Habari za Punde

USHIRIKINA WAONGEZA UDHALILISHAJI KASKAZINI UNGUJA

Na Juma Khamis

ONGEZEKO la vitendo vya ubakaji katika mkoa wa Kaskazini Unguja pia linasababishwa na imani za kishirikika, ambapo wanaume huwatumia waganga wa kienyeji kuwapata wanawake kirahisi.

Hiyo ni kwa mujibu wa Afisa Wanawake na Watoto katika mkoa huo, Mwanajuma Kassim Makame.
Alisema ingawa ripoti ya utafiti wanaofanya kuhusiana na ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia haijakamilika, lakini wanawake wengi waliohojiwa walisema waliingia kwenye mtego wa kuingiliwa bila hiari yao tena na mwanamme ambae alishawahi kumkataa.


“Tumegundua kuwa wanaume wanawatumia waganga wa kienyeji kuwafanyia dawa ili kuwapata wanawake kirahisi,”alisema wakati wa mkutano ulioandaliwa na TAMWA.

Utafiti huo unafanywa kufuatia agizo lililotolewa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kutokana na mkoa huo kukithiri kwa vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa wanawake.

 Lakini alisema utafiti huo pia umegundua kuwa matukio mengi ya mimba hayatokani na wanawake kuingiliwa kwa nguvu (kubakwa)kwani wanawake wengi waliohojiwa walisema ama wamependana, vishawishi vya pesa na hali ngumu za maisha katika familia zao.

Hata hivyo, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la UNICEF kuhusu ukatili dhidi ya watoto Zanzibar, visiwa vya Zanzibar kuna kiwango kikubwa cha ukatili na udhalilishaji dhi.

Ukatili huo ni pamoja na ubakaji, kulawiti, ni pamoja na ajira mbaya, kukatisha matuzo, kutorosha, mimba na ndoa katika umri mdomdogo. Asha Ali kutoka kituo cha mkono kwa mkono alisema watoto wane hadi
watano waliofanyiwa ukatili wanafikishwa katika kituo hicho kilichopo hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kupimwa.

Lakini alisema idadi hiyo ni wale wanaofikishwa hospitali tu lakini kuna watoto wengi ambao wanakatiliwa lakimi hawapati huduma hiyo.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari, Meneja wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) kanda ya Zanzibar, Ali Shaaban alisema wakati umefika kwa vyombo vya habari kuhakikisha matatizo ya watoto hayaishii kwa kusuluhishwa.

Alisema utetezi wa nguvu unahitajika ili kumkomboa mtoto na ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.

Mapema Ali Saleh (Albato) akichambua sheria ya mtoto namba 6 ya mwaka 2011, alisema mtoto aliedhalilishwa mawazo yake yanadumaa kwa muda wa miaka 15 kama hatapatiwa matibabu ya mapema.

Aliwataka wahariri kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mapambamo hayo kwa kuhoji kila kitu ambacho kimeanzishwa katika sheria hiyo ambacho hakijatekelezwa.

Pamoja na mambo mengine yenye manufaa kwa mtoto sheria hiyo inaagiza kuundwa kwa mahakama maalum ya watoto, sehemu maalum za kuwatunza watoto watakaopewa adhabu, ambayo mazingira yake yatakuwa rafiki kwa watoto.

Aliiomba serikali kuharakisha kuunda kanuni za sheria hiyo ili utekelezaji wake uweze kufanyika kwa haraka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.