Habari za Punde

WAZAZI MLENGE ELIMU YA KWA WATOTO - MAMA ASHA

Mwantanga Ame

MKE wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Seif Iddi, amewataka wazazi kutoridhika na elimu ya maandalizi ya watoto wao na badala yake wasimamie kuwapa elimu ya juu ikiwa ni hatua itayowawezesha kuwa na msingi mzuri wa kumudu maisha yao hapo baadae.

Mama Asha aliyasema hayo jana wakati akitoa nasaha zake kwa Walimu na Wazazi walioshiriki katika sherehe ya siku ya Wazazi kwa wanafunzi wa skuli ya Kidutani Mjini Zanzibar.


Alisema wazazi wanapaswa kuona umuhimu wa kusimamia elimu kwa watoto wao kwenda elimu ya juu kutokana na hivi sasa baadhi yao kuwaacha kuwashughulikia zaidi baada ya kumaliza elimu ya msingi.

Alisema mafunzo ya elimu ya msingi ni moja ya ngazi nzuri itayomuwezesha mtoto kuwa katika hali nzuri ya pale mtoto atapoendelezwa na haipaswi kuona wanaridhika na kiwango hicho na badala yake wajitolee kuwasomesha zaidi.

Alisema taifa lolote litajengwa kwa ujuzi wa kinadharia na kivitendo, ndio maana serikali imekuwa ikisisitiza suala la kuwapatia watoto elimu ili kuhakikisha inawawekea mazingira bora ya baadae.

Kutokana na hali hiyo Mama Asha alisema mchango wa wazazi ni moja ya jambo la msingi katika kuona wanasaidiana na serikali kwa kuunga mkono baadhi ya mambo inayoamua katika kuweka mazingira bora ya utoaji wa elimu ya maandalizi.

Alisema inasikitisha hivi sasa kuona katika skuli nyingi za maandalizi kumekuwa na kilio cha wazazi kushindwa kulipa ada za masomo kwa kawaida jambo ambalo limekuwa linapunguza ari ya walimu katika kutoa mafunzo yao.

Alisema tatizo hilo limekuwa likichangia kukosekana kwa vifaa vya msingi katika kutoa mafunzo huku watoto wakiwa wanakosa utulivu wakiwa skuli.


“Wazazi jamani turejeshe utamaduni wa kuchangia elimu ili mazingira ya skuli zetu yaimarike nah ii itayosaidia watoto kusoma katika mazingira bora” alisema Mama Asha.

Hata hivyo aliwataka wazazi wasiwafanye watoto wao kama barua za posta kwa kuwakacha kwa muda mrefu wakiwa tayari wamemaliza muda wa masomo jambo ambalo linaweza kuwasababishia kupata madhara.

Vile vile, Mama Asha, aliwaomba walimu wa Skuli hiyo kuona wanawatumia vyema viongozi wao wa Jimbo ili waweza kuwasaidia kutatua matatizo yao.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mwanaidi Saleh, aliwaomba wazazi wa watoto wanaosoma katika skuli hiyo kuendelea kutoa michango yao ili kuimarisha skuli hiyo.

Aidha, Katibu huyo aliahidi kuona Wizara ya Elimu, inaendeleza kutoa misaada zaidi ili skuli hiyo iweze kwenda vyema na kuwa na vifaa vya kisasa.

Mbunge wa Jimbo la Mji Mkongwe Mohammed Sanya, akitoa salamu zake alisema suala la kulinda haki za watoto ni moja ya jambo la msingi ili nao waweze kushiriki kuijenga Zanzibar, jambo ambalo litawasaidia kuwajenga kuwa uzalendo.

Mbunge huyo amekubali kulibeba deni la mmoja ya watu ambao wanaidai skuli hiyo la shilingi milioni 1,000,000 na kuahidi kutoa mchango wa shilingi milioni 2,000,000 kupitia mfuko wa Jimbo pamoja na kuwapatia vyakula wanafunzi wa skuli hiyo.

Akisoma risala ya Walimu, Mwalimu Zainab Bakari, alisema skuli hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbali mbali likiwemo jengo la kitega uchumi la skuli hiyo kutokana na hivi sasa kuchakaa na hivi sasa linahitaji shilingi milioni 39,000.

Alisema hivi sasa wamepata mkopo wa shilingi zaidi ya milioni 4,000,000 ambazo zimetumika kwa ajili ya kuifanyia mabadiliko madogo katika ukumbi wa skuli hiyo ili uendane na wakati.


Mapema wanafunzi wa skuli hiyo wakisoma risala yao wameomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia vifaa vya msingi vitavyowawezesha kupata mafunzo yao katika mfumo wa teknologia ya kisasa ili waweze kwenda na wakati.

Aidha, wanafunzi hao pia waliwataka wazazi wao kuona wanatimiza wajibu wao kwa kuwalipia ada kwa wakati pamoja na kuwaondosha skuli mapema baada ya kumaliza masomo yao kutokana na baadhi yao hujisahau kiasi ambacho hukaa muda mwingi bila ya kuchukuliwa.

Katika sherehe hiyo Mama Asha, amechangia shilingi 400,000 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa ukumbi huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.