Na Mwandishi maalum, Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete jana alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Marekani George W. Bush ambaye yuko katika ziara ya siku sita nchini Tanzania.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, viongozi hao wamezungumzia jinsi Taasisi ya Bush ya George W. Bush Institute for Global Health, inavyoweza kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na changamoto kubwa za sekta ya afya na hasa magonjwa ya saratani.
Bush ambaye anafuatana na mkewe Mama Laura Bush alimweleza Rais Kikwete mipango ya taasisi yake katika kupambana na ugonjwa wa kansa ikiwa ni pamoja na jitihada za kupima, kuzuia na chanjo.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Mama Salma Kikwete, Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo kumweleza Bush jitihada za serikali yake katika kupambana na magonjwa yanayoua watu wengi ikiwemo malaria, ukimwi na saratani, magonjwa ambayo mapambano yake Bush alichangia sana kifedha alipokuwa madarakani.
Rais Kikwete pia alitumia nafasi hiyo kumweleza Bush kuhusu mipango mingine ya maendeleo inayosaidiwa na Marekani ikiwa ni pamoja na mpango mkubwa wa ujenzi wa miundombinu chini ya Mpango wa MCC.
Rais Bush na familia yake wako katika ziara ya Afrika na mbali ya Tanzania wanatembelea pia Ethiopia na Zambia.
No comments:
Post a Comment