Spika wa Baraza la Wawakilsihi Zanzibar Pandu Ameir Kificho akizungumza katika maadhimisho hayo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Fereji akizungumza katika maadhimisho hayo.
Watu wenye ulemavu tofauti wakishiriki maandamano ya maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani yaliyofanyika kitaifa katika eneo la Mahonda Wilaya ya Kaskazini B Unguja. Picha na Hassan Hamad (OMKR)
Hassan Hamad (OMKR)
Watu wenye ulemavu Zanzibar leo wameonesha umahiri wao na kuwashangaza wananchi waliohudhuria maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani yaliyofanyika kitaifa katika eneo la Mahonda Wilaya ya Kaskazini B Unguja.
Wameanza kuonesha umahiri kwa kushiriki maandamano yaliyowahusisha watu wenye ulemavu wa aina tofauti na kupokelewa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Pandu Ameir Kificho ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
Vijana wa kike wawili wasioona waitwao Awena na Jamila kutoka skuli ya Kisiwandui Zanzibar ndio waliowashangaza watu wengi zaidi baada ya kughani utenzi kwa sauti mwanana ulioandikwa kwa hati za NUKTA NUNDU yaani “Brails”.
Katika utenzi huo vijana hao wameelezea usumbufu wanaoupata kutokana na mazingira yasiyo shirikishi kwa watu wenye ulemavu wa aina mbali mbali.
Hivyo, wameiomba serikali na taasisi binafsi kuajiri wakalimani wa lugha ya alama katika taasisi zao ili kurahisisha mawasiliano na huduma kwa watu wenye ulemavu.
Baadaye kikundi cha ngoma ya Viziwi kilichowajumuisha vijana wa kike kwa kiume walitoa burdani ya ngoma kwa washiriki wa maadhimisho hayo na kuwafanya kutoamini kile kilichokuwa kikiendelea mbele yao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibara Fatma Abdulhabib Fereji ambaye ofisi yake ndiyo inayohusika na masuala ya watu wenye ulemavu amewahakikishi wananchi kuwa serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapatiwa fursa na haki sawa za kimaendeleo na kushirikishwa kikamilifu katika shughuli hizo.
Amesisitiza kuwa watu wenye ulemavu wanaweza kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo iwapo watawezeshwa.
Kwa upande wake Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Pandu Ameir Kificho ametaka watu wenye ulemavu wathaminiwe utu wao kama walivyo watu wengine na kutendewa haki kadri inavyostahiki.
“Kila mmoja anastahili heshima, na sisi sote tukumbuke kuwa ni walemavu watarajiwa na hizi ni kudra za Mwenyezi Mungu”, aliasa kificho.
Katika risala ya watu wenye ulemavu iliyosomwa na kijana Rashid Ali Muhidin mwenye ulemavu wa viungo ambaye pia ni mwanafunzi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu, wamebainisha changamoto mbali mbali zinazowakabili na kuiomba serikali kuzitafutia ufumbuzi.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na majengo yasiyo rafiki kwa watu wenye ulemavu, ugumu wa maisha, tatizo la wakalimani wa lugha ya alama pamoja na upungufu wa nafasi za masomo ya elimu ya juu na ajira kwa watu wenye ulemavu.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, zaidi ya asilimia 15 ya watu wote duniani wanaishi na ulemavu ambapo mkoa wa Kaskazini Unguja umesajili zaidi ya watu 1000 wenye ulemavu tofauti.
No comments:
Post a Comment