MFANYABIASHARA Mohammed Raza Dharamsi, ameongoza katika kura za maoni kwa wanachama CCM Jimbo la Uzini, kumpa kura 1,963, kuwania nafasi ya Uwakilishi ya Jimbo juzi.
Mwakilishi wa zamani Jimbo hilo, Tafana Kassim Mzee, amepata kura 79.
Hali hiyo imejitokeza katika kura za maoni kwa wanachama wa CCM zilizofanyika juzi katika matawi ya CCM 16 ya Jimbo la Uzini, ikiwa ni hatua ya kutafutwa mgombea wa Chama hicho ataeingia katika
kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Uwakilishi wa Jimbo la Uzini.
Uchaguzi huo unakuja baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo, Mussa Khamis Silima kufariki dunia pamoja na Mkewe walipokuwa wakielekea katika shughuli za Bunge Mjini Dodoma.
Kutokana na tukio hilo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar, imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Februari mwaka ujao.
Tafana aliwahi kuwa Mwakilishi kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita na aliingia katika kinyang’anyiro hicho kwa mara ya pili lakini alibwagwa na wanachama wa CCM wa matawi hayo katika kura za maoni za uchaguzi Mkuu uliopita baada ya kushika nafasi ya pili.
Uchaguzi huo ambao umewashirikisha wanachama wa CCM katika matawi ya Pagali, Ghana, Kiboje, Mpapa, Mchangani, Bambi na Uzini.
Mengi ya matawi hayo wakati uchaguzi huo ukifanyika ulionekana kwenda kwa amani huku wanachama hao rika ya vijana kuonekana kuwa na shauku ya ushindi kwa Raza baada ya kupita katika viunga vya Jimbo hilo kushangiria.
Hali hiyo ilizidi kupamba moto baada ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Uzini, kumtangaza Raza kuongoza kura hiyo baada ya kupata kura 1,963 na kufuatiwa na Othman Ali Maulid, aliyepata kura 625 na Khalifa Salum Suleiman kupata kura 560.
Kutokana na ratiba ya NEC baada ya kufanyika kwa kura hiyo matokeo yake yanatarajiwa kufikishwa katika kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili itayokaa kesho.
Baada ya Kamati hiyo, vikao vyengine ambavyo vinatarajiwa kukaa ni cha Kamati ya Siasa ya Wilaya inayotarajiwa kufanyika Disemba 14, Kamati ya Siasa ya Mkoa Disemba 17, Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya NEC Disemba 20 mwaka huu na kufuatiwa na Kamati Maalumu ya NEC, itayokuwa
Disemba 24.
Aidha, Sekretarieti ya NEC itakutana Januari 4 na 5 na Kamati Kuu ya CCM kumthibitisha mgombea ataeteuliwa itakaa Januari 7 na 8.
Hongera sana. Kila la kheri. Mdau Marekani
ReplyDelete