo ambayo haina manufaa kwa upande wowote.
Hassan Hamad (OMKR)
No comments:
Post a Comment